EAC wakutana kujadili changamoto huduma za posta
Muktasari:
Wadau wa Mashirika ya Posta kutoka nchi za EAC wakutana na kujadili namna ya kurahisisha utoaji huduma hizo.
Arusha. Wadau wa mashirika ya posta kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wamekutana jijini Arusha kujadili changamoto pamoja na kuangalia namna ya kurahisisha utoaji huduma za posta katika Jumuiya hiyo.
Akizungumza leo Novemba 2, 2022 jijini Arusha wakati wa ufunguzi wa Jukwaa la Posta Biashara Mtandao na Usafirishaji, Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew amesema kuwa, jukwaa hilo lina lengo la kuwakutanisha pamoja wadau hao katika kubadilishana uzoefu na kuweza kuangalia namna bora zaidi ya kuboresha huduma za posta zinazotolewa katika nchi hizo.
Mhandisi Kundo amesema kuwa,jukwaa hilo ni la kwanza kufanyika na wanatarajia kuona huduma zinawafikia wananchi kwa haraka zaidi na zenye gharama nafuu na kuzalisha fursa ambazo zitawasaidia wateja wa huduma zao.
"Kwanza kabisa nianze kwa kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira mazuri na rafiki ya kidemokrasia ambapo imetuwezesha sisi kupata fursa ya kuandaa mkutano huu wa kwanza wa watoa huduma za posta katika nchi za jumuiya. Hiyo ni katika namna ambavyo Rais amekuwa kinara wa kuhakikisha mifumo na miundombinu ya mawasiliano nchini inazidi kurahisishwa,"amesema Mhandisi Kundo.
Ameongeza kuwa, kupitia mkutano huo kuna mabadilishano mengi kwani huduma nyingi sasa hivi zinaenda kidigitali zaidi na tayari posta wameshaanza kutoa huduma zake kwa njia ya kidigitali zaidi, hivyo wanajivunia sana kuandaa mkutano huo wa kwanza.
Naye Katibu Mtendaji wa Taasisi ya mawasiliano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dk Ally Simba amesema kuwa, lengo ni kuinua na kuipa mwelekeo sekta ya Posta kwani kuna fursa nyingi sana kwenye mambo ya mabadiliko ya kidigitali, pamoja na biashara mtandao.
Simba amesema kuwa, kupitia mkutano huo wataweza kuzungumzia jinsi sekta ya posta itasaidia wananchi wake katika uchumi wa kidigitali na matumizi ya fedha pamoja na masuala ya biashara mtandao.
Amesema kuwa, hivi sasa katika taasisi ya mawasiliano ya EAC kuna mchakato unafanywa ili iwe taasisi ya Tehama ya Afrika Mashariki ili kuhakikisha yale matunda katika sekta hiyo yaweze kuwafikia wananchi wa jumuiya ya EAC.
Naye Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Macris Mbodo amesema kuwa, ni heshima kwao sekta ya posta Tanzania kushirikiana na taasisi ya posta ya EAC kuweza kuandaa mkutano wa kwanza wa posta za Afrika Mashariki ambao haukuwahi kufanyika.
Amesema kuwa,wameona umuhimu wa kukaa pamoja kama wakuu wa posta za EAC kutafakari namna ambavyo taasisi hizo zitaweza kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia na kushiriki mchango katika maendeleo ya jumuiya ya Afrika mashariki.
"Namshukuru Rais kupitia mamlaka zake kuturuhusu sisi kufanya mkutano huu,kwani hivi sasa mageuzi ya posta yanayoendelea kufanyika yamekuwa vivutio kwa posta zingine za EAC na kupitia mkutano huu tunatumia fursa kuonyesha namna ambavyo tunatoa huduma zetu kidigitali ili na wenyewe waweze kupata uzoefu katika nchi zao,"amesema
Ameongeza kuwa, huduma zote za posta wameziweka kidigitali hivi sasa na wanasafirisha vifurushi kupitia anuani za makazi na wateja wanapelekewa hadi majumbani kwao.