Pacha walivyofariki wakikuza matiti kwa mganga kijijini

Simiyu. Oktoba 4 mwaka huu ilikuwa siku ya majonzi kwa ndugu, jamaa na marafiki wa familia ya Yohana Saku, baada ya watoto wao pacha wenye umri wa miaka 17, Pendo Saku (Kulwa) na Furaha Saku (Dotto) kufariki, walipokuwa wakipakwa dawa na mganga wa kienyeji ili kukuza matiti yao.

Marehemu hao waliomaliza kidato cha nne mwaka 2022 walikuwa wakazi wa kijiji cha Lubale, wilayani Bariadi, Mkoa wa Simiyu.

Siku hiyo inadaiwa kuwa walipewa dawa hizo za kuongeza matiti ili waweze kuolewa, huku mganga anayetuhumiwa kuhusika, akitoroka na juhudi za kumsaka zinaendelea.

Watoto hao walizikwa jana na mamia ya wananchi na viongozi wa Serikali waliojitokeza kushiriki mazishi hayo.

Akizungumza katika ibada ya mazishi hayo, Kiongozi wa kanisa la Mtaa wa Majengo Nkololo Adventist Sabato (SDA), Chironge Hezron aliwataka wananchi kujenga imani ya hofu ili kuwakomboa watoto.

"Watoto hawa walikuwa tegemeo la kesho lakini wameruhusu shetani kuyashinda maisha yao ya kesho. Tunaamini kila jambo linapangwa na Mungu, lakini hapa jamii ibaki na tafakari. Mtoto akiwa wapi atakuwa salama? Tusikosoe uumbaji wa Mungu, ghadhabu yake ni kubwa," alisema.

Akizungumza kwa niaba ya Jeshi la Polisi wakati wa kutoa salamu za rambirambi katika msiba huo, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Agnes Chalimaga alisema jeshi hilo linaendelea na taratibu za kiserikali kuhusu tukio hilo.

"Tunaomba utulivu wakati taratibu za kiserikali zikiendelea, lakini jamii ijifunze kupitia hili, kuwa sio kila kitu ni cha kwenda kwa waganga wa kienyeji,’’ alisema.

Pendo (Kulwa) na Furaha (Dotto) walizaliwa Agosti 11, 2006 katika Kata ya Nkololo, wilayani Bariadi na walihitimu kidato cha nne katika shule ya sekondari Nkololo.


Tukio lilivyokuwa

Taarifa za awali zinaonyesha kuwa Septemba 28, 2023 watoto hao walipelekwa kwa mganga wa tiba asili kupata matibabu katika kijiji cha Byuna, wilayani hapo na ilipofika Oktoba 3, 2023 hali zao zilibadilika ndio walipopelekwa katika zahanati ya kijiji hicho.

Mganga mfawidhi wa kituo hicho, Dk Deogratius Mtaki, alisema kuwa Oktoba 4, 2023 alfajiri alipokea mwili wa Kulwa Yohana akiwa amekwishafariki, na Dotto Yohana alipokelewa saa 12 asubuhi akiwa mahututi na alifariki saa tatu asubuhi.

Akizungumza na Mwananchi jana kijijini hapo, baba wa pacha hao, Yohana Saku alisema alipata taarifa za ugonjwa wa watoto wake kupitia simu ya mkononi kutoka kwa dada yao, ambaye alimjuza kuwa Kulwa alikuwa anaumwa na yupo Kijiji cha Byuna hivyo akawaagiza apelekwe hospital kupata matibabu.

"Nilikuwa nipo kwenye familia yangu nyingine Ipililo, ilipofika saa tatu, niliambiwa kuwa Kulwa amefariki, nikaanza safari ya kuja, kabla sijafika nikaambiwa naye Dotto amefariki pia," alisema.

Alisema hakufahamu ugonjwa wa watoto hao hadi alipopigiwa simu alfajiri ya siku ya tukio,

Aidha, alisema hakuwahi kujadiliana na mke wake kuhusu kuozesha watoto na wala hakukuwa na msukumo wa uchumba ambao umesababisha hali hiyo.

"Walikuwa bado wadogo sana na walihitimu kidato cha nne mwaka jana na walikuwa wanajiandaa kwenda chuo cha ufundi. Nilikuwa tayari nimejiandaa ili kuwapeleka na ilikuwa waanze mwezi huu," alisema.

Alisema hafahamu kwa nini mke wake alifikia uamuzi wa kuwapeleka watoto kwa mganga.

Awali baba mdogo wa marehemu hao, Daniel Mishael alisema dawa waliyopewa ilikuwa ya kupaka na baada ya siku mbili hali ikabadilika.

"Kutokana na maelezo ya daktari alisema dawa zilizotumika zilikuwa nyingi sana na ambazo zilibadilika na kuwa sumu, hivyo kuingia kwenye maini na kusababisha kutapika damu na kuharisha," alisema Mishael.


Kauli ya Mkuu wa Wilaya

Juzi Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Simon Simalenga alifika katika eneo la tukio na kukemea kitendo hicho, huku akilitaka Jeshi la Polisi kumsaka mtuhumiwa ili achukuliwe hatua.

"Mganga apatikane awe amekimbia au amekwenda wapi na kama mmemkamata mke wake akae ndani hadi huyo mwanamume ambaye ni mganga apatikane," alisema Simalenga.

Alisema hiyo ni kesi ya mauji kama zilivyo kesi nyingine na wanatakiwa kupelekwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Bubale, Masebu Lubugwa aliwataka waganga wa kienyeji kuacha kutibu magonjwa ambayo hawana uwezo nayo na baadala yake watumie madaktari kwenye vituo vya afya na zahanati.