HESLB yafungua dirisha rufaa mikopo elimu ya juu

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru
Muktasari:
- Dirisha hilo la rufaa kwa wanafunzi ambao hawakuridhika na viwango vya mikopo walivyopangiwa limefunguliwa rasmi leo Jumapili, Novemba 13, 2022 litafungwa Jumapili ijayo.
Dar es Salaam. Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imefungua dirisha la rufaa kwa wanafunzi ambao hawakuridhika na viwango vya mikopo walivyopangiwa kuwasilisha taarifa za uthibitisho ili kuongezewa viwango vya mikopo kulingana na uhitaji wao.
Taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru iliyotolewa leo Jumapili, Novemba 13, 2022 imesema dirisha hilo la rufaa litakuwa wazi kwa siku saba kuanzia leo hadi Jumapili ijayo.
Bodi hiyo imesema kuwa hadi kufikia leo tayari wanafunzi 68,422 wa mwaka wa kwanza wameshapangiwa mikopo.
“Hadi leo Novemba 13, 2022, tumeshawapangia mikopo wanafunzi wa mwaka wa kwanza wapatao 68,422 na tunafahamu kuwa kuna wanafunzi ambao kwa sababu mbalimbali, hawakukamilisha nyaraka muhimu kuthibitisha uhitaji wao, dirisha la rufaa ni fursa kwao,” amesema Badru katika taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa Badru, lengo ni kutoa mikopo kwa wanafunzi wapya 71,000 katika mwaka wa masomo 2022/2023 na kuwasihi wanafunzi wanaowasilisha rufaa kusoma na kuzingatia maelekezo yaliyopo kwenye mfumo wa kuwasilisha rufaa.
Taarifa hiyo imeeleza fedha za wanafunzi waliopata mikopo hiyo zilianza kutumwa vyuoni hata kabla ya wanafunzi kufika vyuoni na kuwa kazi hiyo ni endelevu na kuwashauri wanafunzi waliopangiwa mikopo kufika kwa maofisa mikopo wa vyuo vyao ili kukamilisha taratibu za kupokea fedha.
“Pale mwanafunzi anapoona amepangiwa mkopo kupitia yake ya SIPA (Student’s Individual Permanent Account), basi afike kwa ofisa mikopo wa chuo chake ambaye yupo palepale chuoni ili awasilishe taarifa zake za benki na kupokea fedha,” amesema Badru.
Badru amezishukuru taasisi za elimu ya juu na serikali za wanafunzi kwa ushirikiano wanaoipatia HESLB ambao umeendelea kuimarisha ufanisi katika kuwahudumia wanafunzi wanaonufaika na mikopo ya elimu ya juu inayotolewa na Serikali kupitia HESLB.
“Kwenye huu mnyororo wa kuwahudumia wanafunzi, uongozi wa vyuo, serikali za wanafunzi na jumuiya yao ya TAHLISO ni wadau muhimu … na wamekuwa wakitupatia ushirikiano mkubwa, tunawashukuru sana,” amesema Badru.
Ijumaa Novemba 11, 2022, wakati wa hotuba yake ya kuahirisha mkutano wa tisa wa Bunge la 12, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia wanafunzi 28,000 waliokidhi vigezo vya kupata mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka 2022/2023, waende vyuoni kuendelea na usajili chini ya uratibu wa Wizara ya Elimu wakati taratibu muhimu zikikamilishwa.
“Lengo la Rais ni kuwanufaisha wanafunzi wote wenye uhitaji, waliopata udahili na wenye vigezo vya kupata mikopo. Katika mapitio ya bajeti ya nusu mwaka baadaye mwaka huu tutaliomba Bunge lako tukufu liridhie matumizi ya fedha zitakazohitajika,” alisema Majaliwa.
Kauli hiyo ya Majaliwa ilikuja siku chache baada ya mjadala kuibuka bungeni wa kujadili hoja ya mbunge wa Biharamulo (CCM), Ezra Chilewesa kuliomba Bunge kuahirisha shughuli zake zilizopangwa kwa muda, ili kujadili tatizo la wanafunzi kukosa mikopo ya elimu ya juu.
Hoja hiyo iliungwa mkono na wabunge na Spika, Dk Tulia Ackson alitoa nafasi ijadiliwe na hatimaye Bunge liliazimia wanafunzi hao wawezeshwe kuendelea na masomo.
Hata hivyo, Majaliwa aliwashukuru wabunge kwa kuibua hoja zenye lengo la kuboresha utendaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), pamoja na mfumo mzima wa ugharamiaji, upangaji, utoaji na urejeshaji wa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu nchini.