Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kuchukua sheria mkononi kwaongoza uvunjaji wa haki za binadamu

Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Ellen Rwijage, akizungumza na wanahabari kuhusu haki na wajibu wa raia katika kulinda na kuheshimu mali zao pamoja na umuhimu wa kuzingatia sheria.

Muktasari:

  • Tume yasema wananchi wengi hukiuka haki za wengine kutokana na kutokujua sheria na wajibu wao.

Dar es Salaam. Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imesema tabia ya wananchi kujichukulia sheria mkononi ni miongoni mwa sababu zinazoongoza ukiukwaji wa haki za binadamu nchini.

Imesema hali hiyo inachangiwa na uelewa mdogo wa sheria pamoja na kutotimiza wajibu wa kila mmoja.

Tume hiyo imewataka wananchi kutumia vyombo vya sheria na taasisi husika kutafuta haki badala ya kuchukua sheria mikononi mwao wanapoona wametendewa isivyo.

Akizungumza leo Ijumaa, Julai 3, 2026, katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF) yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa THBUB, Ellen Rwijage amesema ukiukwaji wa haki za binadamu unaweza kupungua ikiwa wananchi watazingatia sheria na kutumia mifumo rasmi ya kutafuta haki.

"Uvunjaji wa haki za binadamu mara nyingi unasababishwa na wananchi kujichukulia sheria mikononi. Tunawasihi Watanzania kufuata taratibu za kisheria na kutumia taasisi zilizopo kutafuta haki zao," amesema.

Rwijage amesema pamoja na kutambua haki zao, wananchi wanapaswa kufahamu kuwa kila haki inaambatana na wajibu.

"Ili udai haki ni lazima utimize wajibu wako. Haki na wajibu vyote vimeainishwa kisheria. Tukitimiza wajibu wetu ipasavyo, tutalinda haki zetu na idadi ya malalamiko itapungua," amesema.

Kauli hiyo inakuja wakati takwimu za Ripoti ya Vifo na Visababishi vya Vifo ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ya mwaka 2024 zinaonyesha kuwa kati ya watu 2,264 waliofariki dunia kutokana na vifo vya nje mwaka huo, 405 walikufa baada ya wananchi kujichukulia sheria mkononi.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, zilizotokana na Jeshi la Polisi, wanaume walikuwa waathirika wakubwa, wakifikia 1,682, sawa na asilimia 74.3 ya vifo vyote vilivyoripotiwa.

Rwijage amesema kutokana na kuwepo kwa pengo la uelewa kuhusu haki za binadamu na sheria, THBUB imeendelea kutoa elimu kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.

Amesema kadiri elimu hiyo inavyozidi kutolewa, ndivyo mwamko wa wananchi unavyoongezeka na kusababisha watu wengi zaidi kufika katika ofisi za Tume kuwasilisha malalamiko yao.

"Hata hapa katika banda letu, moja ya huduma tunazotoa ni kupokea malalamiko ya ukiukwaji wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora. Wananchi wanaotembelea banda hili wanaweza kuwasilisha malalamiko yanayohusu ukiukwaji wa haki za binadamu, matumizi mabaya ya madaraka na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora," amesema.

Hata hivyo, amesema si kila anayefika katika Tume hiyo huwa amevunjiwa haki. Wapo wanaokosa uelewa wa sheria au hawafahamu taasisi yenye mamlaka ya kushughulikia changamoto zinazowakabili.

"Tunapokutana na hali hiyo, tunawapa elimu na kuwaelekeza katika taasisi husika ili wapate huduma kwa wakati," amesema.

Amesema ili kuimarisha ulinzi wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora, THBUB inaendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi za Serikali, asasi za kiraia, mashirika ya kimataifa pamoja na wananchi.

"Tume iko wazi kwa kila mwananchi. Kupitia ushirikiano huu tumefanikiwa kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuwasaidia kupata haki zao kwa mujibu wa sheria," amesema.

Rwijage amesema hakuna mtu aliye juu ya sheria na kusisitiza kuwa viongozi pamoja na watumishi wa umma, wanapaswa kuzingatia misingi ya utawala bora katika utekelezaji wa majukumu yao.

"Katiba yetu inaelekeza nchi kuongozwa kwa misingi ya utawala wa sheria. Hivyo, yeyote atakayekiuka sheria, bila kujali nafasi yake, sheria zitachukua mkondo wake," amesema.

Mmoja wa wananchi waliotembelea banda la THBUB katika maonesho hayo, Mathayo Mujuni, amesema elimu kuhusu haki za binadamu inapaswa kutolewa kwa kina zaidi ili wananchi waelewe kuwa haki na wajibu vinapaswa kwenda sambamba.

"Kuna baadhi ya matukio watu wanaona ni vigumu kuacha kujichukulia sheria mikononi. Ni muhimu elimu hii ikaendelea kutolewa kwa kina ili ibadili mtazamo wa wananchi," amesema.