EAC yaipa UVRI rungu la kupambana na virusi vya Ebola, Marburg
Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia Miundombinu na Sekta za Jamii, Andrea Ariik akizungumza wakati wa uzinduzi wa taasisi hiyo nchini Uganda.
Arusha. Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zinatarajiwa kuimarisha uwezo wa kuzuia, kugundua na kukabiliana na milipuko ya magonjwa ya kuambukiza baada ya Taasisi ya Utafiti wa Virusi ya Uganda (UVRI) kuzinduliwa kuwa Kituo cha Ubora cha Kikanda cha EAC katika elimu ya virusi.
Kituo hicho kilichopo Entebbe kitakuwa kitovu cha utafiti wa virusi, mafunzo ya kimaabara, ufuatiliaji wa magonjwa na kuimarisha uwezo wa utambuzi na mwitikio wa haraka dhidi ya milipuko ya magonjwa kama Ebola na Marburg.
Uzinduzi huo umefanywa leo Alhamisi, Julai 23, 2026, na Waziri Mkuu wa Uganda, Robinah Nabbanja, aliyemwakilisha Rais Yoweri Museveni. Nabbanja amesema kuanzishwa kwa kituo hicho ni hatua muhimu ya kuimarisha usalama wa afya katika Afrika Mashariki na kusisitiza umuhimu wa kuongeza uwekezaji katika tafiti za kisayansi. "Kupitia hatua hii tumeona kwamba taifa linalochunguza vimelea vyake lenyewe ni taifa linalojitegemea. Serikali itaongeza ufadhili katika sekta ya utafiti," amesema.
Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la EAC na Naibu Waziri Mkuu wa kwanza wa Uganda, Rebecca Kadaga, amesema uzoefu wa janga la Uviko-19 umeonyesha kuwa hakuna nchi inayoweza kujilinda peke yake kwa kuwa magonjwa hayana mipaka.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa EAC anayeshughulikia miundombinu na sekta za jamii, Andrea Ariik Malueth, amesema kituo hicho ni miongoni mwa vituo saba vya ubora vilivyoainishwa chini ya Mfumo wa Kipaumbele wa Uwekezaji wa Afya wa EAC wa mwaka 2018–2028 ili kuimarisha uchunguzi wa magonjwa, tafiti na mwitikio wa haraka.
Uzinduzi huo umefanyika sambamba na maadhimisho ya miaka 90 ya UVRI. Kupitia ufadhili wa Serikali ya Ujerumani kupitia Benki ya Maendeleo ya KfW, kituo hicho kitapunguza muda wa majibu ya vipimo vya maabara kutoka saa 72 hadi saa nane.
Naye Naibu Balozi wa Ujerumani nchini Uganda, Peter Primus, amesema Serikali yake ipo katika hatua za mwisho za kununua maabara sita zinazobebeka zitakazosaidia utambuzi wa magonjwa ya kuambukiza na kukabiliana na usugu wa vimelea dhidi ya dawa (AMR), ikiwa ni sehemu ya ushirikiano wa muda mrefu kati ya Ujerumani na EAC.