Hatimaye mwanafunzi Godwin azikwa, mamia wamwombeleza
Wazazi wa Godwin Masaki wakiweka mashada katika kaburi la mtoto wao ambapo mazishi yalifanyika nyumbani kwao Rau Mrukuti katika Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
Muktasari:
- Godwin na Edson Mosha mbao wote walikuwa wanafunzi wa kidato cha nne katika shule hiyo, walifariki dunia Mei 12 mwaka huu kwa kukosa hewa, wakati walipoingia ndani ya tenki la kuhifadhia maharage kwa ajili ya kutoa maharage, baada ya sehemu ya chini ya tenki hilo kuziba.
Moshi. Mamia ya waombolezaji wamejitokeza kwenye maziko ya Godwin Msack (17) ambaye alikuwa mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Kisomachi, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Godwin na Edson Mosha mbao wote walikuwa wanafunzi wa kidato cha nne katika shule hiyo, walifariki dunia Mei 12 mwaka huu kwa kukosa hewa, wakati walipoingia ndani ya tenki la kuhifadhia maharage kwa ajili ya kutoa maharage, baada ya sehemu ya chini ya tenki hilo kuziba.
Akizungumza leo Mei 18, 2023 katika ibada ya maziko, Mwakilishi wa Askofu Jimbo Katoliki la Moshi, Ludovic Minde, Pandri Patrick Soka amesema kijana huyo amefikwa na umauti wakati akijaribu kumuokoa mwanafunzi mwenzake ambaye aliingia kwenye tenki la kuhifadhia maharage.
Katika ibada hiyo ya maziko iliyofanyika Kigango cha Mtakatifu Thomas Aqno Rau, Parokia ya Maonano Mawela, ambapo Padri Soka amesema kifo hicho kichukuliwe kama fundisho kwa watu wote, katika kujiandaa na kutenda mambo yaliyo mema.
Akitoa salamu za jeshi la Polisi, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Moshi, SSP Azizi Kalokola amesema jeshi hilo litatenda haki na kuiomba familia kuwa na subira.
Aidha msemaji wa familia, Firimini Msack ameiomba jamii ya Tanzania kuwasamehe kwa kitendo kilichotokea mara baada ya kupata taarifa la tukio hilo. Godwin amezikwa leo nyumbani kwao, katika Kata ya Rau, Manispaa ya Moshi.