Elimu ya CCM kuhusu uwekezaji wa bandari yahamia kaskazini

Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Manyara, Peter Toima akizungumza mjini Babati juu ya mkutano wa Katibu mkuu wa CCM, Daniel Chongolo unaotarajiwa kufanyika uwanja wa sheikh Amri Abeid jijini Arusha. Picha na Joseph Lyimo

Muktasari:

  • Lengo la mkutano huo unaotarajiwa kufanyika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha ni viongozi wa CCM kuelezea kwa wanachama na wakereketwa wa CCM kanda ya kaskazini kuhusu faida ya uwekezaji wa bandari.

Babati. Katibu Mku wa CCM, Daniel Chongolo kesho atawahutubia wanachama na viongozi wa chama hicho wa mikoa ya Manyara, Arusha na Kilimanjaro katika mkutano wa hadhara utakaofanyika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha.

Lengo la mkutano huo ni kuwajengea uelewa kuhusu mkataba wa makubaliano ya ushirikiano wa kijamii na kiuchumi baina ya Serikali ya Tanzania na ya Dubai, yanayohusisha uwekezaji katika bandari ya Dar es Salaam.

Mkutano huo ni mwendelezo wa kiongozi huyo, baada ya kuifanya katika mikoa ya nyanda za juu kusini (Mbeya, Njombe na Iringa), uliofanyika uwanja wa Ruanda Nzovwe Jijini Mbeya. Pia Chongolo aliyeambata na mawaziri wa sekta ya uchukuzi alifanya hivyo kwa mikoa ya Mtwara na Lindi.

Mwenyekiti wa CCM wa mkoa wa Manyara, Peter Toima amewaambia wanahabari leo Ijumaa Julai 21, 2023 mjini Babati mkoani Manyara kuwa maandalizi ya mkutano huo yamekamilika huku akiwataka wanachama wa mikoa hiyo kuhudhuria kwa wingi.


Toima amesema kupitia mkutano huo wanachama na viongozi wa CCM Arusha, Kilimanjaro na Manyara, watapata uelewa sahihi kuhusu suala la uwekezaji wa bandari ya Dar es salaam lililoibua mjadala hadi sasa.

“Lengo ni kuondoa mijadala potofu iliyoenea kwenye mitandao ya kijamii kuwa bandari ya Dar es Salaam imeuzwa ilihali siyo jambo la kweli.Suala la uwekezaji lipo kwenye ilani ya uchaguzi wa CCM wa mwaka 2020/2025, " amesema Toima.

Toima amesema wanachama na viongozi wa CCM wa kanda ya kaskazini, wanapaswa kushiriki  kwenye mkutano ili kumsikiliza Chongolo na kwenda kuyaeneza kwenye matawi na mashina.

Katibu mwenezi wa CCM wilaya ya Simanjiro, Mosses Makeseni amesema wameshatoa taarifa kwa viongozi wa kata zote ili kuhakikisha wanajitokeza kwenye mkutano huo.