Dk Mpango awapa wiki mbili Dodoma kusafisha mitaa

Saturday January 15 2022
MPANGO PIC

Makamu wa Rais nchini Tanzania, Dk Philip Mpango

By Sharon Sauwa

Dodoma. Makamu wa Rais nchini Tanzania, Dk Philip Mpango ameagiza Jiji la Dodoma kuhakikisha ndani ya wiki mbili linaondoa uchafu wote kwenye mitaa ya Jiji hilo.

 Agizo hilo limetolews baada ya kushuhudia lundo la taka katika maeneo tofauti ya soko kuu la Majengo wakati wa ziara yake ya kukagua usafi katika Jiji la Dodoma leo Jumamosi Januari 15, 2022 alipofanya ziara katikati ya jiji kukagua usafi.

“Mheshimiwa Rais (Samia Suluhu Hassan) alitaka kuja hapa lakini mimi nikamwambia ngoja niende mimi kwanza. Inasikitisha sana jiji ambalo ni makao makuu ya nchi linakuwa hivi,”amesema Dk Mpango.


Pia amewataka viongozi kuacha kukaa ofisini na badala yake kupita mitaani kukagua usafi wa mazingira katika maeneo mbalimbali.

Amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka kukagua hali ya usafi kwenye maeneo mbalimbali ya jiji baada ya wiki mbili kabla ya yeye kurudi kukagua.

Advertisement

Kwa upande wake Mtaka amemhakikishia Makamu wa Rais kuwa watahakikisha kuwa kazi hiyo inafanyika na kwamba changamoto hiyo haitajirudia tena.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru amesema wataifanya kazi hiyo ndani ya muda mfupi.

Hata hivyo, amesema magari ya kuzolea takataka ni machache jijini Dodoma.

Advertisement