Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali yakubali yaishe mikopo elimu ya juu

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasilisha hoja ya kuahirishwa kwa mkutano wa tisa wa Bunge jijini Dodoma, juzi. Picha na Erick Boniphace

Muktasari:

  • Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia wanafunzi 28,000 waliokidhi vigezo vya kupata mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka 2022/2023, waende vyuoni kuendelea na usajili chini ya uratibu wa Wizara ya Elimu wakati taratibu muhimu zikikamilishwa.

Dodoma. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia wanafunzi 28,000 waliokidhi vigezo vya kupata mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka 2022/2023, waende vyuoni kuendelea na usajili chini ya uratibu wa Wizara ya Elimu wakati taratibu muhimu zikikamilishwa.

Kauli ya Rais Samia imekuja wakati Bunge likiazimia wanafunzi wenye vigezo vya kupata mikopo ya elimu ya juu ambao hawajaipata mpaka sasa, Serikali iangalie namna ya kuwawezesha kupokelewa vyuoni, ili waendelee na masomo yao wakati Serikali ikitafuta fedha ya mkopo kwa ajili ya wanafunzi hao.

Majaliwa alitoa uamuzi huo wa Rais Samia juzi, kwenye hotuba yake ya kuahirisha mkutano wa tisa wa Bunge la 12, lililoahirishwa hadi Januari 31, mwakani.

“Lengo la Rais ni kuwanufaisha wanafunzi wote wenye uhitaji, waliopata udahili na wenye vigezo vya kupata mikopo. Katika mapitio ya bajeti ya nusu mwaka baadaye mwaka huu tutaliomba Bunge lako tukufu liridhie matumizi ya fedha zitakazohitajika,” alisema.

Hata hivyo, Majaliwa aliwashukuru wabunge kwa kuibua hoja zenye lengo la kuboresha utendaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), pamoja na mfumo mzima wa ugharamiaji, upangaji, utoaji na urejeshaji wa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu nchini.

Hatua hiyo ilikuja baada ya mbunge wa Biharamulo (CCM), Ezra Chilewesa kuliomba Bunge kuahirisha shughuli zake zilizopangwa kwa muda, ili kujadili tatizo la wanafunzi kukosa mikopo ya elimu ya juu.

Hoja hiyo iliungwa mkono na wabunge na Spika, Dk Tulia Ackson alitoa nafasi ijadiliwe na hatimaye Bunge liliazimia wanafunzi hao wawezeshwe kuendelea na masomo.

“Nyote mtakubaliana nami kwamba lengo la mjadala huo, lilikuwa ni kutafuta suluhu ya suala la wanafunzi takribani 28,000 wenye uhitaji wa kupata mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka 2022/2023, ambao walikuwa hawajapangiwa kutokana na ukomo wa kibajeti,” alisema.


Mishahara ya watumishi

Majaliwa pia alisema taasisi za umma 455 zimeunganishwa na zinatumia mfumo mpya wa taarifa za kiutumishi na mishahara, ili kupunguza muda wa kuchakata malipo ya mishahara kutoka siku 14 hadi siku moja pamoja na kuwa na taarifa sahihi za watumishi wanaotarajia kustaafu.

Akizungumzia utendaji kazi na uwajibikaji wa watumishi wa umma, alisema Serikali imeendelea kuboresha, kuimarisha na kuweka mifumo imara ya usimamizi wa rasilimali watu na utendaji kazi wa watumishi na taasisi za umma.

Majaliwa alisema lengo ni kuhakikisha kuwa mifumo iliyopo na inayojengwa inasaidia kuharakisha utendaji kazi na usimamizi wa watumishi na inakuwa na taarifa sahihi ili kuongeza tija na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Alisema mfumo huo mpya ulioanza kutumika rasmi Mei 2021, umeunganishwa na mfumo wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), kwa ajili ya kubadilishana taarifa za michango ya watumishi na nyaraka za hitimisho la ajira.

Majaliwa alisema pia umeunganishwa na mfumo wa HESLB kwa ajili ya kubadilishana taarifa za mikopo ya elimu ya juu kwa watumishi; mfumo wa ajira portal kwa ajili ya kubadilishana taarifa za waajiriwa wapya na mfumo wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), kwa ajili ya kubadilishana taarifa za utambulisho wa Taifa wa watumishi.

Aliitaja mifumo mingine kuwa ni Mfumo wa Kusimamia Utendaji Kazi wa Watumishi wa Umma (PEPMIS) na Mfumo wa Kusimamia Utendaji Kazi wa Taasisi za Umma (PIPMIS).

“Ujenzi wa mifumo hiyo mipya umekamilika. Hivi sasa inafanyiwa majaribio na inatarajiwa kuanza baada ya kukamilika kwa majaribio na kutoa mafunzo kwa watumishi katika taasisi zote za umma,” alisema.

Alisema hatua ya mifumo hiyo kuwa ya kielektroniki itaondoa muhali, hisia za kupendeleana au kuoneana katika usimamizi wa utendaji kazi, pia itahamasisha uwajibikaji wa hiari wa watumishi wa umma itakayosaidia utoaji huduma bora na kwa wakati kwa Watanzania.