Dk Tulia avutiwa kupanda kwa gawio CRDB

Muktasari:

  • Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Tulia Ackson amesema ukuaji mkubwa wa faida uliopata benkii ya CRDB unastahili kupigiwa mfano na taasisi zingine za fedha nchini.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Tulia Ackson amesema ukuaji mkubwa wa faida uliopata benki ya CRDB unastahili kupigiwa mfano na taasisi zingine za fedha nchini.


Pia, amesema ukuaji huo umetokana na uwekezaji na usimamizi mzuri katika uendeshaji wa benki hiyo hivyo, kuwawezesha wanahisa kupata gawio ambalo sasa litaongezeka hadi kufikia asilimia 64 kwa hisa.


Dk Tulia ametoa pongezi hizo leo Ijumaa Mei 20, 2022 wakati akifungua semina ya elimu ya fedha iliyoandaliwa na benki hiyo kwa wanahisa wake na Watanzania kwa ujumla wakati wakijiandaa na Mkutano Mkuu wa 27 wa Wanahisa unaofanyika Mei 22, 2022 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).


“Nadhani sitakuwa nimekosea nikisema ongezeko la faida baada ya kodi ambayo CRDB imepata mwaka jana kufikia Sh268.2 bilioni kulinganisha na Sh165 bilioni kwa mwaka 2020, ni ukuaji mkubwa wa faida kupata kutokea,” amesema Dk Tulia.


Amesema benki hiyo imeendelea kudhihirisha kwa vitendo kuwa: “Benki kiongozi” nchini kwani kila mwaka imekuwa ikitengeneza faida ya uwekezaji kwa wanahisa wake na kuzitaka taasisi nyingine za umma na binafsi kuiga mfano.


“Nimefurahishwa pia kusikia mwaka huu Bodi ya Wakurugenzi imekuja na pendekezo la ongezeko la asilimia 64 ya gawio kwa hisa. Wanahisa wa CRDB mnastahili kutembea kifua mbele kwa ongezeko hili,” ameongezea Dk Tulia.


Dk Tulia pia ameipongeza benki hiyo kwa kuandaa semina ya elimu ya fedha na uwekezaji kwa ajili ya wanahisa huku akibainisha kuwa umahiri wa masuala ya fedha wa wananchi ni moja ya msingi muhimu wa maendeleo.


“Niwapongeze kwa kuongoza katika utoaji wa elimu ya masuala ya fedha kwa Watanzania. Siku chache zilizopita, mliandaa semina mliyoiita CRDB Bank Uwekezaji Day, niliichungulia mtandaoni nikiwa Dodoma,” Dk Tulia ameongeza huku akiitaka benki hiyo kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili kuongeza ujumuishi wa kifedha.


Aidha, Dk Tulia ameiitaka benki hiyo kuendelea kuwekeza katika kuendelea kuwezesha sekta mbambali za maendeleo nchini hususan sekta ya kilimo, huku akiitaka pia kusaidia malengo ya Serikali katika uanzishwaji wa Benki ya Ushirika ya Taifa kama ambavyo imefanya kwa Benki ya Ushirika ya Tandahimba (TACOBA) na Benki ya Ushirika ya Kilimanjaro (KCBL).


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi benki hiyo, Dk Ally Laay amesema wanajivunia kuendelea kukuza thamani ya uwekezaji wa wanahisa wake ikiwamo Serikali ambayo inamiliki asilimia 36 ya hisa.


“Niwakaribishe Watanzania wengine waje kuwekeza kwetu ili waanze kunufaika na gawio nono ambalo limekuwa likitolewa na benki yao,” ameongeza Dk Laay.


Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Abdulmajid Nsekela amesema malengo ya semina hiyo ni kuwajengea uwezo wanahisa pamoja na Watanzania wengine ili kuwa na uwajibikaji wa kifedha na kuongeza ushiriki katika fursa za uwekezaji hususan katika soko la hisa la Da es Salaam.


“Kwa kutoa elimu hii wanahisa wetu pia wanapata kufahamu zaidi faida za kuwekeza katika benki hii, hivyo basi kuongeza uwekezaji na kupata faida nono zaidi, lakini pia kuwahamasisha wengine pia kuwekeza katika hisa hususan za CRDB na kuanza kupata gawio,” ameongezea Nsekela.


Nsekela alitumia fursa hiyo pia kuwakaribisha Wanahisa katika Mkutano Mkuu utakaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (AICC) na kupitia mtandaoni.