Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Gharama ya ‘wiring’, uharibifu miundombinu vikwazo uunganishaji umeme vijijini

Muktasari:

  • Hadi mwaka 2030, Serikali imedhamiria kuhakikisha inaongeza kiwango cha upatikanaji wa umeme vijijini kutoka asilimia 78.1 hadi asilimia 100 na kuongeza kiwango cha uunganishaji wa wananchi kutoka asilimia 37.2 hadi asilimia 75 katika kipindi cha utekelezaji wa miradi hiyo ifikapo mwaka 2030.

Dar es Salaam. Gharama kubwa ya uwekaji wa mfumo wa umeme majumbani (wiring) na uharibifu wa miundombinu ya umeme zimetajwa kuwa changamoto kuu zinazokwamisha kasi ya uunganishaji wa umeme vijijini nchini.

Changamoto hizi zinabainika wakati ambao Serikali imefanikiwa kufikisha umeme katika vijiji vyote nchini na sasa nguvu ikielekezwa katika vitongoji.

Akizungumza kuhusu hali ya utekelezaji wa miradi ya umeme, Mhandisi Msimamizi wa Miradi Kanda ya Kati kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (Rea), Aneth Malingumu, amesema Tanzania imepiga hatua katika kufikisha miundombinu ya umeme vijijini, lakini changamoto imebaki kwenye hatua ya uunganishaji kwa wananchi.

Amesema hadi sasa, zaidi ya asilimia 85 ya upatikanaji wa umeme imefikiwa nchini, huku maeneo ya vijijini yakifikia takribani asilimia 78.1, hali inayoonesha kuwa huduma ya umeme sasa imefika karibu na wananchi wengi.

Hata hivyo, kiwango cha uunganishaji wa moja kwa moja kwa wananchi katika maeneo ya vijijini bado ni asilimia 37.2.

Amesema hali hiyo inasababishwa na uwezo mdogo wa wananchi kugharamia miundombinu ya ndani ya nyumba, ambayo mara nyingi hugharimu kati ya Sh200,000 hadi Sh300,000, huku gharama ya kuunganisha umeme ikiwa chini zaidi.

“Changamoto kubwa ni kwamba si wote wanaofikiwa na umeme wanaounganishwa. Gharama ya wiring ndani ya nyumba ni kubwa kwa wananchi wengi wa vijijini ukilinganisha na uwezo wao,” amesema.

Changamoto nyingine ni matumizi ya umeme kwa kiwango kidogo, ambapo baadhi ya wananchi hutumia zaidi kwa ajili ya mwanga pekee badala ya shughuli za uzalishaji na biashara, jambo linalopunguza athari chanya za kiuchumi za uwepo wa umeme.

Katika utekelezaji wa miradi, Malingumu amesema pia wanakumbana na changamoto ya maeneo ya mbali na yasiyofikika kwa urahisi, ambayo husababisha ucheleweshaji wa utekelezaji pamoja na matukio ya uharibifu wa miundombinu.

Amesema uharibifu huo hutokea zaidi wakati wa msimu wa kilimo, ambapo moto unaotumika kuandaa mashamba huunguza nguzo za umeme pamoja na kutokea kwa wizi wa vifaa vya miundombinu.

“Hizi changamoto za uharibifu na wizi wa vifaa zinatugharimu sana kwa sababu tunalazimika kuanza upya katika maeneo yaliyoathirika,” amesema.

Licha ya changamoto hizo, amesema Serikali na wadau wa sekta ya umeme wameweka malengo ya kuhakikisha vitongoji vyote vinafikiwa ifikapo mwaka 2030, ambapo tayari zaidi ya vitongoji 10,000 vipo katika hatua ya utekelezaji huku vingine 13,000 vikiwa katika hatua ya kutafutiwa fedha.

Ameongeza kuwa lengo ni kuongeza kiwango cha upatikanaji wa umeme vijijini kutoka asilimia 78.1 hadi asilimia 100 na kuongeza kiwango cha uunganishaji wa wananchi kutoka asilimia 37.2 hadi asilimia 75 katika kipindi cha utekelezaji wa miradi hiyo ifikapo mwaka 2030.

Akizungumzia suala hilo, Malcelina Mashaka ametaka gharama za uunganishaji wa umeme ziwekwe bayana, na pale mtu anapopaswa kununua nguzo, bei elekezi iwekwe wazi ili kupunguza urasimu.

“Kilio kikubwa kipo kwenye nguzo. Kama mtu anapaswa kuchangia, bei iwekwe wazi. Vinginevyo, watu watakuwa na nia, lakini wanashindwa kuunganishwa kwa sababu wanatajiwa bei kubwa ambayo wakati mwingine si halisi,” amesema.