Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Furaha ya Anna yaanza kurejea

Anna Zambi akiwa na wanasheria wa Serikali kutoka RIta, Emmanuela Mwingira na Julius Msengezi wakati wa sherehe za mahafali ya kidato cha sita

Muktasari:

Mungu hamtupi mja wake. Ndivyo unavyoweza kusema katika maisha ya msichana aliyeibua simanzi nchini mwaka 2019, Anna Zambi baada ya kupoteza familia yake katika ajali ya gari iliyohusisha wazazi wake na wadogo zake watatu.


Moshi. Mungu hamtupi mja wake. Ndivyo unavyoweza kusema katika maisha ya msichana aliyeibua simanzi nchini mwaka 2019, Anna Zambi baada ya kupoteza familia yake katika ajali ya gari iliyohusisha wazazi wake na wadogo zake watatu.

Ajali hiyo ilitokea wakati Anna akiwa kidato cha nne, lakini sasa amemaliza kidato cha sita na kufaulu vizuri mitihani.

Anna alijiunga na kidato cha tano katika Shule ya Cannosa iliyopo jijini Dar es Salaam na katika matokeo yaliyotangazwa wiki iliyopita, amefaulu kwa kupata daraja la kwanza katika masomo ya HKL (Historia, Kiswahili na Kiingereza).

Sasa msichana huyu ana nafasi ya kuendelea na masomo ya elimu ya juu katika fani aitakayo kutokana na kuwa na ufaulu mzuri.

Walezi na walimu wa Anna wamemwelezea kama msichana mwenye bidii katika masomo na wanaamini atatimiza ndoto yake ya kuwa mwanasheria.


Ajali iliyombadilisha

Oktoba 25, 2019 familia ya Anna ilisafiri kutoka Dar es Salaam kwenda kusherehekea mahafali ya binti yao yaliyokuwa yakifanyika Oktoba 26 katika Shule ya Sekondari ya wasichana Mtakatifu Teresa wa Calcuta iliyopo Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro.

Familia hiyo ikiwa katika gari binafsi ilipata ajali wakati wakivuka daraja moja mkoani Tanga baada ya gari lao kusombwa na maji kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha siku hiyo. Ajali hiyo ilibadilisha maisha ya Anna na kumfanya kuwa yatima akipoteza wadogo zake watatu waliokuwa wakienda kwenye mahafali hayo pamoja na wazazi wao.

Baada ya ajali hiyo, uongozi wa shule ulitumia busara kutomjulisha mwanafunzi Anna kuhusu tukio hilo, ili lisimchanganye na kushindwa kufanya mitihani yake ya kidato cha nne iliyokuwa mbele yake.

Baada ya kumaliza mitihani, alichukuliwa na baadhi ya ndugu kutoka shuleni hadi nyumbani kwao na kujulishwa tukio hilo.

Anna alipoteza fahamu siku nzima baada ya kushuhudia makaburi matano nyumbani kwao yakiwa na majina ya wazazi wake wawili na wadogo zake watatu.

Kutokana na mazingira magumu ya kisaikolojia yaliyomkumba, ndugu na viongozi wa dini walimtafutia mtaalamu mshauri nasaha amsaidie kuelewa na kuzoea hali halisi iliyojitokeza. Katika matokeo yake ya kidato cha nne, alifaulu na kupata daraja la pili na kwenda kidato cha tano na kumaliza kidato cha sita mwaka huu.

Katika matokeo ya mtihani wa kidato cha sita mwaka 2022, Anna ni miongoni mwa wanafunzi wa kike waliofaulu kwa kupata alama ya daraja la I.8 katika shule ya sekondari Canossa ya jijini Dar es Salaam katika masomo ya HKL.

Akizungumzia maisha ya Anna shuleni hapo, makamu mkuu wa shule hiyo, Sista Angela alisema ni mwanafunzi aliyejituma na kusoma kwa bidii, licha ya changamoto alizopitia za kuondokewa na ndugu zake.

“Alionyesha bidii na nidhamu ya hali ya juu, ndio maana hata katika matokeo yake tumeona amefanya vizuri sana,” alisema Sista Angela.

Pamoja na mambo mengine, mkuu huyo wa shule alisema walikaa na Anna kama mtoto wao na alikuwa akiwasikiliza na kuwapenda kama wazazi wake. Mama mlezi wa msichana huyo, Isabela Liymo alisema Anna amekuwa ni mwanamke wa pekee na shupavu ambaye amepambana na kusahau changamoto aliyopitia ya kuondokewa na wazazi wake. “Hatuwezi kusema chochote kuhusu ufaulu wa Anna zaidi ya kusema tunamshukuru Mungu kwa yote maana alipita katika mapito magumu, lakini Mungu amemvusha kwa neema zake.

“Hata alipokuwa kidato cha tano, alipitia changamoto za ugonjwa, hali iliyosababisha kufanyiwa upasuaji wa goti, lakini alipona,” alisema.

Kwa upande wake, mkuu wa shule ya wasichana ya Mtakatifu Teresa wa Calcuta, Sista Lucy Nduku alisema changamoto alizopitia Anna, haikuwa rahisi, lakini walitumia kila aina ya njia kuhakikisha anasahau mapito hayo japo ni jambo gumu.

“Haikuwa rahisi, unajua kupotelewa na wazazi wote tena kipindi anakaribia mitihani ni jambo zito. Wakati tatizo hili linampata, kama shule ilibidi tufiche siri hadi amalize mitihani yake. Tulitumia jitihada zote kumfariji, alifarijika kwa kuwa malezi aliyopata hapa shuleni yalikuwa ni mazuri na yamemsaidia na ndio maana amefaulu vizuri,” alisema na kuongeza:

“Hata baada ya kumaliza hapa, tulikuwa tukiongea na walezi wake kutokana na mazingira yaliyomtokea hadi akafikia kukubali hali hiyo na ndio maana akaendelea kusoma kwa bidii.” Kwa upande wake, Padri Christopher Mboya aliyekuwa mkuu wa shule hiyo alisema wanaamini ndoto yake ya kuwa mwanasheria itatimia.

“Kufaulu kwake kwetu sisi ni faraja kubwa kwa maana tulimlea vizuri hapa shuleni kwa malezi bora na ndiyo maana ameendelea kufanya vizuri katika matokeo yake ya kidato cha sita,” alisema Padri Mboya.


Rita inavyomsimamia

Kaimu Mkurugenzi wa Ulinzi wa Haki za Kisheria wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita), Reginald Makoko alizungumzia jinsi walivyoingia kati kusimamia mali zilizoachwa na wazazi wa Anna.

Alisema Rita ina majukumu mengi miongoni ni kuwa mdhamini wa umma pamoja na kusimamia mali zisizo na mwenyewe kwa mfano mtu amefariki ameacha nyumba au mali na watu wakavamia au kuanza kuvutana, “tukibaini, tunaingia kwa mujubu wa sheria.”

“Tuna jukumu la kusimamia watoto wenye umri chini ya miaka 18, kusimamia mali zao pale inapoonekana hawana wazazi au walezi wa kufanya hivyo au kwa namna moja au nyingine kuna hali ya kupoteza mali au kutumika vibaya tunakwenda mahakamani,” alisema.

Makoko alisema baada ya kuona hali hiyo, walikwenda Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kufungua kesi ya kuomba kuwa wasimamizi wa mirathi kwa mujibu wa sheria na mahakama ikawakubaliana baada ya kuwasikiliza.

“Mahakama Kuu ya Dar es Salaam baada ya kutusikiliza ikakubali sisi kuwa wasimamizi hadi miaka ya utu uzima ambao Anna alifikisha mwaka jana akiwa shule, tuliwasiliana na yeye pamoja na mama mdogo na kukubaliana tuache asome kwanza,” alisema.

Alisema nyumba iliyoko Goba, Dar es Salaam ambayo kwa sasa ina wapangaji wawili, fedha wanaziingia kwenye akaunti maalumu ya Rita ambayo msimamizi wake ni Ofisa Mtendaji Mkuu.

Aidha, Makoko alisema kulikuwa na akaunti iliyofunguliwa Benki ya CRDB ya rambirambi na walipeleka taarifa kusitoke fedha yoyote, na kueleza kwamba hakuna fedha iliyotoka tangu ilipofunguliwa.

“Kwa sasa Anna hana matumizi makubwa, alipata ufadhili wa kusoma Canossa, hivyo hela zilizopo CRDB bado hatujazichukua, hizi za kodi zinatosha kabisa na akihitaji huwa anatuandikia barua,” alisema na kuongeza:

“Tumekuwa karibu na Anna, tulikwenda kule shuleni kwake alikomaliza kidato cha nne, tumekwenda Canossa na kuzungumza naye, yeye mwenyewe amekuja ofisini kwetu na hata katika mahafari yake ya kidato cha sita tulikwenda.”