Feleshi, wadau wafunguka utata wa kujiuzulu Ndugai

Muktasari:

Wakati kukiwa na mjadala kuhusu utaratibu uliotumiwa na aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai kujiuzulu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Eliezer Feleshi amefafanua kuwa utaratibu uliotumika kupeleka taarifa kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) ulikuwa sahihi.

Moshi. Wakati kukiwa na mjadala kuhusu utaratibu uliotumiwa na aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai kujiuzulu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Eliezer Feleshi amefafanua kuwa utaratibu uliotumika kupeleka taarifa kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) ulikuwa sahihi.

Taarifa ya Ndugai mwenyewe ambaye pia ni mbunge wa Kongwa (CCM) ya juzi ilisema alikuwa ameandika barua kwenda kwa Katibu Mkuu wa CCM na kwamba nakala ya barua hiyo alikuwa ameiwasilisha kwa Katibu wa Bunge.

Kutokana na hatua hiyo, mjadala umekuwa ukiendelea juu ya uhalali wa barua hiyo kuelekezwa kwa Katibu wa CCM badala ya Bunge, huku baadhi ya watu wakiweka wazi kuwa Katiba ya Tanzania inataka taarifa ya kujiuzulu kwa Spika iwasilishwe kwa maandishi bungeni na si kwa Katibu Mkuu wa CCM.

Akifafanua suala hilo jana kwa simu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Feleshi alisema mjadala huo usingekuwepo kama wanaotoa hoja wangekuwa wamesoma aina ya wabunge na Spika anavyopatikana.

“Naomba uelewe dhana zifuatazo na hapa sio ushabiki. Barua ya mwajiriwa yeyote kwa kawaida huandikwa kwa kupitia kwa msimamizi wa kazi kwenda kwenye mamlaka inayohusika.

“Kwa mifumo yetu sisi huwezi ukapata mbunge na ukapata Spika ambaye jina lake halikutolewa na chama cha siasa. Ni kwa mantiki hiyo A na B ukiziunganisha kama ni kisheria huwezi ukakuta kosa kokote pale.”

“Angeweza akaandika barua kwa Katibu wa Bunge kupitia Katibu wa CCM na katibu ambaye ndio dhamana ya udhamini angeweza akaamua kuipeleka kwanza kwenye mamlaka za ndani ya chama kabla ya kuipeleka.

“Sasa ni kwa mantiki hiyo hiyo ndio unamsikia sasa Chongolo anapoipokea wanabaki na dhamana yao wao kwa sababu Katiba yetu ni lazima huyu mtu awe na udhamini wa mgombea, ni kupitia chama cha siasa.

“Na ndiyo maana unamsikia Katibu wa Bunge anasema nimepata nakala yangu lakini hata kama asingeenda kwa Katibu wa chama lazima Katibu wa Bunge angefanya uhakiki na Katibu wa chama kilichomdhamini”.


Wadau wafunguka

Mratibu wa Mashirika ya Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Wakili Onesmo ole Ngurumwa alisema utaratibu aliotumia Spika kuandika barua kwenda kwa Katibu wa CCM ulikiuka Katiba na unachochea haki ya kudai Katiba mpya.

“Kwa ujumla kuondoka kwa Ndugai kwa mambo aliyoyafanya miaka yote ni sawa kabisa, ila mchakato uliotumika na namna alivyoondoka unakwenda kuvunja uhuru wa Bunge. Katiba imeelekeza wazi kuwa taarifa inatolewa kwa nani,” alisisitiza.


Utaratibu alioutumia Ndugai

Katika taarifa yake kwa umma, Ndugai alisema ameandika barua hiyo kwenda kwa Katibu wa CCM na kwamba uamuzi huo ulikuwa ni binafsi na ameufanya kwa kuzingatia na kujali maslahi mapana zaidi ya taifa, serikali na CCM.

“Pia nakala ya barua yangu hiyo ya kujiuzulu nimewasilisha kwa Katibu wa Bunge kwa ajili ya hatua stahiki kwa mujibu wa Katiba ya nchi na sheria nyingine husika ili kuwezesha mchakato wa kumpata Spika mwingine uweze kuanza,” alisema.

Kupitia taarifa ya Ofisa habari, ofisi ya Katibu mkuu CCM, Said Nguya ya juzi, aliujulisha umma kuwa Katibu Mkuu huyo, Daniel Chongolo amepokea barua ya Ndugai na kwamba mchakato wa kujaza nafasi hiyo unaendelea.

Siku hiyo hiyo, Bunge nalo likatoa taarifa kwa umma ikiwataarifu kuwa Katibu wa Bunge alikuwa amepokea nakala ya barua ya Ndugai ya kujiuzulu uspika ambayo alimpelekea Katibu Mkuu wa CCM ambacho ndicho chama kilichomdhamini.

Jana Katibu wa Bunge akatoa taarifa nyingine kwa umma akisema taratibu za kujaza nafasi hiyo zinaendelea na kwamba kwa mujibu wa Katiba, kama spika anakuwa hayupo, basi shughuli nyingine zote za Bunge husimama.

“Kwa Mujibu wa Ibara ya 84(1) ya Katiba, Spika ndiye Kiongozi wa Bunge na ndiye msimamizi wa shughuli zote za Bunge,” alisema na kuongeza Ibara ya 84(8) inasema kiti kinapokuwa wazi shughuli husimama isipokuwa uchaguzi wa Spika.

Kutokana na takwa hilo la Kikatiba, Kamati zilizokuwa zikutane kuanzia Januari 10, 2022 na zilizotakiwa kukutana kuanzia Januari 17, 2022 sasa hazitakutana na badala yake zitakutana wakati wa mkutano wa Bunge wa Februari 1 hadi 11.


Katiba, Kanuni

Ibara ya 149 imeweka masharti ya namna mtu yeyote mwenye dhamana ya kazi yoyote iliyoanzishwa na Katiba anavyoweza kujiuzulu na atafanya hivyo kwa kutoa taarifa iliyoandikwa na kutiwa saini kwa mkono wake mwenyewe.

Kazi hiyo ni pamoja na kazi ya Waziri, Naibu Waziri au Mbunge, isipokuwa mbunge ambaye ni mbunge kwa mujibu wa madaraka ya kazi yake.

Ibara ya 149 (a) iwapo mtu huyo aliteuliwa au alichaguliwa na mtu mmoja, basi taarifa atawasilisha kwa mtu huyo aliyemteua au kumchagua, au iwapo aliteuliwa au alichaguliwa na kikao cha watu, taarifa hiyo ataiwasilisha kwenye kikao hicho. Lakini ibara ndogo ya (c) inasema iwapo mtu huyo ni Spika au Naibu Spika wa Bunge basi taarifa ya kujiuzulu ataiwasilisha kwenye Bunge, lakini Ndugai yeye aliamua kuiwasilisha taarifa kwa Katibu Mkuu CCM na kuzua utata.

Kanuni za Kudumu za Bunge toleo la 2020, haizungumzii Spika wa Bunge kujiuzulu katika mazingira kama yaliyotokea kwa Ndugai, bali ni pale ambapo kunakuwa na hoja ya Mbunge iliyowasilishwa bungeni ya kumwondoa Spika akiwa na tuhuma.

Kulingana na kanuni ya 158(6), Spika anayetuhumiwa anaweza kujiuzulu kwa kutoa maelezo ya kujiuzulu kwake bungeni kabla ya uamuzi juu ya hoja ya kuondolewa madarakani haijaamuliwa kwa kura na Bunge, lakini kwa sasa hakuna hoja hiyo.