Dk Malasusa ataja sababu ongezeko la talaka nchini

Muktasari:
- Baadhi ya watu wanadhani ndoa za utotoni kama jambo la kawaida hali iliyofanya KKKT kuangalia namna ya kukabiliana na tatizo hilo.
Mwanza. Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Alex Malasusa amesema nchi imekuwa ikishuhudia ongezeko la talaka, huku akitaja chanzo ni mmoja wa wanandoa kutokuwa huru na uamuzi wa kuingia katika ndoa.
Ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Januari 20, 2025 wakati akifungua mafunzo kwa waandishi wa habari ya kuripoti habari zinazohusu athari za ndoa za utotoni mkoani Mwanza.
Amesema hali hiyo inatokana na kukosa uamuzi wa kile kilichofanywa na wazazi wao ambao tamaduni imewapa nguvu ya kuwaamulia baadhi ya vitu.
Kwa mujibu wa Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa 2014, kilichotolewa na Wizara ya Fedha talaka zilizosajiliwa zimeongezeka kwa asilimia 93.7 kutoka zilizokuwapo mwaka 2022.
Kitabu hicho kinaonesha kuwa mwaka 2023 ndoa zilizosajiliwa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) zilikuwa 45,455, zikiwa zimeshuka kutoka 51,011 mwaka 2022, huku talaka zikifika 866 kutoka 447.
Dk Malasusa amesema bahati mbaya jamii kupitia tamaduni na mila imekuwa ikiona kuwa watoto ni mali yao hali inayofanya mila ya Kiafrika na makabila mengi watoto kuitwa kwa kutumia jina la baba na kujiona wao ni wamiliki.
“Taratibu inanifanya (kama baba) umiliki uwe zaidi kwangu ikiwamo kuamua chochote kwa mtoto ikiwamo kuuzwa, watoto si wa kuuza watu wanachukua mahari wanakwenda kuuza watoto,” amesema.
Amesema jambo hilo limekuwa likifanya tatizo la talaka kuwa kubwa ndani ya jamii kwa sababu mmoja wa wanandoa hakuwa na uamuzi au utayari wa kuingia katika ndoa.
“Watoto wengi wanasukumwa kuingia katika ndoa na hawana uhuru wa kuamua lini wanataka kuingia katika ndoa,” amesema Dk Malasusa.
Takwimu za Rita za mwaka 2020, zinaonyesha kuwa wakala huo, ulisajili talaka 511 Tanzania nzima kati ya hizo 221 kutoka Dar es Salaam pekee.
Akizungumzia ndoa za utotoni, Dk Malasusa amesema ni suala linalowaumiza viongozi wengi wa dini kwa kuwa linapoteza uelekeo wa wasichana.
“Suala la ndoa za utotoni lifike mwisho tupeleke elimu hii kwa wazazi na watoto wafundishwe haki zao, wakiambiwa juu ya haki zao watajitetea ili waweze kusimama na kujua kuwa wana maisha zaidi kuliko kukimbilia kwenye ndoa,” amesema.
Mkurugenzi wa Upendo Media ambao pia ni waratibu wa semina hiyo, Nang’da Johannes amesema wasichana wanaoolewa wakiwa wadogo hupoteza fursa ya elimu na kuingia katika ndoa zisizo na upendo wala heshima katika jamii.
Amesema ndoa za utotoni ni tatizo linaloikabili Tanzania na nchi zinazoendelea huku mikoa inayoathiriwa zaidi ikiwa ni Shinyanga, Tabora Mara, Dodoma na Lindi.
Johannes amesema baadhi ya watu wanadhani ndoa za utotoni kama jambo la kawaida, hali iliyofanya KKKT kuangalia namna ya kukabiliana na tatizo hilo.
“Hivyo, sisi kama walinzi wa watoto hawa tunawahakikishia kuwa, tutaendelea kutengeneza mazingira mazuri ya kusemea jamii ambazo zimeathiriwa, tumeona kuwa ni tatizo na tukaamua kutengeneza mradi unaolenga kuondoa jambo hili,” amesema Johannes.
Msimamizi Mkuu wa Programu ya Mradi ya Maisha Endelevu na Uwekezaji KKKT, Patricia Mwaikenda amesema mradi huo umepewa jina la ‘Hapana marefu yasiyokuwa na mwisho,’ ikiwa na maana kuwa, imekuwa safari ndefu katika nchi za Afrika tangu enzi za mabibi na mababu walioolewa katika umri mdogo.
“Ndiyo maana kanisa likasema hapana lazima ifike mwisho, kuandaa mtalaa utakaotumika kufundisha viongozi wa dini na tamaduni, kutoa elimu kwa watoto kupinga na kujitetea na kuwafanya viongozi wa dini wakatae jambo hili kwa kuwa wanaaminiwa,” amesema Mwaikenda.
Tayari mafunzo hayo yamefanyika kwa wakufunzi kutoka mikoa minne ya Tanzania bara na Zanzibar huku wilaya zaidi ya 30 zikifikiwa.