Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hii ndio safari ya milima, mabonde ya Rais Samia Suluhu Hassan

Hii ndio safari ya milima, mabonde ya Rais Samia

Muktasari:

  • Samia Suluhu Hassan ameandika historia ya kuwa Rais wa sita wa Tanzania akiwa ni mwanamke wa kwanza Tanzania kushika nafasi hiyo kufuatia kifo cha mtangulizi wake, John Magufuli. Kulingana na mahojiano aliyofanya kwa nyakati tofauti na vyombo mbalimbali vya habari, kuna ishara mama huyu hakuwahi kufikiria kushika wadhifa aliopata.



Dar es Salaam. Samia Suluhu Hassan ameandika historia ya kuwa Rais wa sita wa Tanzania akiwa ni mwanamke wa kwanza Tanzania kushika nafasi hiyo kufuatia kifo cha mtangulizi wake, John Magufuli. Kulingana na mahojiano aliyofanya kwa nyakati tofauti na vyombo mbalimbali vya habari, kuna ishara mama huyu hakuwahi kufikiria kushika wadhifa aliopata juzi.

Akiwa Makamu wa Rais alikaririwa akisema alikuwa anaamini ipo siku Tanzania inaweza kuwa na Rais mwanamke, lakini hakufikiria mwanamke huyo anaweza kuwa yeye kutokana na ugumu wa kazi hiyo aliouona kwa mtangulizi wake.

“Urais sio jambo jepesi, kwa muda niliofanya kazi kama Makamu wa Rais nafahamu kazi za Rais, nafahamu majukumu mazito aliyonayo, binafsi ukiniambia kuhusu urais lazima nifikirie mara sita sita, sio kwamba siwezi ila najua jukumu ni zito,” alisema Samia katika mahojiano aliyowahi kufanya na TBC.

Akihojiwa na televisheni moja ya mtandaoni (jina tunalo), mama huyu anasimulia safari yake ilianza mwaka 1975 alipohitimu kidato cha nne na kupangiwa kwenda Ofisi Kuu ya Maendeleo visiwani Zanzibar akiwa na umri wa miaka 16.

Kutokana na umri wake kuwa mdogo alirudishwa nyumbani hadi mwaka uliofuata ndipo alipokwenda kuanza kazi rasmi kama Ofisa Masijala, kazi aliyodumu nayo kwa miaka mitatu.

“Nilifanya kazi ile kwa miaka mitatu lakini ilikuwa kama niliowakuta nawaongoza mimi, wakubwa wakitaka kitu wanauliza Samia yuko wapi na kueleza mahitaji yao,” alisema na kuongeza:

“Wenzangu kwenye idara wakawa wanaona kama shawishi (wanajiuliza), inakuwaje kila kitu niulizwe mie, nikahisi hapa nilipo si sahihi nahitaji kuwa mahali pengine,” anasimulia zaidi Samia kwenye video hiyo.

Mawazo hayo inaaminika yalimfanya Samia kuanza kusoma kozi ya takwimu kwa ngazi ya cheti, kisha kozi ya utawala ngazi ya cheti pia, na ili kupandisha sifa zake alikwenda kujiunga na kozi ya astashahada ya uongozi wa umma katika Chuo cha IDM kwa miaka mitatu.

Samia katika mahojiano hayo alisimulia kuwa mwaka 1987 alirejea ofisini kwake na kupanda cheo kuwa ofisa mipango, lakini alikuta mambo yanaenda taratibu kama alivyoacha, jambo ambalo anadai hakulipenda.

Akiwa anaendelea kuitumikia nafasi hiyo ndani ya miaka miwili akaona imetangazwa nafasi ya kazi Shirika la Chakula Duniani (WFP) tawi la Zanzibar, aliomba na kufanikiwa kupata ambapo aliifanya kwa miaka tisa.

“Niliporudi Serikalini ninakona watu wanakwenda `too slow’ (taratibu) nikachomoka nikaenda kwenye asasi za kiraia, nikawa kiongozi wa asasi hizo pale Zanzibar,” alisena na kufafanua:

“Ilikuwa ngumu kwa sababu ilikuwa taasisi changa na hatuna fedha, nikapambana kuongoza hivyo hivyo, ubunifu wangu ukaniwezesha kuandika mradi tukapata fedha mambo yakawa mazuri sasa. Baada ya fedha kupatikana maneno yakaanza nikaona isiwe shida nikaacha,” alisema.

Rasmi kwenye siasa

Baada ya kuachana na asasi za kiraia, Samia akahamishia mawazo yake kwenye siasa, wakati wote huo alikuwa mwanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) lakini hakuwahi kuwa kiongozi.

Mwaka 2000 akajitosa rasmi katika ulingo wa siasa kwa kuwania viti maalumu kwenye Baraza la Wawakilishi.

“Niliingia kwenye siasa sio kwa matamanio wala utashi. Nilikuwa naona namna wapinzani walivyokuwa na nguvu kwenye Baraza la Wawakilishi, pia mawaziri walikuwa wanajibu ndivyo sivyo, jambo lile lilikuwa linanikereketa.

Hii ndio safari ya milima, mabonde ya Rais Samia Suluhu Hassan

“Nikasema ngoja na mimi nitaingia huko nikapambane na wapinzani na hawa mawaziri wanaojibu ndivyo sivyo nikawasute, shida ikawa sijui naingiaje,” alisema Samia, ambaye ni mtu wa pili kutoka Zanzibar kupata urais wa Tanzania. Aliuliza na kuelekezwa na kuwania uwakilishi kwa viti maalumu.

Baada ya kupata viti maalumu na kuishia kuwa mjumbe wa baraza, aliteuliwa kuwa waziri katika Serikali, nafasi aliyoitumikia kwa miaka mitano hadi mwaka 2005, aliwania tena viti maalumu na kuteuliwa kuwa Waziri wa Utalii, Biashara na Uwekezaji. Mwaka 2010 akagombea ubunge wa jimbo la Makunduchi.

“Hapo ndipo nilipoona joto ya jiwe, mwanamke nilikuwa peke yangu na jina la kwanza nikapachikwa jina la `kigego’. Nilipofika jimboni nikajifunza mila na desturi, nakumbuka nilikuwa sijifungi ushungi, nikanong’onezwa jitande,” anasimulia Samia.

Samia alipiga kampeni, ambapo alieleza anachotaka kufanya kwenye jimbo hilo na hatimaye akashinda. Baada ya uchaguzi huo aliteuliwa kuwa Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais kushughulikia Muungano.

Hii ndio safari ya milima, mabonde ya Rais Samia

Mwaka 2014 alichaguliwa kuwa makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba lililoandaa Rasimu ya Katiba Mpya akimsaidia Samuel Sitta.