Dk Mwaikali ampinga Askofu Shoo uchaguzi Dayosisi ya konde

Kiongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Fredrick Shoo

Muktasari:

  • Siku moja baada ya kiongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Fredrick Shoo kumtangaza Geofrey Mwakihaba kuwa Askofu Mkuu wa Kanisa hilo Dayosisi ya Konde, Askofu Dk Edward Mwaikali amesema hatambui mabadiliko hayo kwa sababu hajajulishwa chochote.

Mbeya. Siku moja baada ya kiongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Fredrick Shoo kumtangaza Geofrey Mwakihaba kuwa Askofu Mkuu wa Kanisa hilo Dayosisi ya Konde, Askofu Dk Edward Mwaikali amesema hatambui mabadiliko hayo kwa sababu hajajulishwa chochote.

Kwa muda mrefu kumekuwapo na mgogoro katika Dayosisi hiyo hali ambayo imekuwa ikihatarisha amani kwa waumini wa dhehebu hilo hasa baada ya kuhamishwa kwa makao makuu kutoka Tukuyu kwenda Mbeya mjini.

Katika mkutano uliofanyika jana Jumanne Machi 22, 2022 jijini Mbeya ulifanyika uchaguzi kufuatia tume iliyoundwa na Dk Shoo ya kupiga kura ya kutokuwa na imani na Dk Mwaikali ambaye ni Askofu Mkuu wa kanisa hilo.

Jumla ya kura 204 zilimkataa Dk Mwaikali na tano zilimkubali, zoezi hilo liliambatana na uchaguzi, ambapo Dk Shoo alimtangaza Mwakihaba kuwa Askofu Mkuu akisaidiwa na Dk Meshack Njiga.

Dk Mwaikali ameliambia Mwananchi kuwa mkutano huo hautambui kwani hakupata mwaliko wake, lakini pia hajapata barua yoyote yenye kueleza mabadiliko.

“Siwezi kuongea chochote kwa sasa kwa sababu huo mkutano sikupewa mwaliko na sijui kilichofanyika, kama itakuja barua yenye maelezo hayo ndio nitaongea rasmi na kuweka msimamo,” amesema Dk.Mwaikali.