Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hakuna mamlaka iliyo juu ya sheria - Jaji Masaju

Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, George Masaju akitoa hotuba yake ya akifungua Mkutano Mkuu wa Chama cha Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mahakama Tanzania

Muktasari:

  • Jaji Masaju ametoa kauli hiyo jana Jumanne, Juni 30, 2026 jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mahakama Tanzania

Dodoma. Jaji Mkuu wa Tanzania, George Masaju amewataka madalali na wasambaza nyaraka wa Mahakama kuacha kuwaogopa viongozi wa kisiasa na Serikali wanaoingilia utekelezaji wa amri za Mahakama, akisisitiza hakuna mamlaka yoyote iliyo juu ya uamuzi wa Mahakama.

Jaji Masaju ametoa kauli hiyo jana Jumanne, Juni 30, 2026 jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mahakama Tanzania.

Jaji Masaju amesema baadhi ya viongozi wamekuwa wakitumia nafasi zao kama wenyeviti wa Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya kuzuia utekelezaji wa amri halali za Mahakama kitendo kinachodhoofisha utawala wa sheria.

"Hizo sheria zinazowapa madaraka hazikuwapa mamlaka ya kuingilia utekelezaji wa amri na uamuzi wa Mahakama, wachukulieni hatua.

“Haiwezekani Mahakama imeshatoa amri halafu mtu mwingine anazuia, ni lazima tutofautishe shughuli za kisiasa na shughuli za utoaji haki zinazofanywa na Mahakama," amesema Masaju.

Kauli hiyo imekuja wakati Mahakama ikiendelea kusisitiza umuhimu wa kulinda uhuru wa mhimili huo katika kipindi ambacho Taifa linaelekea kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayoweka mkazo katika utawala bora na haki.

Jaji Masaju amesema hakuna mtu aliye juu ya sheria, akiwamo yeye, hivyo kila mwenye dhamana anapaswa kutekeleza wajibu wake kwa kuzingatia Katiba na sheria bila hofu, upendeleo wala chuki.

"Hata mimi Jaji Mkuu siko juu ya sheria, tulikula kiapo cha kuisimamia Katiba na sheria za nchi bila hofu, upendeleo wala chuki, hivyo kila mmoja anatakiwa kufanya hivyo," amesema.

Katika hatua nyingine, amewataka madalali na wasambaza nyaraka kutumia njia za kisheria dhidi ya viongozi au askari polisi watakaowazuia kutekeleza amri halali za Mahakama, akisema tayari Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameeleza watumishi wanaokiuka sheria watawajibika binafsi kwa makosa yao.

Baadhi ya Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mahakama Tanzania walioshiriki katika Mkutano Mkuu wakimsikiliza na kufuatilia hotuba ya Jaji Mkuu (hayupo katika) alipokuwa akifungua Mkutano.

Amesema vitendo vya kuzuia utekelezaji wa uamuzi wa Mahakama vinakwenda kinyume na misingi ya utawala bora na vinaweza kudhoofisha imani ya wananchi kwa mfumo wa utoaji haki.

"Ibara ya 26 ya Katiba inaweka wajibu kwa kila mtu kuheshimu sheria. Hakuwezi kuwa na utawala bora kama uamuzi wa Mahakama unaingiliwa na watu wengine bila sababu za msingi," amesema.

Hata hivyo, Jaji Mkuu amesema changamoto hizo haziwezi kuisha kama madalali hawatazingatia maadili ya kazi zao, akibainisha kuwa, baadhi yao wamekuwa wakitoa mwanya wa kuingiliwa kutokana na upungufu katika utekelezaji wa majukumu yao.

Amewataka kufanya kazi kwa uadilifu, uaminifu na weledi, huku akionya wasio na uwezo wa kutekeleza majukumu yao wanaweza kupokonywa leseni.

"Moja ya sharti la kupewa kazi hizi ni kuwa na uwezo wa kuzimudu. Kama hukuzijua taratibu ulipataje leseni? Tutawanyang'anya leseni hizo kama mtashindwa kutekeleza wajibu wenu ipasavyo," amesema.

Jaji Masaju amesema maadili ya madalali na wasambaza nyaraka yameainishwa wazi katika Kanuni za Madalali na Wasambaza Nyaraka za mwaka 2017 zilizorekebishwa mwaka 2019, hivyo hakuna sababu ya kuyakiuka.

Ametaja miongoni mwa maadili hayo kuwa ni uadilifu, uaminifu, usiri katika kushughulikia taarifa za Mahakama na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Amesema dalali wa Mahakama anapaswa kutekeleza majukumu yake bila kutumia vibaya mamlaka aliyopewa na bila kujinufaisha kupitia nafasi yake.

"Tulianza mkutano huu kwa sala. Mungu hadhihakiwi; unachopanda ndicho utakachovuna. Hatuwezi kutumia nafasi hizi kuwaonea wananchi au kujinufaisha kwa njia zisizo halali," amesema.

Aidha, amewataka madalali kuzingatia utu wa watu wanaowahudumia, hasa makundi maalumu kama wazee, wajane, watu wenye ulemavu, wagonjwa na wanawake wajawazito.

Amesema wakati wa kutekeleza amri za Mahakama wanapaswa kuhakikisha hawawaongezei maumivu watu ambao tayari wanakabiliwa na mazingira magumu.

"Hawa wengine ni wajane. Msiende kuwanyang'anya mali zao na kuwaongezea majonzi. Sheria inawataka kuheshimu utu na faragha ya kila mwananchi," amesema.

Masaju amesisitiza madalali ni sehemu muhimu ya mfumo wa utoaji haki kwa kuwa, ndio wanaohakikisha uamuzi wa Mahakama yanatekelezwa.

Amesema bila utekelezaji wa hukumu, kazi ya Mahakama inapoteza maana na hali hiyo inaweza kusababisha wananchi kupoteza imani kwa mfumo wa haki pamoja na kuhatarisha amani.

"Ninyi ni nguzo muhimu ya haki, kama uamuzi wa Mahakama hautekelezwi, Mahakama itadharaulika na hatimaye kutakuwa na uvunjifu wa amani pamoja na kupotea kwa uhuru wa Mahakama," amesema.

Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Amir Mruma amewaasa madalali wa Mahakama na wasambaza nyaraka kufanya kazi zao kwa kuzingatia uadilifu wa hali ya juu na sheria.

"Mkikosa uadilifu katika hilo, mnatengeneza mazingira rahisi kwa watu wa muhimili mingine kuingilia muhimili wa Mahakama na kuhalalisha uingiliaji wao," amesema Jaji Mruma.

Mwenyekiti wa Chama cha Madalali wa Mahakama na Wasambaza Nyaraka za Mahakama Tanzania, Mwamvua Kigulu ameiomba Mahakama kusimamia ipasavyo sheria na taratibu ili kulinda usalama wao, heshima ya amri za Mahakama na kuboresha mfumo wa utoaji haki nchini.