Fisi ‘wafyeka’ mabaki ya Simba Bob Jr, historia yake kuwekwa makumbusho

Arusha. Simba maarufu aliyepewa jina la "Bob Jr" aliyekuwa anaishi katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti eneo la Namiri ameuawa katika mapigano ya kugombea kuongeza kundi.
Kwa kawaida simba dume wamekuwa na tabia ya kugombana na kugombea kuongeza kundi na simba ambaye hushinda ndio huwa kiongozi.

Simba huyo ameuawa akiwa na miaka 12 baada ya kuongoza kundi kwa miaka mitano lakini safari hii amepigwa na Simba watano hadi kumuuwa na hivyo kumuondoa katika uongozi.
Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), William Mwakilema akizungumza na waandishi wa habari Machi 15, 2023 ameeleza kuwa tukio hilo lilitokea hivi karibuni na limetokana na ushindani unaotokea baina ya jamii za simba ili kupata nafasi nafasi ya kuwa kiongozi.

Kamishna Mwakilema ameeleza kuwa baada ya kugundulika juu ya kifo cha Simba Junior, mamlaka ilitamani kuhifadhi mwili wake katika majumba Ya historia lakini imeshindikana kutokana na simba huyo kushambuliwa vikali na baadaye wanyama aina ya fisi walikula masalia ya simba huyo.

Amesema Simba Bob Jr alizaliwa mwaka 2010 na amekuwa kiongozi  katika eneo hilo la Namiri Ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

"Simba huyu amekufa kutokana na kuwa kiongozi kwa muda mrefu na hivyo ameshindwa kutetea uongozi wake kutokana na kuwa dhaifu na umri mkubwa," amesema.
Amesema Tanapa haitakuwa na mazishi ya aina yoyote kwani kwa kawaida kifo kilikuwa cha asili na cha kiikolojia kuwa mnyama akifa huachwa porini na kugeuka kuwa chakula cha wanyama wengine.

Jina la Bob Jr kwa simba huyo limetokana na wingi wa nywele ambazo zilifananishwa na nywele za  mwanamuziki Hayati Bob Marley.

Baadhi ya waongoza utalii wameeleza simba huyo alikuwa kivutio kikubwa ndani ya Serengeti.

John Minja amesema walitamani Tanapa kutunza historia na picha za simba huyo kutokana na umaarufu wake.