Ewura yavipiga rungu vituo viwili Dodoma
Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano Ewura Titus Kaguo akuzungumza na wanahabari kuhusu kuvifungia vituo viwili vya mafuta vya jijini Dodoma.
Muktasari:
- Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), imewataka watoa huduma wamiliki wa vituo vya mafuta kufuata kanuni na taratibu za leseni, watakaobainika kukiuka hatua kali zitaendelea kuchukuliwa.
Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imevifungia vituo viwili vya mafuta mkoani Dodoma baada ya kubainika kusababisha changamoto ya upungufu wa mafuta.
Hadi kufikia Septemba 29, mwaka huu Ewura ilikuwa imeshavifungia vituo saba kwa muda wa miezi sita kutotoa huduma kwa makosa ya kuhodhi mafuta kinyume cha sheria.
Septemba 18, mwaka huu mamlaka hiyo ilitangaza kuvifungia vituo vitatu katika mikoa tofauti huku Octoba Mosi ikitangaza kuvifungia tena vituo viwili mkoani Dododoma.
Akizungumza na wanahabari leo Jumanne Oktoba 10, 2023 Meneja Mawasiliano na Uhusiano (Ewura) Titus Kaguo amevitaja vituo vilivyofungiwa kuwa ni Kipenda Roho Investment na Oilcom vilivyopo Wila ya Chemba mkoani Dodoma.
"Bodi ya Wakurugenzi hadi sasa itakuwa imegusa vituo tisa na bado uchunguzi unaendelea kwa vituo vingine," amesema Kaguo.
Amesema Ewura itaendelea na uchunguzi wa vituo vingine zaidi ikiwa ni pamoja na kuwapa fursa ya kuwasilisha utetezi wao ndani ya siku 21.
"Katika kikao kilichofanyika jana Oktoba 9, Bodi ya Wakurugenzi ya Ewura ilijiridhisha pasipo shaka kuwa vituo hivyo vilitenda kosa la kuhodhi mafuta kati ya Julai na Agosti mwaka huu hivyo kuamua vifungwe kwa miezi sita," amesema.
Akizungumzia sababu za upungufu wa mafuta kwa baadhi ya mikoa Kaguo alisema, pamoja na kuwepo kwa mafuta katika maeneo mbalimbali baadhi ya wamiliki wa vituo kuamua kuhodhi mafuta ili kujipatia maslahi haramu ikiwemo faida kubwa kutokana na ongezeko la bei.
“Kutokana na hali hiyo mamlaka hiyo imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kisheria ikiwemo kuvifungia baadhi ya vituo, vilivyobainitika kuficha mfauta kinyume na kanuni na miongozo inayosimamia biashara ya mafuta nchini,” amesema.
Aidha mamlaka hiyo inaendelea kuwakumbusha wafanyabiashara wote wa mafuta nchini kuhakikisha wanaendesha biashara zao kwa mujibu wa sheria, kanuni na miongozo inayosimamia biashara ya nafuta nchini.