Ujenzi wa nyumba Hanang wafikia asilimia 40

Muktasari:

  • Jumla ya nyumba 108 za waathirika wa maafa ya Hanang zinajengwa, kati ya hizo 73 zinajengwa na Serikali kupitia Suma-JKT na nyingine 35 zinajengwa na Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.

Arusha. Wakati ujenzi wa nyumba za waathirika wa mafuriko ya Hanang ukipiga hatua kufikia asilimia 40, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dk Jim Yonazi amesisitiza uwekwaji wa anwani za makazi katika eneo linalojengwa nyumba 108 za waathirika hao.

Ujenzi wa nyumba hizo unakuja baada ya wakazi wa eneo hilo kupoteza makazi yao kutokana na maporomoko ya mawe, tope na miti kutoka Mlima Hanang yaliyotokea mwishoni mwa mwaka 2023.

Dk Yonazi ametoa rai hiyo leo Mei 5, 2024 alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa nyumba hizo zinazoendelea kujengwa katika eneo la Gidagamowd, lililopo wilayani Hanang mkoani Manyara.

Amesema ni muhimu eneo hilo likawekwa anuani za makazi kama yalivyo mengine nchini na kuonyesha namba za nyumba na vibao vyenye majina ya mitaa ili kurahisisha utambuzi, ufikishaji wa huduma na bidhaa.

Amesema Serikali imetenga eneo la ekari 100 ambapo jumla ya viwanja 269 vimepimwa na kati ya hivyo 226 ni makazi pekee,  26 ni makazi na biashara na 17 ni maeneo ya huduma za kijamii.

Amewataka wakandarasi kukamilisha utekelezaji wa mradi huo kwa wakati na kuzingatia ubora unaotakiwa.

“Mradi ukamilike kwa wakati kama ilivyokubalika, yaani ndani ya siku 90 na uendane na thamani ya fedha itakayotumika. Pamoja na hilo, endeleeni kushirikiana na wenyeji wa eneo hili ili kuimarisha uhusiano,” amesema Dk Yonazi.

Akizungumza kuhusu maendeleo ya mradi huo, Kaimu Operesheni Kamanda, Luteni Kanali Ashraf Hassan amesema ujenzi wa nyumba 73 umefikia asilimia 40 na unajengwa kwa kuzingatia vigezo vya ubora uliokusudiwa na Serikali.

“Tumefurahi kutembelewa na Katibu Mkuu, Dk Yonazi na sisi tunamuahidi kuwa ujenzi huu utakamilika kwa wakati lakini pia kwa kuzingatia viwango vya ubora vilivyoelekezwa,” amesema Luteni Kanali Ashraf.

Akieleza faida za mradi wa ujenzi huo, amesema umesaidia kutoa ajira kwa wenyeji, biashara ndogondogo hasa za mamalishe, kukuza uchumi wa wakazi wa Katesh pamoja na kuimarisha uhusiano na wakazi wa maeneo hayo pamoja na uboreshwaji wa miundombinu ya barabara, maji na umeme.

Disemba 3, 2023, Wilaya ya Hanang ilikumbwa na maafa yaliyosababishwa na maporomoko hayo na watu 89 walipoteza maisha huku mamia wengine wakiachwa bila makazi.

Serikali iliratibu masuala yote ya menejimenti ya maafa ikiwa ni pamoja na hatua ya kurejesha hali, ambapo kwa sasa zinajengwa nyumba 108 za waathirika wa maafa hayo, nyumba 73 zinajengwa na Suma JKT na nyingine 35 zinajengwa na Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania (Red Cross) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.