Dk Biteko ataka wananchi wasichague kazi, ahimiza bidii kazini
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko akizungumza na wananchi wa kijiji cha Bufanka wilayani Bukombe mkoani Geita leo Juni 8, 2024.
Muktasari:
- Kwa mujibu wa Naibu Waziri Mkuu, siri ya mafanikio ni kuushinda ubaya kwa wema, kuepuka kujibizana na wanaokusema vibaya, kufanya kazi kwa bidii na mwishowe mafanikio yataonekana.
Geita. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema pamoja na maendeleo yanayoletwa na Serikali kwenye jamii, ni wajibu wa mwananchi mmoja mmoja kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo na kujikwamua kiuchumi.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Bufanka kata ya Bugelenga wilayani Bukombe mkoani Geita, Biteko amewataka wananchi kutochagua kazi na badala yake hiyo waliyonayo waifanye kwa bidii zote ndipo watakapoona mafanikio.
“Usidharau kazi yako, anayefuga kuku afuge kwa bidii, walioko ofisini wafanye kwa bidii na anayefanya biashara vivyo hivyo kila mtu afanye kwa bidii,” amesema Dk Biteko.
Akizungumzia maendeleo yaliyoletwa Bukombe, Biteko ambaye pia ni mbunge wa jimbo hilo, amesema kwa kipindi cha mwaka mmoja Serikali imetoa kiasi cha Sh79 bilioni kwa ajili ya shughuli za maendeleo ikiwemo afya, elimu, maji na miundombinu ya barabara.
Amesema wakati akichaguliwa 2015 wilaya hiyo ilikuwa na zahanati nne na vituo vya afya viwili na kata nne hazikuwa na shule ya sekondari lakini sasa vituo vya kutolea huduma za afya vimeongezeka na kufika 25.
Aidha, zimejengwa shule mpya saba za sekondari na msingi mpya 11, huku mtandao wa barabara ukiongezwa kutoka km 256 hadi kilomita 1,400.
Hata hivyo, amesema Serikali imedhamiria kujenga Barabara ya Ushirombo Katoro kwa kiwango cha lami na tayari upembuzi yakinifu umeanza.
Katika hatua nyingine Dk Biteko amesikitishwa na utoro wa wanafunzi shuleni na kuwataka wazazi na walezi kuzingatia elimu kwa kuwa ndio ukombozi wao kwa miaka ijayo.
“Hakuna aibu ninayoiona kama mkuu wa wilaya anavyosimama na kusema anasaka watoto kwa kuwa wameacha kwenda shule. Ni aibu Rais amejenga shule nyingi ili watoto wetu wasome niwaombe wale wanaoficha watoto wawatoe waende shule, huwezi kuona faida sasa lakini kesho utaona faida ya kusoma,” amesema.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Bukombe Paskasi Muragili, akitoa salamu za wilaya amesema moja ya changamoto ni utoro uliokithiri wa wanafunzi na kwa sasa anafanya kazi ya kuwasaka ili kuhakikisha wote wanahudhuria.
Akizungumza katika mkutano huo, Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi Dk Festo Dugange amesema Serikali imetekeleza miradi mbalimbali kwenye wilaya hiyo ikiwemo ukarabati wa hospitali ya wilaya uliogharimu Sh900 milioni.
Pia wamejenga jengo la dharura pamoja na ununuzi wa vifaa na kwamba kwa sasa wanatekeleza ujenzi wa jengo la watoto wachanga linalojengwa kwa Sh500 milioni na kwa kipindi cha miaka mitatu watumishi wa kada ya afya 110 wameletwa Bukombe.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela amesema watendaji wa Serikali, ni watumishi wa wananchi na ni wajibu wao kuwatumikia na kuwatendea haki pamoja na kutafuta suluhu ya changamoto zinazowakabili.