Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Uchunguzi wabaini sababu tano kinara madai ya talaka

Muktasari:

  • Ripoti ya tathmini ya miaka mitatu ya Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia yataja sababu tano zinazoongoza kesi za madai ya talaka, wadau washauri namna ya kukabiliana nazo.

Dar es Salaam. Kasi ya ndoa kuvunjika ikiongezeka, imebainika kutengana kwa wanandoa na uzinzi ndizo sababu zinazoongoza nyingi kufikia hatua ya kutolewa talaka.

Hayo ni kwa mujibu wa matokeo ya uchunguzi yaliyochapishwa kwenye ripoti ya tathmini iliyofanywa katika kipindi cha miaka mitatu cha utendaji kazi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia kilicho chini ya Mahakama ya Tanzania. Kituo hicho kilianzishwa Agosti 27, 2021.

Uchunguzi huo uliofanyika katika kipindi cha miaka mitatu uliohusisha mashauri 1,348 ya ndoa, ambayo ni sawa na asilimia 19 ya mashauri yote yaliyorekodiwa tangu kituo hicho kianze kufanya kazi.

Uchunguzi huo uliolenga kubaini maelezo sahihi na kutathmini hali halisi ya migogoro ya ndoa ili kufikia suluhu bora kwa pande zote, ulibaini wanandoa wengi wanaofikia kutalikiana huanza kwa kutengana.

Tathmini hiyo inaonyesha katika kipindi cha miaka mitatu, jumla ya mashauri 4,843 ya ndoa yalifunguliwa. Mwaka 2023 umeweka rekodi ya kuwa na mashauri mengi zaidi ya ndoa yaliyofunguliwa ambayo ni 2,425.

Mwaka 2021 mashauri 672 ya ndoa yalirekodiwa katika Ofisi ya Usuluhishi wa Migogoro ya Ndoa (OSJC) wakati mwaka 2022 yakirekodiwa mashauri 1,746, ikiwa ni ongezeko la asilimia 62 kutoka mwaka uliotangulia.

Ripoti hiyo inazitaja sababu sababu tano kuu zinazochangia kuongezeka kwa mashauri yanayolenga kuvunja ndoa kuwa ni kutengana inayoongoza kwa asilimia 25 ya kesi zote, ikifuatiwa na uzinzi inayochangia asilimia 16.

Talaka ya Kiislamu inafuata kwa asilimia 15, ukatili asilimia 14 na migogoro ya kifamilia na kutokuelewana kwa wanandoa inachangia asilimia 12.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo wanandoa wengi wanakabiliwa na changamoto za kutokuelewana, hivyo hutafuta suluhu ya kutengana.

“Hizi ni sababu kuu zinazochangia kuongezeka kwa idadi ya mashauri ya ndoa na zinaonyesha hitaji la zaidi ya huduma za usuluhishi na msaada wa kisheria ili kutatua migogoro ya ndoa,” imeeleza ripoti hiyo iliyotolewa Desemba 10, 2024.

Ripoti pia inaonyesha katika kipindi cha miaka mitatu, migogoro ya ndoa 7,054 ilirekodiwa na OSJC.

Migogoro 86 ilirekodiwa Mahakama Kuu, 1,132 mahakama za wilaya na migogoro 5,836 ilirekodiwa kutoka mahakama za mwanzo.


Wasemavyo wadau

Mwanasaikolojia Christian Bwaya, amesema wanandoa wengi hufikia hatua ya kutengana kutokana na kukosa elimu sahihi kuhusu ndoa hivyo wengi huingia wakiwa na matarajio tofauti na msingi mkuu ambao ni upendo.

Amesema matarajio yao yanaposhindwa kutimia, kutengana inakuwa njia rahisi.

“Kinachotokea ni kwamba, vijana wengi siku hizi hawaingii kwenye ndoa kwa sababu ya upendo, wanakuwa na matarajio yao kichwani na linaloonekana zaidi ni ngono, muonekano wa nje na kipato. Inapotokea ameshaingia kwenye ndoa halafu anakutana na vitu tofauti na matarajio yake ndipo visa vinaanza, usaliti unatokea na migogoro ikishika kasi ndiyo wanatengana.

“Kutengana inatumika kama njia ya kukwepa kuwepo kwenye ndoa, migogoro ya aina hii isipotafutiwa ufumbuzi zinakuja talaka,” amesema.

Bwaya ametaja sababu nyingine inayochangia ndoa kusambaratika ni matokeo ya kuingia kwenye uhusiano bila kushirikisha familia.

“Ilivyokuwa zamani, kijana hadi kufikia hatua ya kufunga ndoa ni lazima familia ina ufahamu wa kina kuhusu mwenza wake na familia yake. Hii iliweza kupunguza migogoro kwa namna moja au nyingine.

“Siku hizi vijana wanakutana wanaanzisha uhusiano ghafla wanafunga ndoa, hawajipi muda wa kufahamiana, hawatoi nafasi kwa familia zao kujuana vizuri na kusikiliza mawazo yao,” amesema.

Kukabiliana na hali hiyo, ameshauri viongozi wa dini kusimama imara kutoa mafunzo kwa vijana wanaotaka kuingia kwenye ndoa kuifahamu vyema taasisi hiyo na umuhimu wake.

Amesema ni muhimu kwa taasisi za dini kutenga muda usiopungua miezi sita kwa ajili ya mafunzo kuhusu dhana ya ndoa, uvumilivu na upendo kabla ya kufungisha ndoa.

Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Khamis Mataka amesema ni muhimu kwa wanajamii kurudi katika misingi ya dini na kuzingatia inachoelekeza kuhusu ndoa.

“Ukisimamia misingi ya dini huwezi kupata shida, turudi katika dini tuangalie inatuelekeza kufanya nini. Tukiyajua na kuzingatia maelekezo basi kila kitu kitakwenda sawia.

“Mwanamume atajua wajibu wake na mwanamke atafahamu vitu gani azingatie kama mke ndani na nje ya nyumba. Dini inazuia masuala ya kutoka nje ya ndoa sasa kama unazingatia mafundisho hayo suala la michepuko halitakuwa na nafasi kwako, amani, upendo na utulivu vitatawala kwenye ndoa yenu,” amesema.

Sheikh Mataka amesema: “Wanandoa ni zao la jamii, kuna mmomonyoko wa maadili. Jamii yetu haiishi kidini, uongo umekuwa sehemu ya maisha, kukosa uaminifu inaonekana ndiyo ujanja. Hapa ndoa haiwezi kudumu.”

Mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Richard Hananja amesema vijana wanaoingia kwenye ndoa hawapati mafunzo ya kiroho kutoka kwa viongozi wa dini kuwawezesha kufahamu uhalisia wa ndoa.

Amesema kutokana na hilo, wengi wanaingia bila kufahamu wanaenda kufanya nini na wanapaswa kusimamia vipi viapo wanavyotoa wakati wanaoana.

“Siku hizi watu wanaingia kwenye ndoa hawajapata mafundisho ya kutosha, ikitokea wamepata basi ni kwa siku moja au wiki. Siku moja haiwezi kumfanya mtu ajifunze na kuelewa undani wa ndoa, faida na hasara zake, hapa viongozi wa dini tunapaswa kujitathimini.

“Tukiwafundisha hawa vijana tutawasaidia waishi kwa upendo, kumtanguliza Mungu katika kila jambo na ndoa zao zitadumu tofauti na ilivyo sasa wanaingia wakiwa hawafahamu wanaenda kufanya nini,” amesema.