Faida za ulaji wa mboga ya mchunga
Muktasari:
- Mboga ya mchunga ina kitu cha kipekee kwa ajili ya mwili wa binadamu kutokana na uchungu uliopo.
Dar es Salaam. Mboga za majani rangi ya kijani huwa na faida nyingi mwilini.
Miongoni mwa mboga hizo ni mchunga ambao baadhi ya watu hawapendelei kuutumia kutokana na uchungu uliopo, lakini uchungu huo ni mzuri katika mwili wa binadamu.
Mtaalamu wa mimea asili na virutubisho tiba kutoka taasisi ya Fadhaget Nutrition Science, Dk Fadhili Emily anasema mboga za majani, hasa zile zenye rangi ya kijani zina faida nyingi.
Anasema kuna baadhi ya mboga za majani walizifanyia utafiti na kugundua zina kitu cha ziada na miongoni wa mboga hizo ni mchunga.
“Hii mboga haipewi kipaumbele, lakini ni mboga nzuri kwa watu wanaotaka kulinda afya zao kwa sababu zina kiwango kikubwa cha madini, vitamini na virutubisho vingi.
“Mwili wa binadamu hauwezi kutengeneza vitamini A pekee, badala yake hutengeneza vitamini hiyo kupitia vyakula anavyokula,” anaeleza.
Anasema vyakula vinavyotengenza vitamini A ni mboga za majani zenye rangi ya kijani pamoja na matunda, hivyo kila mmoja ana wajibu wa kula vyakula hivyo kwa ajili ya kujikinga na maradhi.
“Mboga ya mchunga ina kitu cha kipekee kwa ajili ya mwili wa binadamu kutokana na uchungu uliopo.
“Hata ukitumia nje ya mfumo wa chakula, husaidia kutibu magonjwa mbalimbali, ikiwemo vidonda kwa sababu una kiwango kikubwa cha madini ya chuma, vitamini A na virutubisho muhimu,” anafafanua.
Faida nyingine ni kusafisha damu, kuondoa sumu kuvu mwilini na pia husaidia kuimarisha kinga inayosaidia fangasi kuondoka.
Pia ulaji wa mchunga mara kwa mara husaidia mwili kuepukana na changamoto za kiafya kwa sababu mboga hiyo ni moja kati ya mboga muhimu ambazo zikitumika vizuri huzuia matatizo hayo.