Dk Mwinyi avutiwa na ushirikiano kuinua utalii

Monday May 02 2022
dk mwinyi pic

Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Omari Said Shaban (kulia) na Afisa Mkuu wa wateja wakubwa na Serikali, Alfred Shayo wakiwaongoza wateja wa benki ya NMB kuchukua futari iliyoandaliwa kwa ajili ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan. Wa kati ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti wa Baraza la Wawakilishi wa Zanzibar, Ali Suleiman Urembo. (Na Mpiga Picha wetu)

By Mwandishi Wetu

Zanzibar. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imeeleza kuvutiwa na ushirikiano wa kibiashara kati ya Kamisheni ya Utalii Zanzibar (ZTC) na benki ya NMB.

Imesema kuwa ushirikiano huo umekuwa chachu ya kukuza utalii huku ikiitaka kuziunga mkono wizara zote za SMZ na Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuziwezesha kuziona fursa na kuzitumia kwa ustawi wa Uchumi wa Zanzibar.
Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Omar Said Shaaban ameyasema hayo Jumapili ya Mei Mosi, 2022 wakati akiwasilisha salamu za Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, kwenye hafla ya futari iliyoandaliwa na NMB na kuhudhuriwa na mawaziri wa SMZ, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, viongozi wa Dini na wateja wa benki visiwani hapa.
Akizungumza kwa niaba ya Dk Mwinyi, Waziri Omar, alisema ushirikiano huo ulioifungamanisha ZTC na fursa za kiuchumi na kwamba, anatamani kuona unazifikia wizara mbalimbali na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
“Niko hapa kwa niaba ya Rais, Dk. Hussein Mwinyi na nichukue nafasi hii kuwapa salamu zake. Kwanza amefarijika kwa aina ya ushirikiano uliokuwepo baina ya NMB na ZTC ambao unalenga zaidi kukuza utalii wetu. Ushirikiano huo unaangalia mbali zaidi ya yale tuliyoyazoea.
“Kwa muda mrefu utalii wetu ulikuwa umejikita katika kuuza fukwe, lakini NMB mmenyoosha mkono kwa ZTC na kuwaonesha fursa zingine za kiutalii tulizonazo, hasa vivutio vya historia na mambo kale.
“Pia, SMZ inawakaribisha zaidi NMB kushirikiana na wizara yenyewe ya utalii kwa ujumla wake, najua ina mipango mingi mbali ya ile ya Kamisheni, lakini pia mshirikiane na wizara zingine zote za SMZ, kuanzia Wizara ya Elimu, Wizara ya Fedha, Wizara ya Kilimo, hata Wizara ya Biashara na Mamlaka zetu za Serikali za Mitaa.
“Mkikaa na Mstahiki Meya atawaambia fursa zilizopo katika kuendeleza miji na majiji yetu. Kwa hiyo niwaalike mshirikiane na wizara zingine na naamini mtashiriki kwa mapana katika kuendelea kuuimarisha uchumi wa Zanzibar, kupitia dhana hii inayochakatwa na Rais Dk. Mwinyi ya Uchumi wa Bluu,” amesisitiza Waziri Omar.
Naye Afisa Mkuu wa Wateja Wakubwa na Serikali wa Benki ya NMB, Alfred Shao, amesema benki hiyo imekuwa na mahusiano ya muda mrefu na ZTC na kwamba, hautaishia kwenye kuimarisha sekta ya utalii kwenye fukwe za bahari, bali pia unaangazia utamaduni wa Mzanzibar na vyakula asilia.
“Hafla hii inafanyika katika muktadha huo wa mashirikiano baina yetu. Tunafanya mambo mengi katika sekta ya utalii, lengo ni kuunga mkono jitihada za Serikali ya Zanzibar, kwani tunatambua Sekta ya Utalii ni kati ya maeneo yanayoiingizia pesa nyingi sana Serikali, nasi tumeelekeza nguvu zetu huko,” amesema Shao.


Advertisement