Gwajima aagiza mpango wa Taifa uanzie vyuoni

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima akizindua kitabu kinachoelezea mapito ya taasisi ya maendeleo ya jamii Tengeru (TICD)', Novemba 20,2023 mkoani Arusha.

Muktasari:

  • Mpango huo unalenga kuwawezesha wananchi kushiriki moja kwa moja katika shughuli za maendeleo yao wenyewe kwa kutumia rasilimali walizonazo.

Arusha. Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima, amekielekeza Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru kuwajengea uelewa wanafunzi wao juu ya mpango wa Taifa wa kusimamia na kutekeleza maendeleo katika ngazi ya msingi.

 Mpango huo unalenga kuwawezesha wananchi kushiriki moja kwa moja katika shughuli za maendeleo yao wenyewe kwa kutumia rasilimali walizonazo.

Dk Gwajima ameelekeza hayo jana mkoani Arusha, katika kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya Taasisi ya Maendeleo ya Jamii iliyokwenda sambamba na mahafali ya 13 ya chuo hicho, ambapo jumla ya wanafunzi 1,652 walihitimu kozi tofauti.

Amesema kuwa mpango huo uliojengeka katika falsafa ya wananchi ndio kitovu cha maendeleo kuanzia ngazi ya jamii hivyo unahitaji wataalamu wenye uelewa mkubwa kusaidia utekelezaji wake.

"Nielekeze chuo hiki na vingine kuhakikisha wataalamu wanaoandaliwa wanafundishwa na kuufahamu mpango huu vizuri, ili wajue wakitoka hapa wawe wameiva na wanawafata wananchi ambao atashirikiana nao katika kuutekeleza," amesema Gwajima.

"Naelekeza haya mapema kwa sababu mpango huu ni kitovu cha maendeleo, hivyo sio tena wakija kazini tunaanza semina za kufundishana, hapana. Waje wameiva na wajue kule kazi ni moja tu kuutekeleza."

Waziri huyo pia, alikitaka TICD kufanya utafiti mkubwa ili kuwasaidia wananchi kubaini vikwazo na changamoto katika kujiletea maendeleo na Serikali itaunga mkono hatua zote.

Pia, alikitaka kuongeza mchago wake katika sekta ya maendeleo ya jamii kwa kuzingatia mabadiliko ya dunia kwa kuandaa wahitimu wenye stadi na maarifa ya kukabiliana na soko la ajira ikiwemo kuwawezesha kujiajiri na kutoa ajira kwa wengine.

"Mkitoka hapa mmeandaliwa vizuri na zana za uanagenzi na ubunifu wa kidigitali unakwenda mitaani kusoma fursa zilizopo, ikiwemo kufanya ziara kwenye taasisi mbalimbali za kibenki, kujua huduma zao zitakazokusaidia kuandika miradi ya kukupatia fedha na katika utekelezaji wake utajiajiri na utaajiri na wenzako na hivyo kujiepusha na matukio ya uhalifu na dawa za kulevya," amesema.

Mkuu wa TICD, Dk George Bakari amesema jumla ya wahitimu 1,652 wakiwemo wanawake 1,077 wametunukiwa shahada ya uzamili, shahada ya kwanza na astashahada.

Amesema katika mipango yao wanaotarajia kuanzisha mahusiano na taasisi zingine za elimu ya juu za ndani na nje ya nchi ili kutanua wigo wa utoaji wa mafunzo, ufanyaji utafiti na ushauri elekezi huku wakiwa wameweka mazingira ya kujifunzia kwa mfumo wa Tehama ili kuvutia wanafunzi wengi zaidi.

Mbali na hilo pia wanaelekeza nguvu katika utekelezaji wa ndoto ya kukifanyika chuo hicho kuwa kitovu cha taaluma ya maendeleo ya jamii Tanzania na kusini mwa Jangwa la Sahara.

"Ndoto hii inaweza kabisa kutekelezeka kwa kuzingatia mazingira ya sasa ya chuo chetu na katika hilo tutaendelea kuweka uwiano sahihi kati na nadharia na vitendo pia tutaweka mkazo katika dhana za uanagenzi, ufikishaji wa jamii na ubunifu vikisukumwa na mifumo ya Tehama ili kuleta matokeo ya haraka," amesema Dk Bakari.