Hali unaweza kuipata baada ya chanjo ya corona

Hali unaweza kuipata baada ya chanjo ya corona

Muktasari:

  • Wataalamu wa afya wameeleza hali ambayo mtu anaweza kuipata baada ya kupata chanjo ya corona, lakini wanashauri asitumie dawa zaidi ya Panadol.

Dar es Salaam. Wataalamu wa afya wamesema mtu aliyepata chanjo ya corona anaweza kuumwa kichwa, kupata homa, kusikia baridi, kutapika na mwili kuuma saa chache baada ya chanjo.

Hali hizo zimejitokeza kwa baadhi ya watu waliopata chanjo ya Janssen au Johnson&Johnson, iliyoanza kutolewa nchini Julai 28,2021 kwa Rais Samia Suluhu Hassan kuizindua rasmi.

Wataalamu hao wamesema hali hiyo ambayo ilitarajiwa kwa watu waliopata chanjo hutokana na seli za kinga za mwili kupokea protini mpya za mdudu wa Covid-19 zilizoletwa kwa njia ya chanjo, ili kutengeneza kinga imara dhidi ya virusi hivyo.


Tangu kuanza kwa utolewa kwa chanjo, watu waliopata wamekuwa wakitoa shuhuda kuhusu wanavyojisikia kupitia mitandao ya kijamii, huku wasiochoma wakitamani kujua zaidi kuhusu hali hiyo.

Wapo waliochoma na hawakusikia chochote na wengine walipata maudhi madogo, ingawa pamoja na dalili hizo wapo ambao hawakutumia dawa na hali zao zilirejea kawaida baada ya muda.

Hellen John, mkazi wa Mbezi Jogoo, Dar es Salaam amesema alichoma sindano saa 6 mchana siku ya Jumatatu Agosti 2, 2021 na baada ya muda alianza kuhisi utofauti mwilini mwake ikiwamo kupata homa kali na baridi.

“Nilipata homa kali na baridi kwa zaidi ya saa 4.Nilijifunika blanketi na nikavaa na soksi, baadaye nilipata hali nyingine ya kusikia joto kali na kutapika,” amesema Hellen.

Mashuhuda wengi waliozungumza na Mwananchi Digital baada ya kuchanja wamesema walisikia homa huku wachache wakisema hawakusikia hali yoyote ya utofauti mwilini mwao.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Limited (MCL), Bakari Machumu amesema siku mbili baada ya kuchanjwa amepokea maswali mengi yanayojenga hofu.

“Ni hofu mtu aliyonayo na ni kama wanataka kupata uhakika, imani kutoka kwa mtu au watu anaowaamini, kuwajua, kuwaheshimu na kujiridhisha kama wamepata madhara yoyote,” amesema Machumu.

Hata hivyo, Machumu amesema shuhuda hizo zinasaidia kuwaelewesha watu na kuwatia imani na moyo. Nimeona watu wakishawishika na kuacha msimamo wao wa siku mbili nyuma.

Wasemavyo madaktari

Daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa hewa, Dk Elisha Osati amesema kitendo cha mtu kusikia homa na maudhi mengine madogo kinatokana na seli za mwili kuanza kupokea kinga dhidi ya mdudu huyo.

“Ukiwekewa protini za kinga dhidi ya Covid-19 mwilini wengine huanza kupata homa na maudhi madogo madogo, hii inatokana na protini kuanza kuwasiliana na seli za kinga ya mwili kwa ajili ya kutengeneza kinga dhidi ya virusi vya corona,” amesema na kuongeza:

“Yaani hapo seli zinapambana na kitu kipya kilichoingia mwilini ambacho ndiyo zile protini (chanjo),” amesema Dk Osati.

Alipoulizwa iwapo kuna matibabu ambayo mtu anaweza kupata akipata homa kali, amesema: “Tunashauri mtu akipatwa na hiyo hali atulie na kuendelea na shughuli zake. Ikizidi ameze panadol ya kawaida na asimeze vidonge vya kutuliza maumivu vya aina nyingine kwa kufanya hivyo ataharibu dozi. Hali ikizidi anatakiwa kuwahi hospitali.”

Hata hivyo mtaalamu wa macrobaiolojia kutoka chuo cha Muhas, Dk Mtebe Majigo amesema mtu anapopewa chanjo yoyote anaweza kupata maudhi madogo kama homa ingawa si wote.

“Wakati mwili unapozalisha vichocheo vyake ambavyo ndiyo itakuwa kinga ya mwili, vichocheo vingine ndiyo vinasababisha homa kutokea. Vinavyotoka ndiyo vinapeleka taarifa kwenye ubongo na vinarudi kama homa. Hii ni baada ya mwili kushtuka kutokana kilichoingia, lakini inatofautiana kati ya mtu na mtu,” amesema Dk Majigo.