Hatua kwa hatua mjane wa Bilionea Msuya alivyoachiwa huru

Mjane wa Bilionea Msuya, Miriam Mrita akiwa kwenye chumba cha Mahakama Kuu ya Tanzania leo Ijumaa, Februari 23, 2024.

Muktasari:

  • Washtakiwa Miriam Mrita na na Revocatus Muyella wanakabiliwa na shtaka moja la mauaji ya kukusudia la mauaji ya Aneth Msuya (wifi wa Miriam) aliyekuwa mdogo wa Bilionea Msuya

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imewaachia huru, mjane wa aliyekuwa mfanyabiashara wa madini wa Tanzanite, Erasto Msuya maarufu Bilionea Msuya, Miriam Mrita na Revocatus Muyella, baada ya upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha mashitaka dhidi yao.

Hukumu hiyo inasomwa leo Ijumaa Februari 23, 2024 na Jaji Edwin Kakolaki aliyeisikiliza.


Hali ilivyokuwa wakati Jaji akisoma hukumu

Washtakiwa hao, Miriam na Muyella wanakabiliwa na shtaka moja la mauaji ya kukusudia la kumuua Aneth Elisaria Msuya (wifi wa Miriam) aliyekuwa mdogo wa Bilionea Msuya.

Aneth aliuawa kwa kuchinjwa na kitu chenye ncha kali nyumbani kwake Kibada Kigamboni, Dar es Salaam Mei 25, 2016.

Katika hukumu hiyo Jaji Kakolaki ameanza kwa kurejea shtaka linalowakabili kisha ushahidi wa upande wa mashtaka akifanya muhtasari wa ushahidi wa kila shahidi.

Kisha atarejea utetezi wa washtakiwa kabla ya kuchanganua namna gani upande wa mashtaka umeweza au umeshindwa kuthibitisha shtaka bila kuacha shaka kwa washtakiwa wote.


Sintofahamu hoja ya kisu kilichotumika kumuua Aneth

Kuhusu hoja ya Wakili Kibatala kuwa hakukuwa na ushahidi kuwa damu iliyokuwepo kwenye kisu ni ya marehemu kwa kuwa, hapakuwa na hata mlinganisho wa kundi la damu ili kubaini kundi la damu ya marehemu, hakuna ubishi kuwa kulikuwa na vinasaba vya mshtakiwa wa pili katika kile kisu.

Kulingana na taarifa ya uchunguzi wa vinasaba na vilivyopatikana kwenye kile kisu (sehemu ya makali) kuwa vilikuwa na jinsia ya kike na vinasaba katika kisu hicho hicho (sehemu ya mpini) vilioana mshtakiwa wa pili kupitia mpanguso wake.

Hakuna namna ambayo vinasaba hivyo vya mshtakiwa wa pili vingeweza kuoana na vya jinsia ya kike kwenye kile kisu bila mguso wa mshtakiwa wa pili na kisu hicho.

Hii ina maana kuwa mshtakiwa wa pili alikuwepo eneo la tukio au alisababisha vitu hivyo kuwepo eneo la tukio.

Lakini, pia kuna filimbi ambayo vinasaba vilivyokuwepo vilioana na vinasaba kutoka katika mpanguso wa mate ya mshtakiwa wa pili.

Hii ina maana kuwa mshtakiwa wa pili alikuwa eneo la tukio Mei 25, 2016 au alisababisha vielelezo vile kufika eneo la tukio (kisu na filimbi) japo kunakosekana muunganiko kuwa kisu kile kilichotumika kuondoa uhai wa marehemu.

Katika shauri hili baada ya kuzingatia mwongozo wa mahakama na kuwepo kwa vinasaba vya mshtakiwa kwenye kisu na filimbi, ushahidi huo unaondoa uwezekano wa kuwa mshtakiwa wa pili hakuwepo eneo la tukio wakati marehemu anauawa.

Hata hivyo, akubaliana na hoja ya Wakili Kibatala kuwa hakuna sampuli ya damu ya marehemu na ya ndugu yeyote ulivyochukuliwa kuoanisha ili kujiridhisha kama damu hiyo ni ya marehemu.

Shahidi wa 15 kwenye mahojiano ya dodoso alisema kuwa hawezi kuthibitisha kuwa jinsia ile ilikuwa ni mwanamke gani.

Kutokana na ukweli kuwa hapakuwepo na sampuli ya damu ya ndugu yeyote wa marehemu kulinganisha na ile iliyokutwa kwenye kisu, na  kwa kuwa hakuna ushahidi wa upande wa mashtaka kuthibitisha hilo, mahakama inabaki na shaka kwamba kisu kile ndicho kilichotumika kukatisha uhai wa marehemu.

Hakuna ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka kuthibtisha kwa kiwango cha juu kunaifanya mahakama ifikie hitimisho kwamba, kisu hicho sicho kilichotumika kukatisha uhai wa marehemu.

Mjane wa Bilionea Msuya, Miriam Msuya akiwa katika chumba cha Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam wakati kesi ikiendelea leo Februari 23, 2024. Picha na Sunday George

Jaji atupilia mbali hoja kuhusu gwaride la utambuzi

Kuhusu hoja ya gwaride la utambuzi kulingana na ushahidi ambao umeungwa mkono na mshahidi wengine, pia naitupilia mbali kuwa haina mashiko.

Kuhusu hoja ya kuwepo kwa mgongano wa nani aliandaa gwaride la utambuzi, ni kweli shahidi wa 13 alikiri kuwepo kwa mgongano huo kati ya ushahidi wake kizimbani na maelezo yake ya mandishi.

Hata hivyo maelezo hayo hayakuwasilishwa mahakamani ili Mahakama iweze kuona ubishani huo.

 Hivyo Mahakama ilinyimwa nafasi ya kuona ukweli wa ubishani huo.

Hata hivyo ni msimamo kuwa lazima ushahidi wa utambuzi uwe umefanywa kwa mujibu wa sheria.

Ni maoni ya Mahakama hii kuwa kama kulikuwa na maswali aliyepaswa kuyajibu kama aliwasiliana na shahidi mtambuzi wa gwaride ni shahidi wa 10 ambaye ndiye aliyeandaa mashahidi, kama kabla ya gwaride alikuwa na mawasiliano na shahidi mtambuzi na si shahidi wa 13 ambaye yeye aliendesha tu gwaride.

Pia, sioni hoja ya msingi kuhusu shahidi wa 25 kushindwa kutambua alichokwenda kufanyia utambuzi.

Mahakama hii haioni ni kwa jinsi gani shahidi kushindwa kutaja kituo cha polisi alikokwenda kufanyia utambuzi wa washtakiwa kuliwaathiri washtakiwa.

Kuhusu hoja ya shahidi wa 25 kutotoa taarifa polisi, shahidi alitoa ufafanuzi kuwa ni kutokana na hofu aliyokuwa nayo ya kutishiwa.

Ni msimamo wa kisheria kuwa ushahidi wa vielelezo vya gwaride la utambuzi si ushahidi toshelevu maana unapokewa mahakamani tu kuunga mkono ushahidi wa shahidi mtambuzi.

Baada ya kuridhika kuwa ushahidi wa shahidi wa 25 umeungwa mkono Mahakama hii imeridhika kuwa mshtakiwa wa kwanza na wa pili ni watu waliotambuliwa na shahidi wa 25 kuwa ndio waliokuwa wakienda Kigamboni kwa kutumia magari mawili tofuati na kwamba ndio waliompa vitisho na kumtaka aondoke nyumbani siku ya tarehe 25, 5, 2016.

Uchambuzi wa ushahidi, hoja hukumu ya mjane wa Bilionea Msuya

Lakini kwanza kuna hoja iliyoletwa na mshtakiwa wa pili ambayo Mahakama inapaswa kuishughulikia kwanza.

Hoja hiyo ni uhalali wa hati ya mashitaka ndio msingi wa kesi kama hati si halali kesi hiyo inakuwa imekufa.

Wakili Nehemia Nkoko wa mshtakiwa wa pili, Revocatus Muyella anasema, tarehe ya tukio kwenye hati ya mashtaka na maelezo ya mashahidi vinapishana.

Pia, alisema hata eneo, lililotokea tukio ni tofauti kati ya linalotajwa kwenye hati na maelezo ya mashahidi.

Alisema kwa kuwa upande wa mashitaka ulishindwa kufanya marekebisho ya kasoro hizo basi washtakiwa waliathiriwa.

Katika sehemu ya pili ya hoja yake kuna tofauti ya majina ya mshtakiwa wa pili kwenye hati na maelezo ya mashahidi.

Anasema kwa kuwa upande wa mashitaka ulikuwa na wajibu wa kuomba marekebisho na hawakufanya hivyo, basi Mahakama ione kuwa kasoro hiyo haiwezi kutibika kwa sasa na ni batili.

Hati hiyo ifanyiwe marekebisho na kinyume chake mshtakiwa anaachiwa huru.

Katika shauri hili inadaiwa kuwa, katika hati washtakiwa waliotenda kosa hilo Mei 25, 2016 na baadhi ya mashahidi wameeleza kufahamishwa kifo hicho tarehe 26, 5, 2016 na yanaungwa mkono na kielelezo cha 17 cha upande wa mashitaka.

Hata hivyo, hakuna shahidi anasema Aneth aliuawa tarehe 26, 5 2016 bali wanasema ndio kifo kiligundulika.

Kwa kuwa huu ni ushahidi wa kimazingira na hakuna shahidi aliyeshuhudia tukio la kufa, sikubaliani na hoja ya wakili Nkoko kuwa kuna tofauti ya tarehe ya tukio kwa sababu kinachobishaniwa hapa si tarehe ni muda wa tukio.

Lakini pia, kupitia ushahidi wa shahidi daktari wakati anafanya uchunguzi ameeleza kuwa kifo kimetokea ndani ya saa 24, unaweza kuhitimisha kuwa kilitokea kati ya usiku wa tarehe 25 kuamkia tarehe 26, 2016 ambayo iko ndani ya saa 24.

Katika mazingira ambayo kifo kilitokea usiku wa tarehe 25 kuamkia 26, 2016, mashahidi wote wa upande wa mashitaka ambao kimsingi hawakuona akiuawa wasingeweza kueleza kwa hakika kifo kilitokea lini.

Kwa hiyo, ni uamuzi wa Mahakama hii kuwa pamoja na kwamba kuna tofauti lakini utofauti huo hauwaathiri washtakiwa.

Hata ukiangalia ushahidi wa washtakiwa wote wawili wanaonesha kuwa walielewa.

Hivyo Mahakama hii inaitupilia mbali hiyo hoja.

Kuhusu hoja ya tofauti ya majina, kwa mujibu wa ushahidi wa shahidi namba moja, mbili na namba 22, majina katika hati ya mashitaka ni Revocatus Everist Muyella, ukiachia mbali majina Revocatus Everist Mollel kama inavyoonekana katika hati ya upekuzi, jina la Ray halitajwi popote zaidi ya kwenye maelezo ya onyo.

Ray kwenye hati ya mashitaka lipo kama jina maarufu tu, sioni ni kwa namna gani kuna tofauti ya majina na kama ipo sioni kama inawaathiri washtakiwa.

Kwa maana hiyo naona pia hoja hiyo inakosa mashiko naitupilia mbali.

Kwa hivyo hapakuwepo na haja ya kulazimisha hati ya mashtaka ifanyiwe marekebisho. Kwa maana hiyo natupilia mbali hoja hiyo.

Sasa ninaendelea kuangalia hoja nyingine kama upande wa mashitaka umetimiza wajibu wake kuthibitisha vile viini vitatu.

Kiini cha kwanza, kama kuna kifo.

Kulingana na ushahidi na mashahidi hawa wanashuhudia mwili ukiwa umelala kwenye damu na ulipelekwa Hospitali ya Muhimbili na ulitambulishwa kwa shahidi namba 21 Daktari na Ester Msuya.

Shahidi huyo wa 21 anathibitisha kuwa mwili ule ulikatwa kooni na kutokana na kutenganishwa koromeo hilo kulisababisha marehemu kukosa hewa kwenda kwenye mapafu.

Kutokana na ushahidi mzito uliotolewa na shahidi namba 21 ambaye sina sababu ya kutilia shaka ushahidi wake, Mahakama hii inafikia uamuzi kuwa kini cha kwanza kimethibitishwa kuwa Aneth Msuya alifariki kifo kisicho cha kawaida.

Sasa ninahamia kwenye hoja ya pili kama washtakiwa ndio waliohusika.

Kimsingi ushahidi uliopo ni wa kimazingira tu, ambao uko wa aina tatu. Shahidi wa 25, Getruda anadai aliwaona watuhuniwa na kuwatambua mahakamani.

Ushahidi wa pili ni wa kisayansi na aina ya tatu ni maelezo ya kukiri kutokana na maelezo ya onyo kwa polisi na kwa Mlinzi wa Amani.

Katika fungu la kwanza la ushahidi kwa mujibu wa maelezo ya upande wa mashitaka, unadai kuwa unawanyooshea kidole washtakiwa kuwa pamoja na kwamba hakuna mtu aliyewaona ni wao tu ndio waliotenda kosa hilo, lakini upande wa utetezi unapinga vikali kuwa haina nguvu na unaacha shaka.

Kwa mujibu wa shahidi wa 10, 22 wa upande wa mashitaka, baada ya kubaini mauaji hayo walimtafuta shahidi wa 25 aliyewaelezea alimtaja mshtakiwa wa kwanza kuwa anahusika.

Na mshtakiwa wa kwanza alikiri kuhusika na mauaji hayo na kwamba kupitia maelezo ya kukiri ya mshtakiwa wa kwanza walifanikiwa kumpata mshtakiwa wa pili ambaye mpanguso wake wa kinywa ulifanyiwa uchunguzi na kulinganisha na vielelezo vilivyopatikana eneo la tukio.

Shahidi wa 25 aliweza kuelezea kwa maumbile watu aliokuwa anakutana nao wakimuulizia Aneth, walitumia gari aina ya Land Rover rangi ya Silver na jinsi alivyomkumbuka huyo mwanamke kuwa aliwahi kumuona Mererani.

 Alieleza jinsi walivyomfuata tarehe 18 na kumpelekea simu na kumtishia kwa bastola na wakarudi Mei 23, wakiwa na vijana wengine waliomuahidi pesa endapo angeondoka nyumbani hapo na kuwaacha wafanye kazi yao.

Na alipoulizwa ni kazi gani mshtakiwa wa kwanza alimkemea kuwa hiyo si kazi yake.

Pia, shahidi huyu wa 25 alieleza jinsi alivyoondoka pale nyumbani.


Shahidi huyu alipoitwa kuja kuwatambua watu aliowaona Kibada aliweza kuwatambua mshtakiwa wa kwanza na wa pili.

Wakili Peter Kibatala naye aliushambulia ushahidi huo kuwa si wa kuaminika hasa kuhusiana na utambuzi kuwa utambuzi ulikuwa batili.

Wakili Kibatala alidai kuwa shahidi wa 22 hakuongozwa kutambua saini ya mshtakiwa wa kwanza (katika amaelezo anayodaiwa kukiri kosa).

Pia, wakili Kibatala alidai kuwa shahidi wa 25 aliwasiliana na RCO aliyekuwa mpelelezi wa kesi kabla ya kuja kwenye gwaride la utambuzi jambo linalofanya gwaride hilo la utambuzi kuwa batili.

Nimezingatia kwa kiwango cha hali ya juu maelezo ya pande zote kuhusu suala la utambuzi wa washtakiwa kwa shahidi wa 25.

Suala la msingi ni kama washtakiwa wote waliweza kutambuliwa au la.

 Ni kanuni ya kisheria kila shahidi anapaswa kuaminiwa isipokuwa tu pale uhalali wake utakapokuwa umepingwa au kuonesha kuwa ushahidi wake ulikuwa na nia mbaya, au kukinzana au kupishana kwa kiwango kikubwa na uamuzi mwingine.

Baada ya maelezo hayo, sikubaliani na wakili Nkoko kuwa shahidi huyu hakuweza kueleza ni namna gani aliachana na marehemu, maana alieleza kuwa wakati aliporejesha ufunguo (kwa jirani) saa 10 jioni (wakati shahidi wa 25 anaondoka kwa marehemu).


Jaji ahitimisha kutoa muhtasari wa ushahidi wa pande zote

Jaji Kakolaki amemaliza kutoa muhtasari wa ushahidi wa pande zote na sasa anaanza kuchambua ushahidi huo ili kuelekea katika hitimisho kama washtakiwa wana hatia au la.

Jaji Kakolaki: Kama nilivyosema Mahakama hii ilikaa na waungwana wazee wa baraza waliosikiliza hoja za pande zote mbili Desemba 4, 2023 na Desemba 11, 2023 walitoa maoni yao na wakaona kuwa ushahidi wa mashitaka hautoshi kuwatia hatiani na wakashauri Mahakama iwaachie huru.

Ni Kanuni ya kisheria kuwa upande wa mashitaka ndio una wajibu wa kuthibitisha mashitaka ya jinai upande wa mashitaka kwa kiwango cha kutokuacha mashaka.

Pale upande wa mashitaka unapolalia kwenye ushahidi wa kimazingira kanuni ni kwamba ni lazima uthibitishe kosa pasipo kuacha mashaka.

Katika mashauri ya jinai mashaka tu hata kama yangekuwa madogo kiasi gani hayawezi kutosha kumtia mshtakiwa hatiani.

Kwa hiyo, inategemewa kuwa katika shauri hili, upande mashitaka ulete ushahidi mzito kuwa ni hao washtakiwa wawili tu ndio waliotenda kosa.

Pia, ni kanuni nyingine ya kisheria kuwa washtakiwa hawatatiwa hatiani kwa sababu tu ya udhaifu wa utetezi wao, bali ni kwa uzito wa ushahidi wa upande wa mashtaka.

Katika shauri lolote la jinai na mauaji kuna viini viwili yaani kitendo chenyewe kinachosababisha kosa lililokatazwa kisheria na nia ovu ya kutenda kosa.

Kwa ufupi, ni nia ya kutenda kosa ndiyo inayojenga kosa.

Ili upande wa mashitaka uthibitishe mashitaka yake, kuna vitu vitatu vinapaswa kuthibitisha, kwanza kama kuna mtu alikufa kifo kisicho cha kawaida, mbili, kama ni washtakiwa ndio walitenda kosa hilo na tatu kama walifanya kwa nia ovu.


Utetezi wa mshtakiwa wa pili

Jaji Kakolaki: Shahidi wa mwisho alikuwa ni mshtakiwa wa pili, Revocatus Muyella. Alielezea kukamatwa kwake na jinsi alivyofanyiwa upekuzi na alivyofanyiwa mahojiano na kisha akapelekwa Dar es Salaam.

Alikana kuwa mahali ulikofanyika upekuzi si kwake maana polisi wanadai kuwa walifanya kwa Revocatus Mollel na kwamba hilo si jina lake.

Alidai kuwa Mei 25, 2016 (tarehe ya tukio la mauaji) yeye hakuwepo Dar es Salaam bali alikuwa Arusha na alikana kumuahidi shahidi wa 25 kumpa Sh50 bilioni ili kutekeleza mauaji hayo kama alivyodai ilivyodaiwa na shahidi wa 25.

Alidai hakuwahi kuchukuliwa mpanguso wa mate kwa kuwa mtu anayetajwa kwenye fomu ya uthibitisho wa kuchukuliwa sampuli hiyo si yeye.

Alikana kuhusika na mauaji hayo akisema kuwa hakuna shahidi yeyote aliyethibitisha hilo.

Kuhusu ushahidi wa shahidi wa 15, Dk Segumba aliyefanya uchunguzi wa vinasaba alisema shahidi huyo alishindwa kuthibitisha kuwa kisu hicho kilikuwa na damu ya Aneth Msuya.

Alieleza kuwa yeye anaitwa Revocatus Everist Muyella na kwamba hayo yanayoonekana kwenye hati ya mashtaka ni Revocatus Everest Muyella maarufu kama Ray au Revoo si yake.


Ushahidi kuhusu gari aina ya Ford Ranger

Jaji Kakolaki: Shahidi wa pili wa utetezi alikuwa ni Karim Issa Mruma: Huyu aliieleza Mahakama kuwa alikuwa dereva wa familia ya mshtakiwa wa kwanza.

Alieleza kuwa yeye ndiye alikuwa dereva wa gari aina ya Ford Ranger na kwamba gari hilo ni bovu na ni yeye aliyelipeleka gereji ya CMC Motors tangu Mei 9, 2016 mpaka sasa halijatoka.


Muhtasari utetezi wa mjane wa Bilionea Msuya

Jaji Kakolaki: Shahidi wa kwanza upande wa utetezi alikuwa ni mshtakiwa wa kwanza, Miriam Mrita.

Alieleza alivyokamatwa Arusha na akaletwa Dar es Salaam akiwa amefungwa kitambaa usoni na alivyokuwa akiteswa.

Alieleza kwa urefu tu, kuwa kuna mateso aliyapata akiwa anapigwa na kwamba kipindi chote hicho walikuwa wanataka akubali kosa.

 Alisema baadaye alipelekwa Kituo cha Airport alikokaa mpaka Agosti 23, 2016 akapelekwa mahakamani ndipo akakutana na wakili wake.

Alishangaa jinsi shahidi wa 22, SSP Mhanaya alikopata namba za magari wakati Getruda hakumtajia na gari aina ya Ford Ranger lililotajwa wakati gari hilo lilikuwa gereji tangu Mei 9, 2016 na halijawaji kutoka.

Alikanusha kuwa na ugomvi na Aneth akidai kuwa aliishi naye vuzuri akimlea kama mtoto wake na asingeweza kutumia  meseji zisizofaa za kutukana ( kama upande wa mashitaka ulivyodai) na kwamba kama zingekuwepo polisi wangezileta maana walikuwa na simu zake.

Pia, alikanusha kujimilikisha mali za mirathi ya mumewe na kubadili umiliki lakini pia alieleza aliwagawia hata ndugu wa marehemu mumewe sehemu ya mali, akiwamo marehemu japo hawakuwa wanufaika.

Pia, shahidi huyu alikana ushahidi wa shahidi wa kwanza WP Mwajima kuwa alielekzwa na RCO (Richard Mchomvu) kuwa aandike maelezo yake akisema kuwa hata RCO mwenyewe alikana katika ushahidi wake kumuelekeza kuandika maelezo yake.

Aliiomba Mahakama imuone kuwa hana hatia.

Wakati akiulizwa maswali ya dodoso alikana kuwa hakumbuki kama yeye na mumewe waliwahi kumiliki gari aina ya Rangerover Ivoque, lakini aliporejeshwa kwenye kumbukumbu za TRA usajili wa magari alikubali kuwa mmiliki wa mwisho wa gari hilo.

Kuhusu maelezo yake ya onyo alipinga kuwa hakuwahi kutoa maelezo hayo.


Ushahidi wa 'house girl' wa marehemu

Jaji Edwin Kakolaki: Shahidi wa mwisho upande wa mashtaka ni Getruda Peniel Mfuru. Yeye alikuwa mfanyakazi wa ndani wa marehemu Aneth.

Alieleza jinsi Mei 15, 2016 alivyokutana na gari ya bluu na ndani kulikuwa na mama mmoja mwenye uso wa mviringo na ndani alikuwamo mwanamume na walivyomuita wakamuuliza nyumbani kwa Aneth na yule mwanamke akajitanbulisha kuwa ni ndugu wa Aneth lakini wakamwambia wangerudi Mei 17.

Alieleza kuwa Mei 17 hawakurudi bali walirudi Mei 18, akiwa na huyo mwanamume mrefu mweusi na kwamba siku hiyo huyo mwanamke alimuita akampa simu ya Nokia ya tochi kuwa watakuwa wanawasilia naye tu na akamuonya asimwambie mtu mwingine.

Alieleza kuwa, walimwambia kuwa kuna biashara wanakata kuifanya.

Shahidi alieleza walivyorudi tena Mei 23, wakamuita ndani ya gari ambamo kulikuwa na watu wengine waliokuwa wamevaa majaketi na walikuwa wamevaa soksi kuficha nyuso zao.

Alieleza kuwa, walimuonesha pesa zikiwa kwenye ‘briefcase’ wakamwambia ni Sh50 bilioni na kwamba hizo zote wangempa kama wangekamilisha kazi yao, lakini wakampa kwanza Sh20,000 na wakamtaka Mei 25 asiwepo.

Shahidi huyu alieleza alivyoondoka kwenda kwa rafiki yake Chanika na ile simu akaitupa majini akiwa kwenye pantoni na kesho yake akiwa kwa rafiki  yake huko Chanika ndipo akasikia taarifa kuwa Aneth ameuawa, ndipo akamwelezea rafiki yake huyo.

Alieleza alivyoondoka kwenda kwao (mkoani) na alivyowasiliana na polisi, wakaenda kumchukua wakaja naye Dar es Salaam wakamhoji na baadaye akaenda kuwatambua washitakiwa katika gwaride la utambuzi.

Alipoulizwa maswali ya dodoso alishindwa kuelezea alikwenda kuwatambua washitakiwa katika kituo gani cha polisi wala nyumba aliyokuwa akiishi.

Kwa ufupi huo ndio ushahidi wa upande wa mashtaka.

Jaji Kakolaki amemaliza kurejea muhtasari ushahidi wa upande wa mashtaka na sasa anatoa muhtasari ushahidi wa upande wa wa utetezi akianza na mshtakiwa wa kwanza, Miriam Mrita.

Ushahidi aliyechunguza chanzo cha kifo cha Aneth

Jaji Kakolaki: Shahidi huyu ni shahidi wa 18, Dk Hassan Mbonde aliyefanya uchunguzi wa mwili kujua sababu za kifo.

Alieleza kuwa, marehemu alikufa kutokana na kuvuja damu nyingi iliyosababishwa na jeraha shingoni.

Alieleza kuwa, akifanya kipimo kujiridhisha kama wakati marehemu anakatwa shingo (koromeo) alikuwa hai au alikuwa ameshafariki lakini akabaini kuwa alikatwa akiwa hai.

Pia, alieleza kuwa hakuweza kubaini kama marehemu aliingiliwa.


Mtaalamu wa uchunguzi wa sayansi jinai

Jaji Kakolaki: Shahidi huyu alieleza jinsi alivyokwenda kufanya uchunguzi eneo la tukio ( chumbani kwa marehemu Aneth alikouawa), kwa maelekezo ya RCO, Richard Mchomvu.

Alieleza kuwa ndiye aliyekusanya vielelezo hivyo, yaani kisu, nguo ya ndani na filimbi.

Alisema alichukua kisu kwa kuwa aliona mwili wa marehemu una jeraha na nguo ya ndani ili kujiridhisha kama marehemu (Aneth) alikuwa ameingiliwa kabla ya kuuawa na filimbi alitaka kujua kama kabla ya kuuawa alijaribu kuomba msaada.

Shahidi huyu alieleza kuwa, ndiye alimkabidhi WP Mwaka (Shahidi wa 23) vielelezo hivyo hadi baadaye alipotumwa kwenda kuvichukua na kumkabidhi WP Elitruda ambaye alivipeleka kwa Mkemia (shahidi wa 15).

Hata hivyo, alipoulizwa na mawakili wa utetezi iwapo alichukua alama za vidole katika baadhi ya vitu kwenye eneo la tukio alisema hakuchukua.


Ushahidi wa vinasaba

Jaji Edwin Kakolaki amerejea ushahidi wa shahidi 15 wa upande wa mashtaka, Dk Fidelis Segumba aliyefanya uchunguzi wa kisayansi katika vielelezo vilivyochukuliwa eneo la tukio yaani, nguo ya ndani ya marehemu, filimbi, kisu na mpanguso wa mate kutoka kwa mshtakiwa wa pili, Revocatus  Muyella.

Jaji Kakolaki amesema katika matokeo ya uchunguzi huo, Dk Segumba aliieleza Mahakama kuwa vinasaba katika mpini wa kisu vilioana na vinasaba katika mpanguso wa mate ya mshtakiwa wa pili, Muyella.


Idadi ndogo ya ndugu wajitokeza kusikiliza hukumu ya mjane wa Bilioane Msuya

Wakati Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ikiendelea kusoma hukumu ya kesi ya mauaji inayomkabili mjane wa aliyekuwa mfanyabiashara maarufu wa madini jijini Arusha, Erasto Msuya maarufu kama Bilionea Msuya; Miriam Mrita na mwenzake

Idadi ndogo ya ndugu wa pande zote wamejitokeza kusikiliza hukumu hiyo, tofauti na kesi nyingine, huwa wengi hadi kukosa nafasi ya kukaa.

Leo Ijumaa Februari 23, 2024 ndugu, jamaa na marafiki wa washtakiwa na wale wa upande wa walalamikaji wameweza kuingia wote katika ukumbi namba moja wa Mahakama hiyo na kukaa bila changamoto yoyote ikilinganishwa na kesi kama ya kina Halima Mdee, idadi ya watu ilikuwa kubwa na kushauriwa wengine wakae nje ya chumba cha Mahakama wasubirie uamuzi.

Washtakiwa hao, Miriam na Muyella wanakabiliwa na shtaka moja la mauaji ya kukusudia la mauaji ya Aneth Msuya (wifi wa Miriam) aliyekuwa mdogo wa Bilionea Msuya.


Jaji Kakolaki akitoa muhtasari

Jaji Edwin Kakolaki anaendelea na muhtasari wa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka, kile walichokisema kila mmoja kwa ufupi.

Awali, alirejea ushahidi wa shahidi wa kwanza, WP Mwajima aliyeeleza kuwa ndiye aliyeandika maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa kwanza, Miriam Mrita akidai kuwa alikiri katika maelezo hayo kuhusika na kosa la mauaji ya wifi yake, Aneth Msuya.

Katika muhtasari wa shahidi wa pili, Mlinzi wa Amani, Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Ilala, Reunia Kajumlo amesema shahidi huyo pia aliieleza Mahakama kuwa aliandika maelezo ya mshtakiwa huyo ambako pia alikiri kosa.

Shahidi wa nne, aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kigamboni, Richard Mwaisemba ameieleza namna alivyopata taarifa ya tukio la mauaji hayo kutoka kwa askari wa kituo kidogo cha Kibada.

Amedai kuwa, alifika eneo la tukio na kukuta mwili wa Aneth ukiwa umelala chini kwenye dimbwi la damu kisha akamtaarifu aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Temeke, (SSP) Richard Mchomvu ambaye pia alifika eneo hilo.

Mashahidi hao wawili wamedai kuwa, eneo la tukio pembeni ya mwili walikusanya vielelezo ambavyo ni nguo ya ndani ya marehemu, filimbi na kisu kilichokuwa na damu.


Endelea kufuatilia Mwananchi na mitandao yake kwa habari zaidi.