Gari la Kipanya lawaibua wadau

Muktasari:

  •  Uzinduzi wa gari inayotumia umeme uliofanywa na Ali Masoud ‘Masoud Kipanya’ ikiwa na muonekano wa katuni ya KP, umeibuka wadau ambao wamesema hatua hiyo itaongeza ajira nchini na kuiomba Serikali kuendeleza wabunifu.


Dar es Salaam. Uzinduzi wa gari inayotumia umeme uliofanywa na Ali Masoud ‘Masoud Kipanya’ ikiwa na muonekano wa katuni ya KP, umeibuka wadau ambao wamesema hatua hiyo itaongeza ajira nchini na kuiomba Serikali kuendeleza wabunifu.

Uzinduzi wa gari hilo ulifanyika juzi na Kipanya alieleza kila kitu wametengeneza mwenyewe isipokuwa baadhi ya vitu vimeagizwa kutoka nje ya nchi.

Imeelezwa gari hiyo inayotumia mota ikichajiwa na kujaa ipasavyo ina uwezo wa kutembea kilomita 60 na mzigo wakati bila mzigo ni kilomita 80 huku ukiwa umewasha redio.

Mtaalamu wa uchumi, Dk Abel Kinyondo alisema ubunifu aliokuja nao Kipanya kama utaenda mbali utatengeneza ajira nyingi huku akiwaomba wadau ikiwemo Serikali kuwakumbatia watu wa aina hiyo.

“Watu wa aina hii wakumbatiwe ili watengeneza na vitu vingine. Tunajua Kipanya si mhandisi , ila mtundu na mbunifu. Mtu wa aina hii sehemu nyingine anatengenezewa mazingira ya kufanya zaidi na zaidi,”alisema.

Alisema ili afike mbali inatokana na mchango wa wadau, lakini kwa Serikali ni mwanzo wa kukumbatia mawazo yake ikiwemo kumpunguzia kodi inapobidi na kumuondolea tozo, ili maisha ya ufanyaji kazi kwake yawe ya gharama nafuu.

“Kwa sekta binafsi wanatakiwa kuanza kudhamini mradi wake kwa sababu unapounga mkono inasaidia Watanzania wengi, wamuwezeshe kiteknolojia na kumsaidia kurudisha gharama alizotumia na apate nguvu ya kufanya kingine,” alisema.

Alisema kwa nchi nyingine badala ya kumuacha kufanya maonyesho kwa gharama zake, wadau wanafanya kila kitu ili kuendeleza ubinunifu huo.

Mkurugenzi mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Dk Amos Nungu alisema kwa ubunifu aliokuja nao Kipanya si kitu kipya kwa sababu hata kwenye mitandao upo isipokuwa wanapongeza kufanikiwa kujitangaza sokoni.

“Mwaka juzi kuna mbunifu kutoka NIT (Chuo cha Usafirishaji)alikuja na gari ya aina hiyo tulimtambua na kumpatia fedha kidogo kwa ajili ya kuendeleza ubunifu wake,” alisema.

Alisema wanampongeza Kipanya kwa kitendo cha kujitangaza na wameshaandika kwenye kanzidata kwamba wanautambua ubunifu huo na kuwahamasisha wengine kupitia kwake kwenda mbele zaidi.

Alisema changamoto iliyopo wabunifu wengi wanafanya vema, lakini wanaishia kwenye maonyesho, hawaendi mbele na kumuomba ashirikiane na wafanyabiashara kuingiza sokoni ubinifu huo.

Kauli ya TBS

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Dk Yusuph Ngenya alisema bado gari hiyo haijapita kwenye taasisi hiyo na kumshauri Kipanya kuipeleka kufanyiwa vipimo.
“Ubunifu mzuri tunaihamasisha, lakini hatutaki kuisemea kabla haijaja kwetu. Namshauri ailete ili apate nguvu zaidi baada ya kupita kwenye vipimo vyote na kuondoa hofu kwa wateja wanaohitaji kununua,” alisema Ngeya.

Kipanya aelezea gari

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa gari hiyo, Kipanya alisema kila kitu wametengeneza wenyewe ikiwemo kuchonga mabati na kuyapinda dashibodi na plastiki.

“Kama ilivyo viwanda vingine vya magari tairi, vioo, betri na mota tumenunua kutoka sehemu nyingine,” alisema.

Alisema wapo kwenye mchakato wa kujisajili Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kama wawekezaji wa ndani huku akieleza tayari wametengeneza gari nyingine mbili za aina tofauti ambazo zitakuwa kubwa kuliko iliyozinduliwa.

Mkurugenzi wa uzalishaji wa Kampuni ya Kaypee Motor, Rajab Mssumi alisema wazo la kutengeneza gari hiyo lilianza miaka 11 iliyopita, japokuwa walianza kufikiria kutengeneza bajaji, boti baadaye wakarudi kwenye gari.

Miaka miwili iliyopita walikwenda Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido) kukodi eneo kwa ajili ya yadi na walianza kuunda gari hiyo iliyozinduliwa juzi.

Alisema walipitia wakati mgumu hadi kukamilisha gari hiyo, kwani wametumia miaka miwili tangu kuanza kutengenezwa kwake.

Alisema gari hiyo inatumia mota cc 900 ambayo walinunua kutoka China na kwamba mifumo ya breki ni ya kawaida.

Alisema gari hiyo inatumia betri tano huku akibainisha kwamba bado wapo kwenye majadiliano bei ya kuuza gari hiyo na kwamba haitazidi Sh10 milioni kwa sababu ndiyo kwanza wameanza.

“Gari inachajiwa kawaida kama simu na ina uwezo wa kubeba nusu tani kwa maana ya kilo 500 ya mzigo mithiri ya gari aina ya kirikuu na mfumo wa gari hiyo ni automatic.

“Ubora wa gari ni tofauti na mengine kwani mabati tuliyotumia kuunda na kutengeneza ni magumu ikilinganishwa na gari zinazoundwa nje ya nchi,” alisema.

Alisema mahitaji ni makubwa na wanatarajia kutengeneza gari nyingi zaidi, kwani tangu wazindue wamepokea oda nyingi hasa kutoka Zanzibar na Commoro.

Hata hivyo, alisema wanatarajia kupata fungu la fedha kutoka kwa wadau, hivyo wakifanikiwa watakuwa na uwezo wa kutengeza gari nyingi zaidi.Pia alisema hadi sasa hawajajua gari hiyo ina uzito kiasi gani isipokuwa TBS imechukua vipimo na wanatarajia kuwaletea majibu kuanzia wiki hii.