Dk Hoseah ageukia dhamana kesi uhujumu uchumi

Muktasari:

  • Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Dk Edward Hoseah amesema atashirikiana na baraza la uongozi wa chama hicho kushawishi mabadiliko ya sheria zinazowanyima dhamana watuhumiwa na makosa ya utakatishaji fedha na uhujumu uchumi.

Arusha. Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Dk Edward Hoseah amesema atashirikiana na baraza la uongozi wa chama hicho kushawishi mabadiliko ya sheria zinazowanyima dhamana watuhumiwa na makosa ya utakatishaji fedha na uhujumu uchumi.

Dk Hoseah, ambaye alichaguliwa juzi kuwa rais wa chama hicho kwa kupata kura 297, alieleza hayo baada ya kuapishwa na Mwanasheria Mwandamizi, Colman Ngallo jijini Arusha.

Alisema kwa mujibu wa sheria, mtuhumiwa anapaswa kuhesabiwa hana hatia hadi Mahakama itakapomwona ana hatia kutokana na ushahidi mahakamani.

Kauli ya Dk Hoseah inatokana na vilio vya baadhi ya wabunge na watu wa kada mbalimbali kuhusu kesi za utakatishaji fedha na uhujumu uchumi kwamba zinaipatia Serikali mabilioni ya fedha na watuhumiwa hawatendewi haki.

Kwa nyakati tofauti Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe aliwahi kunukuliwa akihoji sababu za Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kukubaliana na baadhi ya washtakiwa kuhusu malipo ya mabilioni ya fedha huku mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akisema kesi hizo zimegeuzwa mkakati mpya wa kukusanya mapato.

Katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mwaka 2019/20, imeelezwa kulikutwa Sh51.52 bilioni kwenye akaunti ya DPP zilizopatikana kutokana na kesi zilizomalizika katika Mahakama mbalimbali miaka sita iliyopita.

Katika uchambuzi wake kuhusu ripoti hiyo, Zitto alisema fedha hizo hazikutumika kwa sababu ya kukosekana kwa sheria na kanuni zinazoelekeza matumizi yake, bali zilipatikana baada ya DPP kutaifisha fedha za watu kabla ya kuwepo kwa sheria ya ‘plea bargain.’

Katika maelezo yake ya jana, Dk Hoseah ambaye amewahi kuwa mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) alisema atatumia uzoefu wake kushawishi mabadiliko ya sheria zote kandamizi zinazotweza utu wa watuhumiwa kwa sababu kila mtu anayo haki ya kupata dhamana, isipokuwa pale tu ambapo mahakama itajiridhisha vinginevyo.

“Watuhumiwa wa makosa ya utakatishaji fedha na uhujumu uchumi sheria inawanyima kupewa dhamana, unapomweka mtuhumiwa mahabusu kwa muda mrefu unakuwa umemnyima haki ya msingi, zipo nchi ninazozifahamu Kenya, Nigeria na Afrika Kusini makosa hayo yana dhamana.”

Hata hivyo, alisema sheria imempa madaraka makubwa DPP hata wakati mwingine kuiamuru Mahakama wakati inapaswa kuwa huru kutoa maamuzi yanayozingatia sheria za nchi kulingana na kesi husika.

Alisema sheria zinazotungwa, msingi wake ujikite kwenye utu kwa sababu ndio msingi wa demokrasia, utawala bora na maendeleo ya nchi yoyote ambayo imeamua kuwajali wananchi wake kupitia mfumo wa kisheria.

“Mtakumbuka tume ya Jaji Nyalali iliainisha uwepo wa sheria kandamizi kwenye mfumo wetu wa sheria; ni wakati mwafaka kuangalia ripoti hiyo kwa mapana yake, naamini Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ni sikivu na TLS itashirikiana na Serikali kuwahudumia wananchi,” alisema Dk Hoseah.

Kuhusu wanachama wa TLS, alisema watarajie utumishi uliotukuka kwa kuwatumikia kwa usawa na kuangalia masilahi yao ambayo ni huduma muhimu za matibabu ya kibingwa, bima za afya, kuondoa ada ya kujiunga kwa wanachama wapya na kuongeza usimamizi wa fedha na uwazi wa matumizi yake.

Katika uchaguzi ulifanyika Ijumaa, chama hicho kilimchagua Dk Hosea kuwa rais, huku nafasi ya makamu mwenyekiti akichaguliwa Gloria Kabalamu, mweka hazina ni Fredrick Msumali na mwenyekiti wa kamati ya nidhamu ni Ibrahim Bendera. Viongozi wa kanda waliochaguliwa ni Stephen Mwakibolwa (Bagamoyo), James Malenga (Mzizima), Mwansoho Gabriel (kanda ya kati), Elibariki Maeda (kanda ya kaskazini), Ladislaus Rwekaza (kanda ya kusini), Lenin Njau (kanda ya ziwa) na Kamaliza Kayaga (kanda ya mashariki).