Ukatili dhidi ya wanawake kudumaza uchumi

Muktasari:

  • Takwimu za shirika la Umoja wa Mataifa linashoghulikia masuala ya wanawake (UN Women), zinaonesha vitendo vya ukatili wa dhidi ya wanawake hugharimu asilimia mbili ya uchumi wa duniani, huku baadhi ya nchi zikitumia hadi asilimia 3.5 ya pato ghafi la ndani kushughulikia masuala ya ukatili wa kijinsia.

Dar es Salaam. Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima amesema Tanzania haitaweza kusonga mbele ikiwa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake vitaendelea kufumbia macho.

Gwajima ameyasema ameyasema hayo Novemba 25, 2023 wakati akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, katika wa uzinduzi wa Kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Aidha, Waziri huyo aninukuu takwimu za shirika la Umoja wa Mataifa linashoghulikia masuala ya wanawake (UN Women), zinaonesha vitendo vya ukatili wa dhidi ya wanawake hugharimu asilimia mbili ya uchumi wa duniani.

“Sambamba na hilo, pia baadhi ya nchi hutumia hadi asilimia 3.5 ya pato ghafi la ndani kushughulikia masuala ya ukatili wa kijinsia...hatuwezi kusonga mbele kama nchi ikiwa ikiwa vitendo hivi vya ukatili vitaendelea kufumbia macho,” amesema.

Akizungumzia kauli mbiu ya kampeni hiyo, inayosema ‘Wekeza: Kuzuia Ukatili wa Kijinsia’ Gwajima mesema inampa jukumu kila mmoja katika nafasi yake kuwekeza zaidi kuzuia, kupinga na kutokomeza mauaji na ukatili dhidi ya wanawake na watoto kwa sababu ni kundi linalopitia changamoto nyingi zaidi za vitendo vya ukatili.

“Kwa upande wa Serikali imeendelea kuwekeza na kuchukua hatua mbalimbali za kuzuia na kutokomeza ukatili ikiwemo kuridhia mikataba na maazimio ya kikanda. Pia kuwezesha wanawake kiuchumi kupitia fursa mbalimbali,” amesema Waziri huyo.

Aidha Dk Gwajima amesema kuwa, takwimu zilizofanyika nchini za utafiti wa Afya ya Mzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria wa mwaka 2022, zimeonyesha matukio ya ukatili wa kimwili kwa wanawake wa umri kati ya 15 hadi 49; yamepungua kutoka asilimia 40 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 27 mwaka 2022.

“...hata ukatili wa kingono, pia umepungua kwa wanawake wa umri kati ya 15 hadi 49 kutoka asilimia 17 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 12 mwaka 2022. Hii inatokana na utoaji wa elimu kwa jamii na wadau mbalimbali yakiwemo mashirika yanayotetea haki za wanawake na watoto.” Amesema na kuongeza;

“Pamoja na juhudi hizo na kupunguza ukatili bado lengo la kupunguza kwa asilimia 50 halijafikiwa, hivyo bado tuna kazi kubwa ya kufanya hasa katika awamu ya pili ya Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (Mtakuwwa II).

Awali mratibu wa siku hizo za kupinga ukatili wa kijinsia kupitia mtandao wa Mkuki, Anna Kulaya ametaka kufanyika kwa mambo kadhaa kama sehemu ya kupambana na ukatili wa kijinsia ikiwemo marekebisho sheria ya ndoa  ya mwaka 1972 na uwepo kwa sheria ya ukatili wa kijinsia.

Akilizungumzia hilo, Dk Gwajima amesema la Sheria ya ndoa bado linashughulikiwa na Wizara ya Katiba na Sheria baada ya kukusanya maoni kutoka kwa wadau mbalimbali.

Wakati kuhusu la kuwepo kwa sheria ya ukatili wa kijinsia, Waziri huyo amemuelekeza Katibu Mkuu wizara hiyo, Dk Seif Shekalaghe kulifikisha suala hilo wizarani kwa kuwa ni la kisekta.

Aidha, mtandao huo wa Mkuki umesema kuwa umejipanga kuwekeza katika maeneo tofauti kupambana na ukatili japo umesisitiza pamoja na mambo mengine, kipaumbele kiwekwe katika uundwaji wa sheria ndogondogo za Serikali za Mtaa kudhibiti vitendo hivyo kuanzia ngazi ya chini.

Baadhi ya washiriki waliohudhuria uzinduzi huo akiwemo Edwin Rumboyo, amesema katika vita hiyo ya kupambana na ukatili kumekuwa na tabia ya familia kulindani, na kukemea matendo hayo kwa kutaka sheria ifuate mkondo wake.

Kwa upande wa Najma Mandela, amesema jamii haipaswi kufumbia macho vitendo vya ukatili kwani kuna wanaoona wakitendewa ni jambo la kawaida jambo ambalo sio sahihi.