Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Haki za mmiliki wa ardhi kisheria

Muktasari:

Haki hizo ni kama haki ya kumiliki eneo lake. Mmiliki ana haki ya kumiliki na kutambulika kwa kupewa hati ya umiliki ikiwa ya kimila au ya kawaida.

Watu wengi humiliki ardhi kwa njia zozote zinazotambulika kisheria kama kukaa muda mrefu, kwa kurithi au kupewa.

Tutajikita japo kwa ufupi kuangalia haki za msingi ambazo mmiliki wa ardhi anazo kisheria.

Haki hizo ni kama haki ya kumiliki eneo lake. Mmiliki ana haki ya kumiliki na kutambulika kwa kupewa hati ya umiliki ikiwa ya kimila au ya kawaida.

Kwa mujibu wa kifungu cha 25 cha Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999, mtu anaweza kuomba kwa msajili wa ardhi kupewa hati hiyo, lakini kwa maeneo ya vijijini mtu anakuwa na haki ya kupata hati ya umiliki wa ardhi ya kimila.

Hiyo haki inamfanya kuwa mmiliki pekee tofauti na watu wengine wote duniani. Pia, msajili wa ardhi au mtu yeyote katika mamlaka hawezi kumkatalia mtu kutambulika kwa kumnyima hati bila sababu zinazotambulika kisheria.

Haki ya kuuza eneo lake, mtu yeyote anayemiliki eneo atakuwa na haki ya kuuza eneo lake wakati wowote na kwa mtu yoyote, isipokuwa kwa wageni labda iwe kwa ajili ya uwekezaji. Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 20 cha Sheria ya Ardhi Sura ya 113 ya Mwaka 1999.

Kwa hiyo mtu anakuwa na uwezo wa kuuza kama yeye ni mmiliki na mauzo yake ni halali na yanatambulika kisheria. Kama ni mali ya marehemu, basi iuzwe na msimamizi wa mirathi, siyo mtu yeyote yule.

Haki ya kupangisha eneo lake, sheria inaruhusu mtu anayemiliki eneo kihalali atakuwa na haki ya kulipangisha kwa mujibu wa sheria.

Haki hii inatambulika na kifungu cha 77 na vifungu vingine vya Sheria ya Ardhi, sura ya 113. Mtu anaweza kupangisha na kuweka kodi ambayo anaona inafaa. Hakuna sheria inayotoa mwongozo wa kiasi cha ulipaji kodi. Hii haki ya kupangisha ipo katika, mashamba, viwanja na nyumba.

Kuhusu haki ya kuchukulia mkopo, benki na taasisi zingine za kifedha zinapenda kutumia ardhi kama dhamana ya mkopo wa aina yoyote kwa sababu kila siku thamani inapanda na ardhi ni mali ambayo haihamishiki.

Mtu anayemiliki ardhi ana haki ya kuomba mkopo na kuweka ardhi dhamana kwa mujibu wa kifungu cha 111 cha Sheria ya Ardhi ya Mwaka 1999.

Kwa mujibu wa sheria ya ardhi itakuwa dhamana tu. Kwa hiyo mtu hapaswi kutumia dhamana hiyo kujimilikisha eneo na kama mtu ameshindwa kulipa mkopo huo, basi taratibu zinapaswa kufuatwa ili kuweza kukodisha hilo eneo au kuliuza ili kulipia fidia.

Kila mtu ana haki ya kutoingiliwa au kuvamiwa na mtu kwenye eneo lake. Kila mtu ana haki ya kikatiba ya kumiliki eneo lake. Ni kosa la jinai kuvamia eneo la mtu kwa mujibu wa kifungu cha 299 cha Sheria ya makosa ya Jinai Sura ya 16. Pia ni kosa la madai kuingia kwenye eneo la mtu na kufanya ujenzi au kufanya lolote.

Kimsingi kila mmiliki wa ardhi ana haki ya kumiliki eneo lake bila kuingiliwa na mtu yeyote na endapo ataingiliwa au kufanyiwa uvamizi atakuwa na uwezo wa kushtaki.

Makala ijayo tutazidi kufafanua haki za mmiliki wa ardhi kisheria, usikose.

Mwandishi wa makala hii ni Wakili wa Kujitegemea kutoka Kampuni ya uwakili ya Law Guards Advocates, Dar es Salaam.