Dk Gwajima ataka uhuru kwa wanahabari

Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima. Picha na Habel Chidawali

Muktasari:

  • Amesisitiza wanahabari kupewa ushirikiano na uhuru wa kuandika alimradi wasimame kwenye ukweli.

Dodoma. Wakurugenzi na watoa habari katika taasisi za umma, wamekumbushwa wajibu wa kushirikiana na waandishi wa habari kwenye maeneo yao kukubali kuandikwa kwa wasiyoyapenda alimradi yawe na ukweli ndani yake.

Kingine ametaka wakurugenzi kutenga bajeti katika maeneo yao kwa ajili ya kusaidia makuzi na lishe kwa watoto, ili kusaidia kujenga Taifa imara na lenye misingi mizuri kuanzia ngazi ya chini.

Wito huo umetolewa leo Jumatatu Desemba 10, 2023 na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Doroth Gwajima wakati akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano wa siku tatu kuhusu makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto.

Mkutano huo wa siku tatu umeandaliwa na mashirika ya Children In Crossfire,TECDEN na Muungano wa Klabu za Waandishi wa habari Tanzania (UTPC).

Waziri Dk Gwajima amesema hakuna sababu ya kuwaonea wivu na kuwanyima habari waandishi na kwamba viongozi wasipende kuandikwa kwa mrengo wanaotaka wenyewe bali ufike wakati wapokee hata kile wasichokipenda,alimradi  kimeandikwa kwa ukweli na usahihi.

“Tusiwaonee kijicho pembe wanahabari, tuwape nafasi ya kuandika wanachoona ni habari hata kama sisi hatupendi, lakini tusiwanyime habari  katika kutusaidia,” amesema Dk Gwajima.

Awali Mkurugenzi wa UTPC, Keneth Simbaya alimwambia Waziri namna waandishi wanavyopitia kwenye magumu ikiwemo kunyimwa habari hata pale inapotakiwa kwa maslahi ya umma.

Simbaya amesema vyombo vya habari ni chachu katika kukuza maendeleo, demokrasia na kubainisha haki hivyo ni jambo la busara ikiwa watoa habari watakumbuka mambo hayo na kuamua kuwapa waandishi ushirikiano.

Ametaja alichokiita ushirikiano hafifu kutoka kwa watoa habari, lakini mara nyingine watu hawapendi kuandikwa kwa kuwatambua upande wa pili badala yake wanataka kila jambo linalowasifia ndiyo iwe habari, jambo alilosema linawafitinisha na viongozi wengine.

Mkurugenzi wa masuala ya lishe kutoka Ofisi ya Rais Tamisemi, Dk Rashid Mfaume amesema kwa sasa mpango huo unaelekeza nguvu katika ngazi ya chini ili kuwafikia watu wengi zaidi.

Dk Mfaume amesema lengo la kupelekea nguvu huko ni kutaka kujiimarisha ili hata wafadhili wa mradi wakiondoka, uwepo mwendelezo wa kuwasaidia watoto.

Kwa mujibu wa Dk Mfaume, halmashauri 70 za Tanzania zimeshafikiwa, lakini malengo ni kuona ifikapo Aprili mwaka wawe wamezifikia halmashauri zote.