Dk Slaa kushiriki maandamano Chadema Mwanza

Dk Wilbrod Slaa

Muktasari:

  • Maandamano hayo yatahitimishwa katika uwanja wa Furahisha wilayani Ilemela mkoani Mwanza yakilenga kushinikiza matakwa mawili ambayo ni ugumu wa maisha na Serikali kusikiliza maoni ya wananchi kuhusu miswada mitatu ya sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani pamoja na ya vyama vya siasa.

Mwanza. Maandalizi ya maandamano ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), mkoani Mwanza yamefikia asilimia 90 huku miongoni mwa waliothibitisha kushiriki ni mwanasiasa mkongwe, Dk Wilbrod Slaa.

Taarifa hiyo imetolewa jana Jumanne Februari 13, 2024 na Katibu wa Chadema Kanda ya Victoria, Zacharia Obad, wakati viongozi wa kamati ya maandalizi ya maandamano hayo walipotembelea na kukagua uwanja wa Furahisha wilayani Ilemela jijini hapa, yanapotarajiwa kuhitimishwa.

Dk Slaa alipozungumza na Mwananchi Digital lililotaka kujua kama kweli atashiriki maandamano hayo amesema, “ni kweli nitashiriki na nitakuwepo.”

Obad amewataja wengine waliothibitisha kushiriki mbali na Dk Slaa aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chadema,  ni wakili Boniface Mwabukusi, Mdude Nyagali (mwanaharakati) na viongozi wakuu wa chama hicho wakiongozwa na Mwenyekiti Freeman Mbowe.

Amewaomba waajiri kutoa ruhusa kwa watumishi wanaohitaji kushiriki maandamano hayo yanayofanyika kesho Alhamisi ya Februari 15, 2024.

“Tutatumia maandamano hayo kuomboleza kifo cha (Edward) Lowassa kwa sababu aliwahi kuwa mwanachama na kiongozi ndani ya chama chetu, pia alikuwa kiongozi wa umma alipokuwa Waziri Mkuu nchini,” amesema Obad.

Amewataka wafuasi wa Chadema na wasiokuwa wafuasi kujitokeza kwa wingi kushinikiza matakwa hayo mawili ambayo ni ugumu wa maisha na Serikali kusikiliza maoni ya wananchi kuhusu miswada mitatu ya Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani pamoja na ya vyama vya siasa iliyokwisha pitishwa na Bunge.

Kuhusu uhalali wa maandamano hayo, Obad amesema Chadema imewasilisha barua ya kufanya katika Ofisi ya Mkuu wa Polisi (OCD) Ilemela, OCD Nyamagana na nakala ya barua hiyo katika Ofisi ya Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza.

Mwananchi Digital imeshuhudia nakala ya barua yenye kumbukumbu namba EA.740/794/01/6 na kusainiwa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Ilemela mkoani humo, Apolinary Ndibaika (SP).

Hata hivyo, alipopigiwa simu kufahamu iwapo Jeshi hilo limejibu taarifa ya maandamano iliyotolewa na Chadema, Kamanda wa Polisi mkoani wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amesema yuko kwenye kikao, alipotumiwa ujumbe wa ‘WhatsApp’ umeonakana kumfikia (bluetick) bila kujibiwa.

Maandamano kama hayo ya amani yalifanyika jijini Dar es Salaam, Januari 24, 2024 yaliyoanza sehemu mbili, Mbezi Mwisho na Buguruni na kukutania Shekilango kisha kwenda Ofisi za Umoja wa Mataifa (UN) kuwasilisha ujumbe wao juu ya masuala hayo mawili.

Wakati wakiandamana jijini Dar es Salaam, Bunge lilikuwa halijaijadili miswada hiyo iliyokuwa imewasilishwa bungeni Novemba 10, 2023. Mara hii wanaandamana miswada hiyo ikiwa imeshapitishwa na Bunge na kilichobaki na kusainiwa na Rais ili iwe sheria kamili.

Katika maelezo yake, Obad amedokeza kuwa tayari viongozi na wajumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), Benson Kigaila wamewasili jijini Mwanza kukamilisha maandalizi ya maandamano hayo.

Kwa upande wake, Katibu Mwenezi wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha) Taifa, Twaha Mwaipaya amewataka vijana kujitokeza kwa wingi kushiriki maandamano hayo kwa kile alichodai ajenda zake zinalenga kuleta ukombozi kwa vijana.

“Maandamano hayo yamebeba ajenda kubwa ya ugumu wa maisha, asilimia 60 ya Watanzania ni vijana ndiyo wanakumbana na kadhia ya ukosefu wa ajira na ugumu wa maisha. Tuko hapa kwa sababu ya kuratibu maandamano ya kupinga ugumu wa maisha na k/atiba mpya,” amesema Mwaipaya.

Imani ya Mkazi wa Nyasaka jijini Mwanza, Mary Songe ni kwamba maandamano hayo ya amani ni moja ya njia ya kuwasilisha changamoto zinazoikumba jamii, kutoa ushauri na Serikali kutumia hoja zitakazowasilishwa kuboresha utendaji kazi wake.

“Ninachokiamini ni kwamba jamii itapokea maandamano hayo kwa mwitikio mkubwa na watu wengi hasa wanawake watajitokeza kutimiza takwa hilo la kisheria. Hakuna mabadiliko yaliyowahi kutokea bila kuchukua hatua, maandamano ni moja ya hatua ya kuyaleta,” amesema Mary.

Njia za maandamano

Februari 8, 2024, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), Benson Kigaila akitoa taarifa ya maandamano hayo alisema waandamanaji wanatarajiwa kutumia njia tatu tofauti katika Wilaya za Ilemela na Nyamagana kabla ya kukutana eneo la Ghandi Hall na kuhitimisha kwa mkutano wa hadhara katika uwanja wa Furahisha.

Alitaja njia hizo ni Ilemela-Kanisani katika barabara ya Makomgoro, Pasiansi, Nyamanoro, Kona ya Bwiru, Darajani mpaka kwenye bustani ya Ghandi Hall huku, njia ya pili ikianzia Buhongwa kupitia Kenyatta, Mkolani, Nyegezi, Butimba, Mkuyuni, Igogo, Nyamagana, Isamilo hadi Ghandi Hall.

“Njia ya tatu itaanzia Igoma center na itapita Barabara ya Nyerere, Mandu, Mabatini, Natta, Nyerere Plaza mpaka Ghandi Hall, maandamano ya sasa yataishia kwa wananchi… tunaenda kukutana na wananchi wa Mwanza ili tuzungumze nao kwa maana haya malalamiko ya katiba na hali ngumu yanawahusu,” amesema Kigaila

Ujumbe wa Mbowe

Kupitia kurasa zake za kijamii, Mbowe ametoa ujumbe wa kuwakaribisha wananchi kwenye maandamano hayo ambayo amesema atayaongoza.

Sehemu ya ujumbe huo unasomeka,

Kwa mapenzi ya Mungu, nitaongoza maandamano ya Taifa ya Amani jijini Mwanza, Alhamisi 15 Februari 2024 Taifa likiwa katika maombolezo ya hayati Edward Ngoyai Lowassa.

Lowassa aliamini sana katika kazi na alisisitiza salam za hongera kwa kazi badala ya pole kwa kazi.

Tunamuenzi kwa kuendeleza maombolezo pamoja na kazi... aliyoijaribu kwa kuungana nasi 2015, akawa mgombea wetu wa urais.

Taifa bado linalilia Katiba mpya na mifumo huru na ya haki ya uchaguzi.

Taifa lina vilio vingi. Watawala wanapaswa kulitambua hili. Ni wajibu wetu kwa pamoja tupaze sauti zetu usiku na mchana hadi wenye mamlaka watambue hali halisi ya hisia za umma wa Watanzania.

Maumivu yetu makubwa ni umasikini unaotesa maelfu kwa maelfu ya Watanzania kunakosababishwa na kupanda kwa viwango visivyohimilika vya gharama za maisha, ikiwemo chakula, pembejeo, nauli, mgao mkubwa usioelezeka wa umeme n.k.

Watanzania wote tukutane Mwanza tukaandike historia.