Gwajima alaani pacha waliokufa wakikuzwa matiti

Muktasari:
- Katika kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike duniani Oktoba 11, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima amelaani vifo vya pacha waliokufa wakikuzwa matiti mkoani Simiyu, huku akiahidi kwenda kufanya uchunguzi zaidi wa sakata hilo.
Dar es Salaam. Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima amesema anakwenda kuchunguza zaidi sakata la mabinti waliokufa wakikuzwa matiti ili kuja na mkakati wa pamoja wa kisekta.
Pacha hao waliokuwa wakiishi katika kijiji cha Lubale Kata ya Nkololo Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, walifariki dunia Oktoba 4 baada ya kupakwa dawa za asili na anayesadikiwa kuwa mganga wa kienyeji Masunga Tumoro ili kuongeza matiti kwa ajili ya kuolewa.
Waziri Gwajima ameyasema hayo leo Jumamosi Oktoba 7, 2023 wakati akielezea kuhusu Mkutano wa Kimataifa wa Kutokomeza Ukeketaji unaotarajiwa kufanyika nchini kuanzia Oktoba 9 hadi 11 hapa nchini unaotegemewa kuwa na wageni zaidi ya 700.
"Mimi kwangu ninakwenda kuzama zaidi maofisa ustawi wa eneo hili waende kwenye hiyo jamii, huwa tunafanya utafiti wa kiustawi eneo lilikotokea tatizo ilikuwaje yule mtoa huduma alikuwepo hapo siku zote?
“Alikuwa amesajiliwa kwa maana kuna baraza la Tiba asili huwa linawasajili watoa huduma wa tiba asili kihalali kwa vigezo," amesema.
Amesema tayari amewasiliana na Mwenyekiti wa Baraza la Tiba asili na Tiba Mbadala, Profesa Hamisi Malebo ambaye tayari analishughulikia kwa nafasi yake.
"Tatizo kubwa lililopo katika eneo hilo na maeneo mengine, lazima tuangalie hao watu huwa wanaingiaje kwenye jamii zetu na jamii kwa nini inakubali? Ili tuje na mkakati wa pamoja wa kisekta ili tiba asili wawepo hapo, Wizara ya Afya, Jeshi la Polisi pia tuna kamati yetu ya ulinzi ya wanawake na watoto ipo pale inafanya nini haya yote lazima tujue," amesema.
Waziri Gwajima ameongeza; "Tunalaani, tunakemea, Tunasikitika, hatujafurahishwa na hatujapenda, jamii ituunge mkono wizara hii bila kushirikiana na jamii yenyewe haiwezi kufanya vizuri."
Amezishukuru Wizara za kisekta pamoja na Jeshi la Polisi kwa kuchukua hatua za haraka ikiwemo Wizara ya Afya ambayo tayari
Amesema tayari Mkuu wa Wilaya hiyo, Simon Simalenga ameshachukua hatua kama mwenyekiti wa kamati ya ulinzi wa wilaya yake ambapo ndani yake kuna wataalamu wa ustawi wa jamii.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Watoto Wizara hiyo, Katiku Sebastian amesema tayari mshukiwa huyo amekamatwa na Jeshi la Polisi na taratibu zingine zinaendelea.
Katika hatua nyingine, Waziri Gwajima amesema Tanzania ilipata fursa ya kushiriki mkutano wa kwanza wa kimataifa wa kutokomeza ukeketaji nchini Burkina Faso mwaka 2018 ambao ulishirikisha jumla ya nchi 22 wanachama wa Umoja wa Afrika.
"Umoja wa Afrika umechagua Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano wa pili wa Kimataifa utakaowakutanisha washiriki 900 ambapo Tanzania itakuwa na washiriki 200 na nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Afrika na mabara mengine watakuja washiriki 700," amesema.
Amesema lengo la mkutano huo wenye kaulimbiu ya mabadiliko katika kizazi kimoja kwenda kingine na ni sehemu ya utekelezaji wa Ajenda ya Maendeleo Endelevu ya mwaka 2030 na agenda ya 2063 ambazo zote mbili zimeweka ajenda ya kutokomeza ukeketaji na aina zote za mila na desturi zenye madhara kwa wanawake na wasichana kuwa kipaumbele muhimu na vinahitaji kufanyiwa kazi haraka.
Amesema takwimu za Afya, Idadi Watu na Viashiria vya Malaria za mwaka 2015/16 zinaonyesha kwamba ukeketaji umepungua kutoka asilimia 30 mwaka 2010 hadi asilimia 10 mwaka 2015 na kuna baadhi ya mikoa takwimu zake ni za juu zaidi ya wastani ambayo ni Manyara asilimia 58, Dodoma 47, Arusha 41, Mara 38, Singida 31 na Tanga 14.
Hata hivyo, amesema kwa kuwa Serikali imekuwa ikitekeleza Sheria kuzuia vitendo hivi, baadhi ya jamii imekuwa ikikeketa watoto wadogo kwa kukwepa kufahamika na kuchukuliwa hatua.
Waziri Gwajima amesema sambamba na mkutano huo, kutafanyika pia Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike Oktoba 11 katika ukumbi wa Mlimani City.