Dk Kihamia: Niliteuliwa nikiwa ndani ya basi, nimetenguliwa nikiwa kitandani - VIDEO

Dar es Salaam. Katika maisha tunayopita kila binadamu huwa na mambo fulani hawezi kuyasahau. Yanaweza kuwa ya kufurahisha, huzuni au ya kushangaza.

Dk Athuman Kihamia anaweza kuwa na stori ya kusisimua kuisikiliza ambayo unaweza kudhani ni ya kubunia au kutunga, lakini ni ukweli.

Mazingira yake ya kuteuliwa kuwa mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na jinsi alivyoondolewa yanataka kufanana, lakini yapo katika mazingira tofauti kidogo.

Dk Kihamia aliyehudumu nafasi hiyo kwa siku 457 sasa anasubiri kupangiwa kazi nyingine na Rais John Magufuli ambaye usiku wa kuamkia Jumanne ya Oktoba Mosi alimteua Dk Wilson Charles kuchukua nafasi yake.

Taarifa ya mabadiliko hayo ilitumwa na mkurugenzi wa mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa saa 8 usiku wa kuamkia Jumanne.

Akizungumza na Mwananchi jana, Dk Kihamia ambaye ni mtaalamu wa uhasibu na usimamizi wa miradi ya maendeleo anasema wakati anateuliwa Julai Mosi mwaka jana alikuwa safarini ndani ya basi akitoka Dar es Salaam kwenda Dodoma, lakini Jumanne alipotenguliwa alikuwa kitandani.

“Taarifa za kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi nilizipata saa 1:00 asubuhi kupitia TBC TV (TBC1), niliona tu wakati wakitoa muhtasari wakasema Mheshimiwa Rais ateua mkurugenzi wa uchaguzi NEC.”

“Nikakaa kitandani, kwa sababu saa 1:15 asubuhi ndio huwa natoka nyumbani, nikakaa kuangalia (televisheni)...nazipata (taarifa) mara ya kwanza. Nikashindwa kwenda kazini nikatulia nyumbani siku nzima,” alisema Dk Kihamia baba wa watoto watatu na mke mmoja.

Mkurugenzi huyo wa zamani wa Jiji la Arusha na Kaliua Tabora alisema “baada ya hii taarifa ya kuondolewa, changamoto niliyoipata ni simu na meseji zimekuwa nyingi, hadi sasa kuna meseji zaidi ya 300 kiasi kwamba hata utulivu unaondoka.”

Dk Kihamia ambaye hakuwa tayari kuzungumzia masuala ya kiutendaji ya NEC kwa kuwa si msemaji tena wa taasisi hiyo alisema “nikiwa NEC nimesimamia chaguzi (ndogo za ubunge) karibu tisa na kweli nilijitahidi kusimamia misingi ya Katiba na sheria kiasi kwamba malalamiko yalipungua sana kwa sababu tulijielekeza kwenye maeneo ya elimu.”

Akizungumzia mazingira ya utendaji kazi NEC alisema “nilijifunza nikiwa NEC unakuwa na masaa mengi sana ya kufanya kazi, mchana mzima na usiku ufanye kama sehemu ya mchana, huwezi kufanya kazi chini ya saa tano.

“Muda mwingi lazima ufanye kazi, kile chombo kiko katika kila kata hivyo, lazima ufanye kazi usiku na mchana.”

Dk Kihamia ambaye ni mtoto wa pili kati ya watoto wanane wa Mzee Athuman Juma mkazi wa Korogwe, Tanga alisema siku alipoteuliwa kuwa mkurugenzi wa Jiji la Arusha alikuwa Kaliua anaangalia televisheni.

“Siku nateuliwa kuwa Mkurugenzi Tume ya Uchaguzi nilikuwa katika basi kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma,” alisema Dk Kihamia

Alisema alitoka Arusha kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu ya meno na akiwa Dar es Salaam akapata taarifa za kikao kazi kinachofanyika mkoani Dodoma.

Dk Kihamia alisema “nikaamua kwenda Ubungo kupanda basi, nilipofika nikakosa basi la Shabiby, nikaamua kupanda mtwangio (basi) la kawaida kisha nikamwambia dereva wangu aliyekuwa Arusha aje tukutane Dodoma.”

Alisema akiwa katika basi maeneo ya Kibaigwa, Morogoro “nikapata simu kutoka kwa mkurugenzi wa Tanga ambaye ni rafiki yangu, ananipa hongera, nikamwambia hongera ya nini, akasema soma meseji, pale hapakuwa na mtandao, nikaja kuona baadaye.”

“Niliposhuka Dodoma nikachukua kibegi changu na kupanda daladala, nilipofika mjini nikakutana na mkurugenzi mwenzangu na kunipeleka katika mgahawa na wakati huo nikaona ni taarifa za kweli baada ya kuona kuwa natakiwa kuapishwa kesho yake. Hivyo nikaanza safari kurudi Dar es Salaam,” alisema Dk Kihamia ambaye ni mwanachama wa Yanga na Liverpool ya England.