Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hiki hapa kinachodaiwa kumponza Katibu Mkuu Wizara ya Maji

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Nadhifa Kemikimba

Dar es Salaam. Siku tatu baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutengua uteuzi wa Nadhifa Kemikimba kama katibu mkuu Wizara ya Maji, kinachodaiwa kumponza kimewekwa wazi mitandaoni.

Kemikimba amehudumu katika nafasi hiyo kwa siku 173 kuanzia Februari 26, mwaka huu hadi Agosti 18, uteuzi wake ulipotenguliwa.

Taarifa ya kutenguliwa kwenye wadhifa huo, ilitolewa juzi na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais-Ikulu, Zuhura Yunus lakini haikueleza sababu za kutenguliwa kwake.

Licha ya taarifa hiyo kutoeleza sababu, kipande cha video cha dakika 4:13 kinachosambaa kwa mitandaoni kikionyesha tukio la Agosti 4 mwaka huu linalomuhusisha Kemikimba, kinadaiwa kuwa huenda ikawa ndiyo sababu.

Video hiyo ilirekodiwa katika kikao kazi cha kufungua mwaka mpya wa fedha cha wafanyakazi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa), kilichohudhuliwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Maji, Jumaa Aweso na Kemikimba.

Kipande hicho kinamwonyesha Kemikimba akihamaki baada ya kupelekewa kikaratasi wakati akizungumza na kumtaka ahitimishe hotuba yake, jambo ambalo hakulikubali.

Mara baada ya kupokea kikaratasi hicho kilichotoka mbele ya meza kuu, alikisoma kisha akakitupa upambe wa kushoto kwake ilipokuwa meza kuu yenye viongozi mbalimbali akiwemo mgeni rasmi, Waziri wa Maji na Mwenyekiti wa Bodi ya Dawasa, Jenerali mstaafu, Davis Mwamnyange.

Pia, kikao hicho kilichofanyika Agosti 4 mwaka huu katika ukumbi wa Diamond Jubilee, kilihudhuriwa na naibu katibu mkuu wa wizara hiyo, Cyprian Luhemeja na Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Kiula Kingu.

“Nyinyi watu wa Human Resource (rasilimali watu) mfanye kazi yetu, haiwezekani mimi naongea hapa, mtu ananiletea kinote na kama ingekuwa hivyo msingetuita, mngefanya kikao chenu wenyewe

“Mimi sipendi insubordination (dharau), sipendi insubordination. Mimi natoa maagizo ya sekta…Mheshimiwa waziri (Aweso) nakuheshimu wewe, namheshimu mwenyekiti wa bodi, otherwise (vinginevyo) ningeondoka, siwezi,” alisema Kemikimba.

Baada ya kimya cha sekunde kadhaa, Kemikimba alikatisha hotuba yake na kumkaribisha Waziri Aweso, kisha akarudi kukaa sehemu yake.

Kipande hicho cha video kinamwonyesha Waziri Aweso akijaribu kumsihi Kemikimba awasamehe watendaji ‘walimkosea’ kwa sababu yeye ndiye katibu mkuu wao na kwamba kama kiongozi anatakiwa kuwa na ngozi ngumu.

“Mama yangu, Mama Nadhifa Kemikimba, uongozi ni jalala, wakati mwingine vijana wetu wanapatia na wakati mwingine kuna maeneo wanakosea. Kwa niaba yao, nikuombe sana radhi kwa kilichoteka,” alisema Aweso na kumtaka aende kuzungumza, hata hivyo alikataa.

Waziri Aweso aliwaomba watu wote ukumbini kusimama kuomba radhi kwa kile kilichotokea, lakini kipande hicho cha video cha dakika 4:13 kinamwonesha Kemikimba akitikisa kichwa kuashiria kukataa.

Mmoja wa viongozi wa Dawasa aliyekuwepo ukumbini akishuhudia tukio hilo, alilieleza Mwananchi kuwa “lile tukio si la kawaida aise, halafu licha ya sisi kusimamishwa kuomba radhi alikataa, lakini kubwa zaidi aliondoka ukumbini hata kabla ya waziri (Aweso) kuondoka.”

Kiongozi huyo aliyeomba hifadhi ya jina lake alisema, “kuna shida sehemu. Kuchukua ki-note na kukitupa ni dharau, kuombwa msamaha na ukumbi mzima, unakataa, kuna shida sehemu.”

Alipotafutwa na Mwananchi kwa simu jana kuzungumzia kilichotokea kwenye kikao kikihusishwa na kutenguliwa kwake kwenye nafasi hiyo, Kemikimba alihoji, “sasa kwani hiyo ni habari?”

Alipoelezwa kuwa ni tukio ambalo limeibua mijadala mitandaoni na wengine wakidhani kuna shida, yeye alijibu kwa kifupi, Kemikimba aliyeteuliwa kuwa katibu mkuu akitoka kuwa naibu katibu mkuu wa wizara hiyo alijibu kwa kifupi, “hakuna shida na wala hiyo si habari.”

Wakati yeye akisema hivyo, wasomi na wadau wa siasa na utawala wamependekeza kuundwa kwa mfumo wa utatuzi wa migogoro baina ya viongozi wa juu serikalini na watendaji wao ili kutoathiri shughuli za Serikali katika sekta au maeneo husika.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Dk Paul Loisulie alisema anaamini kwamba kuna mambo mengine nyuma ya kilichotokea ukumbini kwa sababu kwa namna alivyokasirika, huenda kuna mambo mengine yalikuwa hayaendi vizuri.

Alisema Kemikimba alipaswa kujua yeye ni kiongozi wa umma na anamwakilisha Rais, kwa hiyo alipaswa kujua kwamba chochote anachokifanya anamwakilisha Rais kwa kuwa akifanya vibaya watu watamlaumu Rais aliyemteua.

“Kwa kweli attitude (mtazamo) aliyoionyesha ni mbaya, lakini pia huwezi kujua, pengine kuna mambo mengine zaidi ya tunayoyaona kwenye clip (video) kwa sababu mpaka amefika hapo, huenda kuna mambo mengine yalikuwa hayaendi vizuri,” alisema Dk Loisulie.