Majaribio ya dawa za kutibu Ebola yaanza rasmi DRC
Muktasari:
- Kwa mujibu wa wataalamu, dalili za awali za Ebola hujitokeza ghafla na hufanana na za mafua na mtu hupata homa, maumivu ya kichwa na uchovu mkali, kadiri ugonjwa unavyoendelea, mgonjwa huanza kutapika na kuharisha
Dar es Salaam. Shirika la Afya Duniani (WHO) limeanza rasmi majaribio ya kitabibu ya dawa zinazolenga kutibu aina ya virusi vya Ebola vya Bundibugyo vinavyosababisha mlipuko wa ugonjwa unaoendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema hayo jana Alhamisi Julai 2, 2026 mjini Geneva kuwa mgonjwa wa kwanza tayari ameandikishwa kushiriki majaribio hayo, hatua inayotajwa kuwa muhimu katika jitihada za kupata tiba salama na yenye ufanisi dhidi ya ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa WHO, hadi sasa hakuna chanjo wala tiba iliyoidhinishwa dhidi ya aina ya virusi vya Bundibugyo, ambavyo ni miongoni mwa aina za Ebola zinazosababisha maambukizi makubwa na vifo.
Majaribio hayo yanafadhiliwa na WHO na kuratibiwa kwa ushirikiano kati ya Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Tiba ya DRC (Institut National de Recherche Biomédicale), Taasisi ya Tiba za Kitropiki ya Ubelgiji na Chuo Kikuu cha Oxford nchini Uingereza.
Tedros amesema majaribio ya dawa mbili yameanza rasmi baada ya mgonjwa wa kwanza kuandikishwa kushiriki, ingawa baadhi ya wagonjwa wamekuwa wakipona kupitia huduma za matibabu zinazotolewa, kupatikana kwa dawa salama na zenye ufanisi kutasaidia kuokoa maisha ya watu wengi zaidi.
Mlipuko wa sasa wa Ebola nchini DRC na Uganda ulianza Mei mwaka huu, huku WHO ikiutangaza kuwa dharura ya afya ya umma inayohitaji uangalizi wa kimataifa.
Takwimu za WHO zinaonesha hadi Juni 30, mwaka huu, DRC ilikuwa imerekodi wagonjwa 1,406 waliothibitishwa kuambukizwa Ebola na vifo 438.
Uganda nayo imeripoti wagonjwa 20 waliothibitishwa na vifo viwili hadi Julai 1, huku Ufaransa ikithibitisha mgonjwa mmoja maambukizi.
Ebola husababishwa na virusi vinavyoshambulia mfumo wa kinga na viungo mbalimbali vya mwili. Kwa kawaida huambukiza wanyama, hasa popo wanaokula matunda, lakini maambukizi kwa binadamu yanaweza kuanza pale watu wanapogusa au kushughulikia wanyama walioambukizwa.
Mtu aliyeambukizwa huanza kuwaambukiza wengine baada ya kuanza kuonesha dalili, ambazo huweza kujitokeza ndani ya siku mbili hadi 21 tangu maambukizi. Dalili za awali hufanana na za mafua au malaria, zikiwamo homa, maumivu ya kichwa na uchovu mkali.
Wataalamu wanaeleza kila aina ya virusi vya Ebola huhitaji chanjo yake maalumu. Hadi sasa, aina sita za virusi vya Ebola zimegunduliwa, lakini ni aina tatu pekee zinazojulikana kusababisha milipuko kwa binadamu.
Wajibu wa vyombo vya habari
Wakati juhudi za wataalamu kutafuta tiba zikiendelea, Jumuiya ya Afya ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA-HC) imezitaka vyombo vya habari kuzingatia maadili ya taaluma katika kuripoti milipuko ya magonjwa ili kuepusha kusambaza taarifa potofu zinazoweza kuhatarisha afya ya umma.
Katika mkutano wa mtandaoni uliofanyika Julai 2, 2026 na kuwakutanisha waandishi wa habari kutoka nchi wanachama wa ECSA-HC, wataalamu wa afya wamesisitiza umuhimu wa uandishi unaozingatia ushahidi wa kisayansi, muktadha na masilahi ya wananchi wakati wa kuripoti kuhusu mlipuko wa Ebola.
Mwanzilishi Mwenza wa Willow Health Media ya nchini Kenya, Dk Mercy Korrir, amesema uandishi wa habari za afya unapaswa kuongozwa na ukweli, uthibitishaji wa taarifa na ushahidi wa kisayansi badala ya uvumi au taarifa zisizothibitishwa.
Amesema waandishi wa habari wanapaswa kuthibitisha kila taarifa kutoka kwa vyanzo vya kuaminika kabla ya kuichapisha ili kuepusha kusambaza upotoshaji unaoweza kuhatarisha maisha ya watu.
"Kanuni yetu ya kwanza ni usahihi wa taarifa, kabla ya kuchapisha habari yoyote tunahakikisha imehakikiwa kutoka kwa wataalamu na taasisi husika.
“Hatufuati kelele za mitandaoni au misimamo ya kisiasa, bali tunafuata ushahidi wa kisayansi, upotoshaji wa taarifa unagharimu maisha ya watu, ndiyo maana ni muhimu kwa waandishi wa habari kuwa sehemu ya suluhisho, si sehemu ya tatizo," amesema Dk Korrir.
Kwa upande wake, Mtaalamu Mwandamizi wa Epidemiolojia wa ECSA-HC, Dk Mohamed Mohamed, amesema vyombo vya habari vinapaswa kuangalia ubora wa hatua zinazochukuliwa katika vituo vya mipakani badala ya kuripoti idadi ya wasafiri wanaokaguliwa pekee.
Amesema waandishi wanapaswa kufuatilia kama mifumo ya uchunguzi, uthibitishaji wa wagonjwa, utenganishaji wa washukiwa na ufuatiliaji wa watu waliokutana na wagonjwa inatekelezwa kwa ufanisi.
"Mipaka si maeneo ya kupima joto la mwili pekee, bali ni vituo vya tahadhari ya mapema na uratibu wa kudhibiti mlipuko.
“Waandishi wa habari wanapaswa kufuatilia mnyororo mzima wa mwitikio ili wananchi wapate picha halisi ya hatua zinazochukuliwa kuzuia kuenea kwa Ebola," amesema Dk Mohamed.