Waziri Gwajima apokelewa na mabango siku ya mwanamke

Waziri mwenye dhamana ya maendeleo ya jamii, Dorothy Gwajima akisoma mabango mbali mbali zenye jumbe za kupinga matukio ya ukatili, Leo octoba 15, katika Kata ya Kimnyaki wilayani Arumeru katika maadhimisho ya siku ya mwanamke anaeishi kijijini kitaifa mkoani Arusha.
Muktasari:
- Mabango hayo yaliwasilisha jumbe mbali mbali zinazoelezea matukio ya ukatili yaliyokithiri katika jamii zao wakiiomba Serikali kutengeneza upya sheria zenye adhabu kali za kutokomeza matukio hayo.
Arusha. Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dorothy Gwajima amejikuta akipokelewa na mabango yanayomtaka kuongeza nguvu katika kupambana na matukio ya ukatili hasa maboresho ya sheria na adhabu.
Mabango hayo yamewasilishwa leo Jumapili Oktoba 15, 2023 na watoto wa jamii ya kifugaji, katika maadhimisho ya siku ya mwanamke anayeishi kijijini yaliyofanyika katika kata ya Kimnyaki, wilayani Arumeru mkoa wa Arusha.
Wakizungumzia mabango hayo, Stella Saitabau amesema wameamua kutuma jumbe hizo kwa Serikali kuongeza nguvu katika kupambana na matukio ya ukatili hasa, ndoa za kulazimishwa na vipigo lakini pia matukio ya ubakaji na ulawiti ambavyo vinazidi kushamiri siku hadi siku na kujenga visasi na vinyongo kwa vizazi vijavyo.
"Kuendelea kushamiri kwa matukio haya yana madhara makubwa sana hivyo Serikali kupitia waziri wetu na wadau waongeze nguvu katika kupambana nayo ikiwemo kuboresha sheria na adhabu husika itakayotisha watekelezaji,"amesema.
Akizungumzia hayo, Waziri Gwajima amesema kuwa jukumu la kutokomeza matukio haya lianzie ngazi ya familia kutengeneza watoto wao katika hofu ya Mungu ili waogope kutekelezewa au kutekeleza matukio ya ukatili.
"Matukio 12,000 ya watoto waliofanyiwa ukatili kwa mwaka huu, zaidi ya 10,000 ni watoto wa kike na wengi wanafanyiwa na wanaume watu wazima hivyo wanaume nanyi mjitathimini nafasi yenu katika kutokomezatukio haya,"amesema.
Amesema kutokana na matukio hayo kushamiri na kuathiri jamii huku, wizara yake kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo itaangalia namna ya kuipa kipaumbele changamoto hiyo katika hatua ya utatuzi ikiwemo kuona namna nyingine ya kushughulika nazo.
Wakisoma risala ya maadhimisho hayo, afisa Mtendaji wa Kijiji cha Olevolos, Ngunyinyi Loitare amesema siku ya kimataifa ya mwanamke anayeishi kijijini huadhimishwa ikiwa ni utekelezaji wa Azimio la Umoja wa Mataifa iliyopitishwa 2007.
"Changamoto kubwa kwetu imebaki kuwa ukatili wa kijinsia ambayo yanashindwa kukoma kutokana na mengi kusuluhishwa nyumbani au kimila hivyo tunaomba Serikali ione namna gani inaweza kukabiliana nayo kuwekeza kizazi kijacho chenye nguvu na huruma kwa jamii"
Amesema ukatili mkubwa yanayofanyika kwenye jamii hiyo mbali na ndoa za kulazimishwa, vipigo na ubakaji na udhalilishaji ndani ya ndoa zao, pia yapo matukio ya ukeketaji, ubakaji na ulawiti kwa watoto wadogo ambayo yanaleta athari kubwa kimwili na kisaikolojia.