DMDP awamu ya pili kujenga kilometa 250 Dar

Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba (kulia) na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia (WB) nchini Tanzania, Nathan Belete, wakisaini hati ya mkataba wa mkopo kwa ajili ya kutekeleza awamu ya pili ya Mradi wa Kuendeleza Miundombinu Dar es Salaam (DMDP II). jijini Dar es Salaam leo Februari 20, 2024. Picha na Michael Matemanga
Muktasari:
- Awamu ya pili ya DMDP itaboresha barabara za kiwango cha lami kilomita 250 jijini Dar es Salaam, ukiwamo ujenzi wa madampo ya kisasa yatakayohifadhi taka kwa ufanisi, ujenzi wa masoko, mifereji na vituo vya mabasi tisa.
Dar es Salaam. Utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu Dar es Salaam (DMDP), awamu ya pili umeanza kunukia baada ya Serikali kusaini mkataba na Benki ya Dunia (WB) wa mkopo wa ufadhili wa mchakato huo utakaogharimu takribani Sh1 trilioni.
Awamu ya pili ya DMDP itaboresha barabara za kiwango cha lami kilomita 250, ujenzi wa madampo ya kisasa yatakayohifadhi taka kwa ufanisi, ujenzi wa masoko ya kisasa, mifereji na vituo vya mabasi tisa. Miradi hiyo itatekelezwa katika halmashauri zote za mkoa wa Dar es Salaam.
Katika awamu hiyo, Ilala imepewa kilomita 53.5 za barabara, Temeke (42), Kigamboni (57), Ubungo (52) na Kinondoni (48), zitakazotekelezwa kwa awamu tofauti hadi kukamilika kwake.
Miongoni mwa maeneo yatakayonufaika na mradi huo ni Manzese, Tabata, Sinza, Majumbasita hadi Stakishari, Tabata Mawenzi, Migombani, Tabata Baracuda hadi Chang’ombe, Mbezi Msumi, Kigamboni na Pemba mnazi.
Leo Februari 20, 2024, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba na Mwakilishi Mkazi wa WB nchini, Nathan Belete wamesaini mkopo huo katika ofisi ndogo za Hazina, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa baada ya kusaini mkopo huo, Dk Mwigulu amesema tukio hilo ni muhimu katika safari ya uendelezaji wa miundombinu ya mkoa wa Dar es Salaam na itabadilisha taswira ya maeneo mbalimbali.
"Wabunge wa Dar es Salaam walinikabaa koo sana kuhusu mradi huu, sasa hatua ya leo tumefikia pazuri, mradi ni mwendelezo wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya 2023/26 pamoja na Ilani ya CCM ya mwaka 2020/25.
"Awamu ya pili itajumuisha uboreshaji wa mtandao wa barabara, ili kupunguza msongamano, ujenzi wa mitaro ya maji, miundombinu ya masoko pamoja na kupunguza athari za mabadiliko tabia nchi," amesema Dk Mwigulu.
Naye Belete amesema, "leo tuna furaha kwa sababu DMDP ni miongoni mwa mradi uliotupa presha ndani ya WB nchini, huu ni mradi muhimu sio tu kwa Tanzania pekee, bali hata kwa Benki ya Dunia kwa sababu unajibu mahitaji ya muda mfupi na mrefu ya Dar es Salaam.
"Dar es Salaam ni eneo kubwa lenye wakazi milioni 5.4, ambapo bandari yake inaiwezesha Tanzania na nchi sita jirani zisizo na bandari kupata soko la kimataifa, tunajivunia kuunga mkono jitahada za ukuaji wa mkoa huu," amesema Belete.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa amesema awamu ya pili ya DMDP itazifikia halmashauri zote tano za Dar es Salaam na utaboresha barabara, vituo vya mabasi masoko na miundombinu ya madampo.
"Dar es Salaam imekuwa ikisumbuliwa na taka ngumu, lakini mradi utahusika namna ya kukusanya, kuzisafirisha na kuzihifadhi kupitia madampo, hatua hii itaondoa hali ya uchafu ndani ya mkoa wa huu.
"Tutakwenda kujenga masoko ya kisasa 18, mifereji itakayodhibiti mafuriko sambamba na vituo tisa vya mabasi na utekelezaji wake utaanza hivi karibuni," amesema Mchengerwa.
Mchengerwa ameishukuru WB kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali, huku akiwataka watendaji wake kuanza mara moja kazi ya utekelezaji wa mradi huo kwa sababu kila kitu kimekwenda vizuri.
Mbunge wa Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile amesema hatua ya Serikali kusaini mkopo huo ni furaha kwa wakazi wa Dar es Salaam waliosubiri kwa muda mrefu utekelezaji wa mradi huo.
"Tuna furaha kubwa haikuwa kazi rahisi tulipambana sana kwa sababu kipaumbele cha Dar es Salaam ni barabara, sasa kinachotakiwa ni kuanza haraka utekelezaji wake zabuni zitangazwe, ili Aprili kazi zianze kama tulivyoahidiwa," amesema Dk Ndugulile.
Mbunge wa Viti Maalumu Dar es Salaam, Mariamu Kisangi ameishukuru Serikali na WB kufikia hatua hiyo, akisema walikuwa wanaisubiri kwa hamu na mradi huo utakaokwenda kuboresha barabara za Dar es Salaam.