Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dk Mpango awatahadharisha vijana wasitumike kisiasa kuchochea vurugu nchini

Baadhi ya wanachama wa Chama cha Mapinduzi,wakiingia kwa maandamano katika kiwanja cha Kawawa, Manispaa ya Kigoma Ujiji kwa ajili ya Tamasha la kuelekea miaka mitatu ya mafanikio ya Rais Samia Suluhu Hassan na maadhimisho ya miaka 47 ya kuzaliwa kwa CCM.

Muktasari:

  • Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango ameshiriki kwenye tamasha maalumu ya kuadhimisha miaka mitatu ya Serikali ya awamu ya sita na kuwatka vijana kutokubali kutumika kisiasa.

Kigoma. Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango amewataka vijana nchini kutokubali kutumika kisiasa katika kuchochea vurugu, uhasama na maandamano yasiyo na tija nchini.

Akizungumza leo Jumapili Januari 28, 2024 mjini Kigoma kwenye tamasha la kuelekea miaka mitatu ya mafanikio ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na maadhimisho ya miaka 47 ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) lililoandaliwa na Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), amesema vijana wasiwe sehemu ya kundi la kuharibu na kuchochea machafuko.

Amesema uchumi wa dunia nzima umeathiriwa na ugonjwa wa Uviko-19, vita kati ya Ukraine na Russia, athari za mabadiliko ya tabianchi na kwa sasa vita inayoendelea mashariki ya kati ambapo athari hizo haziwezi kutatuliwa kwa siku moja tena kwa maandamano.

“Uchumi wa dunia nzima umeathiriwa, hivyo ndugu zangu tuambizane ukweli, athari hizi hatuwezi kutatua kwa siku moja tena kwa maandamano kama ambavyo baadhi ya wanasiasa wa upinzani nchini wanavyojaribu kuwaaminisha wananchi,” amesema Dk Mpango.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye amesema mkoa huo umepokea Sh11.40 trilioni katika kipindi cha miaka mitatu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo barabara, reli, meli, ukarabati wa kiwanja cha ndege, hospitali ya kanda pamoja na nyumba wakuu wa wilaya na wakurugenzi.

Wakizungumza kwenye tamasha hilo, baadhi ya vijana wamesema hawezi kuunga mkono maandamano katika kupata suluhu na badala yake kukaa mezani na kujadili changamoto ndiyo njia sahihi.

“Kufanya maandamano si kupata suluhu katika matatizo yanayokabili nchi yetu, lakini kukaa na kushauriana, naamini ndio njia nzuri na yenye amani, kwani kila kijana ana jukumu la kuilinda na kutunza amani yetu,” amesema Salum Haji.

Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Mohammed Kawaida amesema wanatarajia kumsindikiza Rais Samia Suluhu Hassan kuchukua fomu ya kugombea urais na kwa niaba ya umoja huo amemkabidhi Makamu wa Rais, Sh1 milioni ya kuchukua fomu katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2025 pamoja na kumkabidhi tuzo ya heshima.