Faida za waathirika wa ukatili kupata haki chini ya paa moja
Muktasari:
- Jamii inapaswa kupata elimu ya kutosha kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia ili kuhakikisha kesi haziishii njiani.
Dar es Salaam. Kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia, safari ya kutafuta haki mara nyingi huanza na hofu, maumivu na sintofahamu.
Wengi hujikuta wakikabiliana na majeraha ya mwili na nafsi, huku wakihitaji msaada wa haraka ili kurejea katika maisha ya kawaida.
Katika mazingira hayo, Kituo cha Huduma Jumuishi cha Mwananyamala kimeendelea kuwa sehemu muhimu ya matumaini kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia jijini Dar es Salaam na maeneo jirani.
Hivi karibuni, Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) kupitia Mradi wa Sauti Zetu, kilifanya ziara katika kituo hicho kujifunza namna kinavyotoa huduma kwa waathirika na kusimamia mchakato wa haki kwa wale walioathiriwa na ukatili wa kijinsia.
Ziara iliwapa wanahabari fursa ya kuona namna huduma zinavyounganishwa katika eneo moja ili waathirika wapate msaada wa kitabibu, kisheria na kisaikolojia bila kulazimika kuhangaika kutoka taasisi moja kwenda nyingine.
Awali, wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Sauti Zetu, Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Dk Rose Reuben, alieleza kuwa mradi huo umebeba dhamira ya kuongeza uelewa wa jamii kuhusu aina za ukatili, hususani unaofanyika katika mifumo ya kidijitali.
“Kupitia mradi wa Sauti Zetu, Tamwa inapaza sauti kwa kutoa elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia mtandaoni, unaowalenga wanawake na watoto kutokana na ukweli kwamba, kundi hili mara nyingi hukosa uelewa wa kutosha kuhusu madhara na namna ya kujilinda,” alisema.
Kauli hiyo inaakisi umuhimu wa kuongeza uelewa wa jamii wakati ambao teknolojia imekuwa sehemu ya maisha ya kila siku na kufungua milango mipya ya ukatili, unaoweza kuathiri usalama, utu na haki za wanawake na watoto.
Safari huanzia hapa
Mwathirika anapofika Kituo cha Huduma Jumuishi Mwananyamala, hupokewa na wataalamu wenye mafunzo maalumu ya kushughulikia masuala ya ukatili wa kijinsia.
Hatua ya kwanza ni kusikiliza maelezo yake faragha, ili kubaini aina ya msaada anaohitaji kwa haraka.
Baada ya hapo hufanyika uchunguzi wa kitabibu ili kutathmini madhara yaliyotokana na tukio husika, pamoja na kuhifadhi ushahidi unaoweza kutumika katika hatua za kisheria.
Sambamba na huduma hizo, mwathirika hupatiwa ushauri nasaha ili kumsaidia kuanza safari ya kupona kutokana na athari za tukio alilopitia.
Dk Yusuph Kashoro, anayehudumu katika kituo hicho, anasema kuripoti mapema ni hatua muhimu kwa mwathirika ili kupata msaada stahiki.
“Tunatoa elimu na ushauri kwa mwathirika na tunasisitiza kuripoti ukatili wa kijinsia mapema ili kupata msaada wa haraka na kurejea katika hali ya kawaida,” anasema.
Kwa mujibu wa daktari huyo, kuchelewa kuripoti kunaweza kuathiri matibabu na wakati mwingine kupunguza uwezekano wa kupata ushahidi muhimu kwa ajili ya kesi.
Haki inaanzia kwenye taarifa
Baada ya huduma za awali, wataalamu wa sheria na vyombo vya dola huingia kusaidia uchunguzi na mchakato wa kufikisha kesi kwenye mamlaka husika.
Hata hivyo, changamoto inayobaki ni ukosefu wa elimu kwa jamii kuhusu ukatili wa kijinsia na haki za mwathirika.
Mwanasheria katika kituo hicho, Ramadhani Kisengo anasema baadhi ya kesi hushindwa kufika mwisho kutokana na uelewa mdogo wa wananchi.
“Jamii yetu bado haina elimu ya kutosha kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia. Hali hii husababisha kesi nyingi kuishia njiani huku baadhi ya wazazi wakiziachilia kutokana na vitisho mbalimbali. Hivyo, kuna uhitaji mkubwa wa kuongeza elimu ya kisheria kwa jamii,” anasema.
Anabainisha kuwa baadhi ya familia huamua kumaliza kesi kwa makubaliano yasiyo rasmi, jambo linalowanyima waathirika haki na kuwapa nafasi wahalifu kuendelea kufanya ukatili.
Ukatili wa watu wa karibu
Taarifa zilizowasilishwa wakati wa ziara hiyo zinaonyesha kuwa wahusika wa matukio mengi ya ukatili wa kijinsia si wageni, bali ni watu wanaofahamika kwa waathirika.
Ofisa wa Dawati la Jinsia na Watoto, Nicodemus Kimario anasema hali hiyo imeendelea kuwa changamoto kubwa katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia.
“Asilimia kubwa ya waathirika wanaripotiwa kubakwa au kulawitiwa na mara nyingi wahusika huwa ni watu wa karibu ndani ya familia,” anasema.
Kauli hiyo inaonyesha umuhimu wa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuwa karibu na watoto na kuwajengea mazingira salama ya kutoa taarifa wanapokumbana na vitendo vya ukatili.
Kurejesha matumaini
Kwa mtazamo wa mwandishi, Kituo cha Huduma Jumuishi Mwananyamala ni zaidi ya eneo la kutolea huduma. Ni ngome ya matumaini kwa waathirika ambao mara nyingi hufika wakiwa wamekata tamaa na kuondoka wakiwa na matumaini ya kupona na kupata haki.
Kituo hiki kinaonyesha jinsi ushirikiano kati ya sekta ya afya, vyombo vya sheria, ustawi wa jamii na wadau wa maendeleo unavyoweza kuleta matokeo chanya katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia.
Hata hivyo, mafanikio ya mapambano hayo hayatategemea uwepo wa vituo pekee, bali pia elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kuripoti matukio ya ukatili mapema na kuyafikisha kwenye vyombo vya sheria.
Kadiri jamii itakavyozidi kuelewa haki za waathirika na wajibu wake katika kupinga ukatili, ndivyo safari ya haki itakavyokuwa rahisi zaidi kwa maelfu ya waathirika wanaohitaji msaada kila mwaka.
Ndani ya kituo hicho, safari hiyo ya matumaini inaendelea kila siku ikilenga kurejesha utu, kuponya majeraha na kuhakikisha waathirika wanapata haki wanayostahili.