Hanang' wampongeza Giniki kwa kushinda Poland
Mkuu wa Wilaya ya Hanang' Mkoani Manyara, Janeth Mayanja (kushoto) akimkabidhi zawadi mwanariadha Emmanuel Giniki aliyeshinda mashindano ya half marathon nchini Poland hivi karibuni, katikati ni Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Paul Bura. Picha na Joseph Lyimo
Muktasari:
Serikali wilayani Hanang’ pamoja na wadau mbalimbali wamempongeza mwanariadha Emmanuel Giniki, kwa kufanya vizuri katika mbio za kimataifa.
Hanang'. Serikali wilayani Hanang' Mkoani Manyara, imempongeza mwanariadha, Emmanuel Giniki kwa kushika nafasi ya kwanza katika mashindano ya kimataifa ya riadha Nusu Marathon yaliyofanyika nchini Poland.
Mkuu wa Wilaya ya Hanang' Janeth Mayanja akizungumza wakati wa pongezi hizo amesema japokuwa Giniki anawaikilisha nchi ila anaitangaza vyema pia wilaya hiyo.
Mayanja amesema alikuwa anamuona Giniki kwenye matukio mbalimbali wilayani Hanang' ikiwemo maadhimisho ya miaka 45 ya uhuru.
"Siku unashinda mashindano ya kimataifa ya riadha ya half marathon Machi 27 nchini Poland nilikuona kwenye mitandao nikakukumbuka," amesema Mayanja.
Amesema wananchi wa Hanang' wanapaswa kujivunia watu wanaowakilisha nchi hivyo wawapongeze wanaporudi nyumbani na siyo kupokelewa kimya kimya.
"Tunafahamu unawakilisha Tanzania nje ya nchi, pia sisi wana Hanang' wenzako tunapaswa kukuunga mkono na kukupongeza kwani unatuwakilisha vyema," amesema Mayanja.
Mwanariadha Emmanuel Giniki amesema japokuwa yeye ni mzaliwa wa wilaya ya Hanang' hiyo ni mara yake ya kwanza kupokewa na viongozi wa serikali ya wilaya hiyo.
"Tangu nianze riadha mwaka 2015 sijawahi kupokelewa kama hivi na viongozi wa Hanang' zaidi ya viongozi wangu wa riadha na ndugu, jamaa na marafiki," amesema Giniki.