DK Tulia: Tumuunge mkono Rais nishati safi ya kupikia
Muktasari:
- "Tumefanya mashindano haya kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ametambuliwa kimataifa kama kinara wa nishati safi ya kupikia. Pia, tunapofanya mambo kama haya, tunaelimishana kuhusu umuhimu wa kutumia nishati safi na kuachana na nishati isiyosalama, hivyo tutakuwa tunalinda mazingira.
Mbeya. Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, amesisitiza umuhimu wa kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ametambuliwa Afrika kama kinara wa nishati safi ya kupikia.
Dk Tulia alitoa wito kwa wananchi kutumia nishati safi ambayo ni salama kwa afya na mazingira leo Septemba Mosi, 2024 jijini Mbeya alipokuwa akitoa shukrani kwa wadau mbalimbali waliofanikisha mashindano ya kupika kwa gesi ya Oryx.
Mashindano hayo yamewashirikisha baba na mama Lishe 1,000 kutoka kata zote za Jimbo la Mbeya Mjini.
"Tumefanya mashindano haya kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ametambuliwa kimataifa kama kinara wa nishati safi ya kupikia. Pia, tunapofanya mambo kama haya, tunaelimishana kuhusu umuhimu wa kutumia nishati safi na kuachana na nishati isiyosalama, hivyo tutakuwa tunalinda mazingira," amesema Dk Tulia ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya mjini.
Amesema majiko na mitungi ya gesi waliyopatiwa na Oryx itawawezesha mama na baba lishe hao kukua kibiashara.
Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga aliyekuwa mgeni rasmi, amesema Serikali inafanya jitihada mbalimbali kuhakikisha wananchi wanatumia nishati safi ya kupikia. Amesisitiza kuwa Serikali tayari imeona umuhimu wa kupunguza bei ya gesi ili kuwawezesha wananchi kumudu gharama, huku akipendekeza mfumo wa kununua gesi kidogo kidogo kwa siku.
Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Gas Tanzania, Benoit Araman amesema lengo la mashindano hayo ni kuhamasisha matumizi ya nishati safi ili kulinda mazingira.
"Kwa miaka zaidi ya 15, upatikanaji wa nishati ya kupikia umekuwa ukijadiliwa, lakini sasa Serikali chini ya Rais Samia inahamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia," amesema Benoit. Amesema kupika kwa gesi kutasaidia kupunguza muda wa wanawake kutafuta kuni na mkaa na hivyo kuwakinga dhidi ya wanyama wakali na vitendo vya ukatili porini.
Chief Rocket Mwashinga, akizungumza kwa niaba ya Machifu wa Mkoa wa Mbeya, ameiomba Serikali na wadau wa gesi kuangalia uwezekano wa kupunguza bei ya gesi ili wananchi waweze kumudu gharama na kulinda mazingira.
Kwa upande wao, baadhi ya mama na baba lishe walioshiriki mashindano hayo wameshukuru kupata mafunzo na msaada wa majiko, wakisema yamewasaidia kuelewa umuhimu wa kutumia nishati safi na kulinda mazingira