Halmashauri Dodoma yakaribisha wawekezaji ujenzi wa mji mpya Hombolo

Muktasari:
- Halmashauri ya Jiji la Dodoma imepanga kujenga mji wa kisasa ambao utabeba utamaduni wa Mtanzania na wa nchi za Magharibi pamoja na makazi ya mabalozi wanaowakilisha nchi zao kwa lengo la kuvutia watalii na wawekezaji.
Dodoma. Halmashauri ya Jiji la Dodoma imepanga kujenga mji wa kisasa kuzunguka bwawa lililopo kata ya Hombolo ambalo litabeba utamaduni wa Mtanzania, utamaduni wa nchi za Magharibi, makazi ya mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini pamoja na maeneo ya uwekezaji.
Mji huo utapakana na Mji wa Kiserikali wa Magufuli uliopo Mtumba, Ikulu ya Chamwino, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato na barabara ya mzunguko hivyo kurahisisha upatikanaji wa huduma zote muhimu kwa wakazi wa Jiji hilo.
Akizungumza na Mwananchi Digitali wakati wa kutambulisha ujenzi wa Jiji hilo kwa mabalozi wa nchi za Norway, Sweden, Finland na Denmark zinaounda umoja wa nchi za (Nordic), Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dk Frederick Sagamiko amesema litakuwa kitovu cha uchumi wa jiji la Dodoma.
Amesema maandalizi ya ujenzi huo yameshaanza ikiwemo upembuzi yakinifu ili kujua wananchi watakaolipwa fidia ili kupisha ujenzi wa mji huo pamoja na wawekezaji ambao watakuwa tayari kushirikiana na Jiji kuujenga mji huo wa kisasa.
“Kuna mabalozi wengi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini, mji huo utakuwa na makazi ya kutosha kwa ajili yao, hoteli za kitalii, shule zinazofundisha michepuo ya kimataifa na maeneo ya fukwe kwa sababu mji huo utajengwa kando ya bwawa letu lililopo pale Hombolo,” amesema Dk Sagamiko.
Dk Sagamiko amewakaribisha wawekezaji kutoka nchi za Nordic kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika ujenzi wa mji huo wa kitalii kwani fursa za uwekezaji ni nyingi.
Amesema mji huo utajengwa kwa kuzingatia utunzaji wa mazingira kwa kutumia nishati safi ya kupikia na pia kufikisha huduma za kijamii kwa watu walioko pembezoni mwa jiji la Dodoma.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema mkoa wa Dodoma una maeneo mengi ya uwekezaji ikiwemo kwenye sekta ya kilimo, nishati safi ya kupikia, utalii na viwanda na hivyo kuwakaribisha mabalozi hao kuja kuwekeza Dodoma.
Naye Balozi wa Norway, Tone Tinnes amesema nchi zinazounda umoja wa Nordic zimekuwa zikishirikiana na Tanzania kwenye sekta ya nishati kwa muda mrefu, hivyo watawashirikisha wawekezaji kutoka kwenye nchi zao kushiriki ujenzi wa mji huo wa kimkakati.
Amesema mabalozi wanaowakilisha nchi zao nchini pia hawana makazi kutokana na Jiji la Dodoma kujaa, hivyo kukamilika kwa ujenzi wa Mji wa kisasa wa Hombolo utawavutia mabalozi wengi kuhamia Dodoma pamoja na familia zao.