Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dk Mwigulu ataka sekta binafsi iheshimiwe

Waziri Mkuu wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba akizindua ghala la forodha, Chamwino mkoani Dodoma.


Muktasari:

  • Sekta ya umma ina watumishi wasiozidi 600,000 kwa miaka yote tangu uhuru maana yake sio rahisi kuingiza wote wanaoingia kwenye soko la ajira zaidi ya milioni mbili kila mwaka. Njia sahihi ya kuifuata ni sekta binafsi.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba ameeleza umuhimu wa kuheshimu sekta binafsi kutokana na mchango wake kiuchumi ambapo si tu Tanzania bali duniani kwa ujumla.

Dk Mwigulu ameyasema hayo leo Jumatano, Juni 10, 2026 wakati anazindua ghala la forodha, Chamwino mkoani Dodoma,  ambapo amesema kitendo cha kufika kuzindua kwa uzito ghala hilo ni sehemu ya kuheshimu sekta binafsi.

Dk Mwigulu amesema hata uchumi wa mataifa yaliyoendelea nguzo yake ya muhimu ni sekta binafsi.

Akielezea umuhimu wa maghala, amesema yanatoa huduma ya kuhifadhi bidhaa zinazoingia na kutoka nchini, hivyo yana mchango mkubwa katika maendeleo ya biashara,  yanarahisisha minyororo mzima wa ugavi na usafirishaji wa kikanda, maendeleo ya biashara pamoja na kuongeza ufanisi.

“Kama tunavyoheshimu sekta ya umma inatakiwa pia tuheshimu sekta binafsi, mchango wa Serikali na mashirika yake ya umma unatarajiwa kuwa asilimia 30 na  70 inatarajiwa itoke sekta binafsi,” amebainisha.

Amesema mradi huo ambao ni sekta binafsi ni kielelezo katika utekelezaji wa dira hiyo ya maendeleo na Serikali itaendelea kuhakikisha unakua na manufaa makubwa.

Akifafanua zaidi, Dk Mwigulu amesema maghala hayo yanapunguza msongamano bandarini kuongeza ufanisi wa bandari zetu na kudhibiti upotevu wa mapato ya Serikali.

“Sekta ya umma ina watumishi wasiozidi 600,000 kwa miaka yote tangu uhuru maana yake sio rahisi kuingiza wale wote wanaoingia kwenye soko la ajira zaidi ya milioni mbili kila mwaka. Njia sahihi ya kuifuata ni sekta binafsi ambayo hata mataifa makubwa yanavyofanya, hivyo lazima tujenge sekta itakayowezesha kuleta nafasi kubwa na vyanzo vya ajira kwa vijana,” amesema.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema kupitia ghala hilo la forodha, Dodoma itakuwa ndiyo makao makuu ya ubadilishanaji, usafirishaji na uhifadhi wa bidhaa.

“Dodoma ni eneo la kimkakati kwa kuwa inafikika kirahisi kutoka pande zote za Tanzania kupitia njia za barabara, reli na viwanja vya ndege vilivyopo,” amesema.

Amesema Watanzania watakuwa wanakwenda Dodoma kununua bidhaa ikiwa ni fahari ya mkoa huo, huku kuanzishwa kwa bandari kavu pia ni miongoni mwa mradi wa kimkakati, ambapo tayari Serikali imeshatenga eneo Ihumwa kwa ajili ya kuendeleza bandari hiyo.