Heri yasaidia ujenzi wa miundombinu shule ya msingi Funguni

Dar es Salaam.Taasisi ya Heri imekabidhi madarasa mawili na madawati 20 yaliyokarabatiwa, pamoja na madawati mapya 20 katika shule ya msingi Funguni wilayani Pangani, inayokabiliwa na changamoto ya uchakavu wa miundo mbinu.

Shule hiyo inatajwa kukabiliwa na changamoto ya uchakavu wa miundombinu ya madarasa, madawati, vyoo, majiko pamoja na ukosefu wa ukumbi wa chakula kwa wanafunzi na uhaba wa nyumba za walimu huku zile zilizopo zikiwa zinavuja nyakati za mvua na hazina maji wala umeme.

Mkuu wa Shule hiyo, Flora Mayaka ameeleza namna msaada wa taasisi ya Heri ulivyokuwa wa kipekee na kuwapa faraja, licha ya changamoto hizo za miundombinu shuleni hapo.

"Leo ni siku ya kipekee kwa shule yetu, msaada huu si tu kwamba utawapa wanafunzi wetu mazingira mazuri ya kujifunzia bali pia msukumo wa ndoto kubwa na kufikia uwezo wao kamili," amesema.

Mkuu wa wilaya ya Pangani, Zainab Abdallah amesema dhamira ya taasisi ya Heri katika kuleta maendeleo ya elimu wilayani hapo ni mwanga kwa ustawi wa elimu.

"Naishukuru na kuipongeza sana Heri Foundation (Taasisi ya Heri) kwa moyo wenu wa kujitoa kuja kuunga mkono maendeleo ya elimu wilayani Pangani, nawaomba muendelee na moyo huu na muwe walezi wa shule ya msingi Funguni," amesema.

Mkurugenzi mtendaji wa taasisi hiyo, Susan Ngole amesema dhamira ya shirika hilo ni kuboresha mazingira ya elimu na kuunga mkono juhudi za Serikali.

"Tumekabidhi madarasa na madawati haya ambayo kabla yalikuwa katika hali mbaya yasiyoweza kutumika," amesema.

Diwani wa Kata ya Pangani Mashariki, Akida Boramimi amesema umuhimu wa ushirikiano wa taasisi za wadau wa elimu na jamii katika kuinua elimu.

"Mchango huu ni matokeo ya juhudi za pamoja za Serikali na taasisi kama HERI Foundation, inatia moyo kushuhudia mashirikiano kama haya yanafanya kazi kwa lengo moja," amesema diwani huyo.