Waziri Gwajima ataka utafiti kukabiliana na matukio ya ukatili

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima akizindua kitabu kinachoelezea mapito ya taasisi ya maendeleo ya jamii Tengeru (TICD)', Novemba 20,2023 mkoani Arusha.
Muktasari:
- Kutokana na kukua kwa maendeleo ya Tehama kunakochochea mmomonyoko wa maadili na ukatili katika jamii, Serikali imewataka wataalamu kufanya utafiti utakakaotatua changamoto hizo.
Arusha. Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima amewataka wataalamu wa wizara yake kuwekeza nguvu zaidi katika kufanya utafiti zenye kusaidia kutatua changamoto ya mmomonyoko wa maadili na ukatili.
Dk Gwajima ameyasema hayo mkoani Arusha leo Novemba 20, 2023 katika ufunguzi wa kongamano la siku tatu la wataalamu wa maendeleo ya jamii nchini, inayokwenda sambamba na kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru (TICD).
Amesema kuwa katika zama hizi za kidigitali kumekuwepo na matukio makubwa na ya kutisha ya ukatili wa kijinsia, vipigo kutokana na mmomonyoko wa maadili hali inayohatarisha usalama wa maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla miaka ijayo.
"Haya matukio yako chini yenu kama wataalamu, hebu nendeni tena mkafufue majukwaa ya maendeleo ya jamii kuanzia ngazi za chini kabisa mkishirikiana na asasi za kiraia kufanya tafiti upya wa nini kifanyike kurudisha maadili ya Taifa hili upya dhidi ya matukio haya ya ukatili, na mmomonyoko wa maadili," amesema Dk Gwajima.
Dk Gwajima pia amevitaka vyuo vya maendeleo ya jamii kuzalisha wataalamu wanaoweza kujiajiri na wanaokubalika kwenye soko la ajira hasa kwa kutoa mafunzo yanayoakisi mipango ya nchi na vipaumbele vya jamii, ili kuleta matokeo chanya nchini.
"Hatutaki maofisa maendeleo ya jamii wanaoingia mitaani kuungana na malalamiko ya uhaba wa ajira bali wanaokuja kujiajiri, kuzalisha ajira lakini pia watakaoweza kupambana kwenye soko la ajira kwa upeo wa maandiko mbali mbali ya miradi ya kusaidia utekelezaji wa majukumu ya maendeleo ya jamii," amesema.
Awali mkurugenzi wa TICD, Dk Bakari George amesema kuwa wanaadhimisha miaka 60 ya taasisi hiyo wakijivunia mafanikio makubwa ya kuzalisha watalaamu wa sekta hiyo wenye kuleta maendeleo makubwa nchini wakipewa sapoti ya kutosha.
Amesema chuo hicho kilichoasisiwa na hayati Mwalimu Julius Nyerere kimekuwa kikizalisha watalaamu wanaofanya kazi kwenye taasisi na mashirika ya umma na binafsi.
"Miaka hii 60 bado tuna malengo makubwa ya kuzalisha wataalamu wenye kuja na bunifu mbali mbali zenye matumizi ya Tehama katika kurudisha uzalendo, maadili na kupinga matukio ya ukatili nchini.
Akizungumza awali, Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda amesema kuwa sekta ya maendeleo ya jamii hasa wenye taaluma ina umuhimu mkubwa katika kurudisha Taifa katika misingi yake ya kimaadili, kiuchumi, kisiasa na hata maendeleo ya kilimo na afya.
"Naomba Serikali ione namna gani chombo hiki cha wataalamu wa maendeleo ya jamii kinapewa silaha ili kiweze kutimiza majukumu yake inavyotakiwa katika maendeleo ya nchi hii," amesema.