Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanzania haina ugonjwa wa Ebola, Serikali yaongeza ulinzi mipakani

Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo Alhamisi, Juni, 18 2026. Picha na Eldaima Mangela.

Muktasari:

  • Katika taarifa yake Waziri amesema hadi kufikia Juni 18,2026, Tanzania haikuwa na mgonjwa wa Ebola aliyeripotiwa nchini na hali ya usalama wa afya inaendelea kuwa nzuri.

Dodoma. Serikali imesema hadi sasa Tanzania haina mgonjwa wa Ebola na imesisitiza wananchi kuendelea kuchukua hatua za kuwalinda wananchi wake.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma ambapo amesisitiza kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha utayari wa kukabiliana na ugonjwa huo, kutokana na mlipuko unaoendelea kuripotiwa katika nchi jirani za Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Katika taarifa yake Waziri amesema hadi kufikia Juni 18,2026, Tanzania haikuwa na mgonjwa wa Ebola aliyeripotiwa nchini na hali ya usalama wa afya inaendelea kuwa nzuri. "Napenda kuwafahamisha wananchi kuwa hadi sasa nchi yetu haina mgonjwa wa Ebola na Serikali imejipanga kikamilifu kuzuia, kugundua mapema na kudhibiti tishio lolote linaloweza kuhatarisha afya za Watanzania," amesema Mchengerwa.

Waziri Mchengerwa ametoa taarifa hiyo akiwa ameambatana na Naibu Waziri wa Afya, Dk Florence Samizi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Seif Shekalaghe, Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Grace Magembe, Dk Erasto Sylvanus na Menejimenti ya Wizara ya Afya, amesema Serikali imeendelea kuimarisha uchunguzi katika mipaka, viwanja vya ndege, bandari sambamba na kutoa miongozo kwa wataalam wa afya na wananchi.

Kwa mujibu wa Waziri, tangu kutangazwa kwa tishio hilo, tetesi 64 kutoka mikoa 21 zimeripotiwa na kufanyiwa uchunguzi ambapo wahisiwa 11 walikidhi vigezo vya uchunguzi na kuchukuliwa sampuli zilizothibitisha kutokuwa na maambukizi ya ugonjwa wa Ebola.

Amesema hatua zote muhimu zinaendelea kuchukuliwa ili kuhakikisha usalama wa wananchi na wataalamu wa afya hapa unakuwa wa hali ya juu ili kulinda na kuzuia ugonjwa huo.

Ameahidi kuwa Serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa ugonjwa huo na kutoa taarifa za uwazi kwa wananchi kadri itakavyohitajika ili kila mmoja achukue tahadhari.

Katika hatua nyingine Waziri amewataka wananchi kuendelea kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa afya na kufuatilia taarifa kutoka vyanzo rasmi vya Serikali, lakini waepuke kueneza taarifa ambazo hazijathibitishwa kwa lengo la kuendelea kuilinda Tanzania dhidi ya tishio la Ebola.