Gwajima ataka mtoto wa kike kuinuliwa

Muktasari:

  • Waziri Dorothy Gwajima amesema Jamii za Watanzania zinapaswa kuondokana na mila, desturi na tamaduni zinarudisha nyuma maendeleo ya mtoto wakike kufikia malengo ya kupigania haki na kuisaidia jamii yake kwa ujumla.

Dar es Salaam. Ili kumuendeleza mtoto wa kike na kufanikiwa kushika nafasi za uongozi, Watanzania hawana budi kuweka kando mila, desturi na tamaduni zinazorudisha nyuma kundi hilo.

Kauli hiyo ameitoa leo Oktoba 12, 2023 jijini Dar es Saalam na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dorothy Gwajima, katika hafla ya kuwatambua baadhi ya wasichana 300, wanaoandaliwa kuwa viongozi.

Wasichana hao wanaandaliwa shirika la kimataifa la Plan International, kupitia programu ya ‘Girls Take Over’ yenye lengo la kuwawezesha kushika nafasi mbalimbali za uongozi ndani na nje ya nchi.

"...tunaomba jamii ufungue milango zaidi iruhusu watoto wakike waende shule kwa kuwa Serikali imefuta karo na watumie fursa hiyo kujiendeleza tupate viongozi wengi," amesema.

Akiwazungumzia vijana hao 300, amesema Serikali inachukua takwimu za wasichana wote waliofanyiwa maendeleo kwa kutambua maeneo wanakopatikana ili zinapopatikana fursa iwe rahisi kuwafikia.

"Tunaomba zaidi  wadau tuzame hadi ndani vijijini maana wako wasichana wengi ambao wanashindwa kupelekwa shule lakini wanatunu za kiuongozi, na Serikali tunaunga mkono  kuhakikisha ndoto zao zinafikiwa katika kuona jinsia ya kike inashiriki kikamilifu kwenye ngazi mbalimbali za kimaamuzi," amesema

Amesema katika kuunga mkono wataweka mpango wa kuona nao wanaingia kwenye programu ya hiyo kwa kuongezea nguvu na kuipanua zaidi ili wafikiwe wengi zaidi.

Mwanafunzi kutoka Chuo cha Tumaini kampasi ya Dar es Salaam, Hilda Kibonde, ni miongoni mwa wanufaika wa programu hiyo, ambapo amesema lengo la mpango huo ni kuwaendeleza watoto wakike ili waweze kuonyesha chachu zao katika harakati za kukomboa jamii zao.

"Programu ilianza miaka sita iliyopita kwa kubaini vijana wenye ndoto mbalimbali na kuwaendeleza kielimu, tumekuwa tukiwapa motisha zaidi katika mapambano yao kuona wanashika nafasi mbalimbali ambazo zimezoeleka kushikwa na jinsia nyingine ili iwe rahisi kupitisha agenda zao," amesema.

Mkakati wa Serikali

Mkurugenzi wa Idara ya Watoto kutoka wizara hiyo, Sebastian Kitiku amesema Serikali imejikita katika maeneo matatu katika kuendeleza mtoto, kwanza kumuagalia maendeleo yake kuanzia mwaka sifuri hadi 08.

"Katika kipindi hiki ni muhimu kujenga vizuri ubongo wa mtoto kwani ndani ya kipindi hicho ubongo wake unakua kwa asilimia 90 na akikuzwa vizuri hapa uwezo wake wa kutafakari na kupambanua mambo unakuwa mkubwa hata katika kujenga hoja," amesema

Amesema kwa kuwa wizara imepewa dhamana ya kusimamia makuzi na malezi ya watoto imewekeza katika sehemu hiyo kwa kuandaa muongozo utakaotekelezwa hadi mwaka 2025 kwa watoto wote nchini.

Amesema pili wanamuangalia mtoto wa miaka 10 hadi 19 kwa kuwa ni kundi ambalo vijana wengi wanakuwa wamebalehe na wanapaswa kupewa aina yao ya makuzi na wanapaswa kupewa elimu ya utambuzi zaidi

"Ni kundi linalokabiliwa na janga la maambukizi ya virusi vya ukimwi, jamii imesahau ikidhani ukimwi umeisha lakini kundi hili lina maambukizi makubwa ya ugonjwa huu na linaongoza. Tumeandaa programu jumuishi ili kuangalia namna ya kuwasaidia watoto wenye umri huo wasipate tatizo hili," amesema

Ametaja eneo lingine ni afya kwa kuhakikisha watoto hao wanapata afya bora kwa kuwekeza eneo la lishe mathalani watoto wa kike kwa kuwa wanapoingia kwenye siku za hedhi, wanapoteza damu nyingi.

Amesema eneo lingine ni ulinzi kwa kuwa wanahitaji kuendelea kukua wanahitaji kulindwa wasikupambane na unyanyasaji au ukatili wowote.