Ewura yatoa msaada wa vifaa tiba vya Sh5.2 milioni

Mwenyekiti wa Baraza la wafanyakazi wa Ewura, Poline Msuya (Wa kwanza kushoto) akimkabidhi mfano wa hundi Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi (wa pili kushoto) pamoja na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Dk Sebastian Pima (wa pili kulia) yenye thamani ya fedha ya ununuzi wa vifaa tiba katika Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana. Wa kwanza kulia ni Mwenyekiti wa Tughe tawi la Ewura, Victor Laba.
Muktasari:
- Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Umeme (Ewura) imetoa msaada wa vifaa tiba hospitali ya Nyamagana jijini Mwanza ambavyo vitasaidia upatikanaji bora wa huduma za afya hasa kwa wanawake wajawazito ambao kwa mwezi zaidi ya wanawake 650 mpaka 750 hujifungua hospitalini hapo.
Mwanza. Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Umeme (Ewura) imetoa msaada wa vifaa tiba katika Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana vyenye thamani ya zaidi ya Sh5.2 milioni.
Miongoni mwa vifaa vilivyotolewa ni mashine sita za kupima presha (Bp Machine) zinazogharimu Sh426,000, viti viwili vya wagonjwa vyenye thamani ya Sh709,000, vitanda vya uchunguzi vinne vyenye thamani ya zaidi ya Sh1.9 milioni na vifaa vya kujifungulia vyenye thamani ya zaidi ya Sh2.1 milioni.
Akizungumza leo Jumatano, Februari 8, 2023 katika kikao cha tano cha baraza la wafanyakazi wa Ewura kilichofanyika jijini Mwanza, Mwenyekiti wa baraza hilo, Poline Msuya amesema taasisi hiyo ya umma imekuwa na utaratibu wa kutoa msaada kwa jamii kila inapowezekana.
“Ni Imani yetu kuwa mchango huu kwa hospitali utasaidia kuokoa maisha ya Watanzania wenzetu na pia kuboresha huduma ya utoaji afya katika Mkoa wa Mwanza,”amesema
Vifaa hivyo vitapunguza changamoto ya vifaa tiba hospitalini hapo ambapo kwa mujibu wa Mganga Mkuu Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Dk Sebastian Pima wanawake wajawazito kati ya 650 hadi 750 hujifungua katika hospitali hiyo kwa mwezi.
“Kitakwimu ukienda kuangalia idadi ya kina mama wanaojifungua ndani ya Mkoa wa Mwanza hospitali yetu ndiyo inaongoza,” amesema Dk Pima.
Amesema hospitali hiyo pia inahudumia wanawake wajawazito wanaoudhuria kliniki kati ya 3,500 hadi 5,000 kwa mwezi huku ikipokea wagonjwa wa nje kati ya 8,000 hadi 12,000 ndani ya mwezi mmoja.
“Sisi hatujiendeshi kwa faida wala hatufanyi biashara, Sera ya Afya inasema huduma ya afya kwa kina mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano ni bure, sehemu nyingine watatakiwa kuchangia watatozwa kwahiyo sehemu pekee ambayo ni kimbilio lao kwa mujibu wa miongozo ya Serikali ni Butimba jiji (hospitali ya Nyamagana). Ewura mmeaona hilo na kupeleka huduma pale wananchi wanapohitaji,” amesema Dk Pima.
Akizungumzia lengo la kikao cha baraza hilo, Msuya amesema baraza hilo ni moja ya nyenzo muhimu katika kuhakikisha malengo ya upatikanaji wa huduma zinazodhibitiwa na Ewura ambazo ni huduma za nishati na maji zinapatikana kwa wakati na kwa gharama nafuu yanafanikiwa.
“Katika kikao hiki, baraza linalenga kujadili mwenendo wa utekelezaji wa huduma za udhibiti wa nishati na maji nchini pamoja na bajeti ya taasisi kwa mwaka wa fedha 2023/24,”amesema
Akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi amesema Taifa linaitegemea mamlaka hiyo kufanya kazi kwa weledi na kasi ili kuleta unafuu wa utoaji wa huduma na huduma zenye ubora kwa wananchi katika sekta ya nishati na maji.
“Ninawashukuru kwa utendaji wenu ambao hadi sasa umeendelea kuweka alama njema ya kuigwa katika uwajibikaji nchini, ni vyema kuzingatia uwazi katika upimaji wa utendaji wa wafanyakazi na kuhakikisha utekelezaji wa majukumu unakwenda sanjari na thamani halisi ya rasilimali zilizopo,” amesema.
Ameishukuru mamlaka hiyo kwa kutoa vifaa tiba na kumtaka Mganga Mkuu wa jijini Mwanza kuhakikisha misaada hiyo inalenge kuimarisha huduma kama ilivyokusudiwa.